1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chow Hang-tung afungwa miezi 15 jela Hong Kong

Amina Mjahid
4 Januari 2022

Mahakama ya Hong Kong imemhukumu kifungo cha miezi 15 jela mwanaharakati mashuhuri mjini humo Chow Hang-tung kwa uchochezi na kuandaa mkesha uliopigwa marufuku wa kila mwaka wa kukumbuka mauaji Tiananmen mwaka 1989

https://p.dw.com/p/458rL
China I Politik I Hongkong I Chow Hang-tung
Picha: Rafael Wober/AP/picture alliance

Jaji Amy Chan aliyetoa hukumu hiyo amesema uchochezi uliofanywa na Chow wa kuyakusanya makundi ya watu ulihatarisha afya ya Umma huku akisema sheria haimruhusu yeyote kuwa huru kufanya mambo ya uvunjifu wa sheria hizo.

Mwanaharakati huyo aliyekuwa naibu mwenyekiti wa kundi la Muungano wa Hong Kong lililowajumuisha wanaharakati wengi lililopigwa marufuku mwezi Septemba mwaka jana, amesema hana hatia na kile alichokifanya ni kujaribu kuwashinikiza watu kutosahau Juni 4 wala sio kuchochea mikusanyiko.

soma zaidi: Hong Kong: Wahariri wawili washtakiwa kwa uchochezi

Akibubujikwa na machozi Chow aliiambiwa mahakama kwamba nafasi ya wazi ya kuzungumzia kile kilichotokea Juni 4 huenda ikapotea kabisa, akisema udhalimu ni uchoyo na msitari mwekundu utazidi kutanuka.

Chow ambaye pia ni wakili alikamatwa mwaka jana kufuatia jumbe zake mbili alizoziandika mtandaoni siku moja kabla ya Juni 4 ambayo ni siku ya kuwakumbuka waliouwawa katika uwanja wa Tiannmen mwaka 1989.

Makosa yake yanahusiana na jumbe hizo, moja iliyokuwa na ujumbe huu"kuwasha mshumaa sio uhalifu, tusimamie tunachokiamini" na nyengine ni nakala iliyochapishwa katika gazeti inayosema "kuwasha mishumaa kunatubebesha dhamana na watu wa Hong Kong wanaumia kwa kusema ukweli"

Chow pia anakabiliwa na makosa ya kuyumbisha usalama wa kitaifa chini ya sheria mpya ya Hong Kong. Muungano wa Hong Kong ni miongoni mwa mashirika mengi yaliokuwa yanachunguzwa na baadae kupigwa marufuku kwa kisingizio cha kuwa vibaraka wa maafisa wa kigeni.

Sheria mpya ya usalama wa kitaifa yawaweka wengi hatiani

Hong Kong Ivan Lam Joshua Wong Aktivisten
Wanaharakati Joshua Wong na Ivan Lam walipokamatwa mjini Hong KongPicha: Kin Cheung/AP/picture alliance

China inaendelea kuwakamata wanaharakati baada ya kupitisha sheria mpya iliyo na utata ya usalama wa kitaifa mwaka 2020 iliyopunguza makali ya mahakama za Hong Kong. Tayari China imewaandama na kuwakamata watu wanaotetea uhuru wa kujieleza na wale wanaodai demokrasia katika mji huo unaotawaliwa na Beijing.

Katika miaka iliyopita, maelfu ya watu walishiriki mkesha huo kuwakumbuka watu waliouawa baada ya kufyatuliwa risasi na polisi, katika maandamano ya kudai demokrasia yaliyoandaliwa na wanafunzi nchini China mwaka 1989.

soma zaidi: Mataifa ya G7 yalaani kuvurugwa kwa demokrasia ya Hong Kong

Kwa miaka miwili, polisi ilipiga marufuku mkusanyiko wa watu kushiriki kumbukumbu hiyo kwa madai ya kitisho cha virusi vya corona. Lakini baada ya maandamano makubwa ya kudai demokrasia mwaka 2019, wanaharakati wengi waliiona marufuku hiyo kama njia moja ya kuwanyamazisha wapinzani wa Beijing. Hata hivyo serikali imekanusha madai hayo.

Licha ya marufuku hiyo maelfu waliwashaa mishumaa mjini Hong Kong mwaka 2020 na makundi mengine machache yakafanya vivyo hivyo mwaka 2021. 

Chanzo: afp/ap