1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaHong Kong

Kesi kubwa zaidi ya "usalama wa taifa" yaanzishwa Hong Kong

6 Februari 2023

Wanaharakati wanaounga mkono demokrasia huko Hong Kong wamefikishwa mahakamani Jumatatu katika kesi kubwa zaidi chini ya sheria ya usalama wa taifa iliyowekwa na China ili kukandamiza upinzani.

https://p.dw.com/p/4N9PU
China | Prozess Pro-Demokratie Aktivisten Hongkong
Picha: Tyrone Siu/REUTERS

Hii ni kesi kubwa zaidi chini ya sheria hiyo ya usalama wa taifa ambapo makumi ya watu wanaounga mkono demokrasia wanatuhumiwa kujaribu kuipindua serikali. Washtakiwa 47, ambao ni pamoja na baadhi ya wanaharakati mashuhuri wa jiji hilo, wanakabiliwa na kifungo cha maisha jela iwapo watapatikana na hatia.

Washtakiwa 18 wanakabiliwa na kifungo cha maisha jela iwapo watapatikana na hatia chini ya sheria hiyo ya usalama wa taifa ambayo wakosoaji wanasema inakandamiza uhuru ulioahidiwa wakati Hong Kong iliporejea chini ya mamlaka ya China mwaka 1997, na hadhi yake kama kituo cha biashara duniani.  

Washtakiwa 16 wamekana mashtaka ya kula njama ya kuipindua serikali katika uchaguzi usio rasmi huku wengine 31 wakikiri mashtaka na watahukumiwa baada ya kesi hiyo.

Soma zaidi:Chow Hang-tung afungwa miezi 15 jela Hong Kong 

China | Prozess Pro-Demokratie Aktivisten Hongkong
Watu wakiandamana nje ya Jengo la Mahakama huko Hong Kong 06.02,2023Picha: Anthony Kwan/AP Photo/picture alliance

Maandamano ya nadra na yaliyoitikiwa na watu wachache yalizuka kabla ya mahakama kuitishwa, licha ya kuwepo kwa idadi kubwa ya polisi. Mwanaume mmoja alionekana akiinua mkono na ishara ya ngumi kuonesha mshikamano.

Washtakiwa wanadai kuteswa kutokana na masuala ya kisiasa huku mashirika ya kutetea haki za binadamu na waangalizi wakisema kesi hiyo inadhihirisha ni jinsi gani mfumo wa sheria unavyotumika kukandamiza upinzani uliosalia.

Mada inayohusiana: 

Uhuru wa Hong Kong mashakani miaka 25 baadae

Wengi wa washtakiwa hao tayari wamekaa karibu miaka miwili gerezani. Kwa sasa wanakabiliwa na kesi inayotarajiwa kudumu zaidi ya miezi minne, ikisimamiwa na majaji waliochaguliwa na serikali.

Wanaharakati walaani keshi hiyo

Chan Po-ying, mwanaharakati mkongwe anayeunga mkono demokrasia na mke wa mshtakiwa  Leung Kwok-hung, ameungana na wafuasi waliokuwa wamebeba bango lililosomeka kuwa ni ukandamizaji usio na aibu. Po-ying amesema:

"Kushiriki katika uchaguzi sio kosa. Haya ni mateso ya kisiasa na tunatoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa wafungwa wote wa kisiasa."

Waliofikishwa mahakamani wanawakilisha sehemu mbalimbali za upinzani wa Hong Kong na wana umri kati ya miaka 24 na 66 , wakiwemo wanaharakati Joshua Wong na Lester Shum, profesa Benny Tai na wabunge wa zamani Claudia Mo na Au Nok-hin.

Kesi hii ni kubwa zaidi chini ya sheria ya usalama wa taifa, ambayo China iliweka Hong Kong baada ya maandamano makubwa ya kudai demokrasia mnamo mwaka 2019 ambayo yalizusha vurugu. Sheria hiyo ambayo hutumiwa dhidi ya wanafunzi, wanachama wa vikundi vya wafanyakazi na waandishi wa habari, imesababisha madadiliko kwa raia wa jiji hilo waliyokuwa na desturi ya kujieleza kwa uwazi.