1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Hong Kong: Wahariri wawili washtakiwa kwa uchochezi

Angela Mdungu
30 Desemba 2021

Wahariri wawili waandamizi wa shirika la habari la Stand News mjini Hong Kong wamefunguliwa mashtaka mapema leo kwa tuhuma za kufanya njama za uchochezi.

https://p.dw.com/p/44zvJ
Polizisten durchsuchen das Büro des Online-Magazins Stand News in Hongkong
Picha: Vincent Yu/AP/picture alliance

 Wahariri hao walikamatwa jana Jumatano baada ya polisi kuvamia ofisi za shirika hilo. Polisi wa usalama wa taifa wamesema wamewashitaki wahariri hao wawili huku kila mmoja akikabiliwa na tuhuma za kuchapisha habari za uchochezi. Hata hivyo polisi hawakutaja majina ya wahariri hao, ingawa vyombo vya habari vya ndani ya Hong Kong vimeyatambua majina yao kuwa ni Chung Pui-Kuen na Patrick Liam waliokuwa wahariri wa jarida la habari la mtandaoni la Stand News .

Kauli ya polisi imeongeza kuwa watalishtaki shirika hilo la habari kwa tuhuma za  uchochezi. Akizungumzia kukamatwa kwa wahariri hao, kiongozi wa Hong Kong Carrie Lam, amesema anaheshimu waandishi wa habari lakini akatahadharisha kuwa kama mtu akivunja sheria na akijifanya kuwa mwanahabari, basi mamlaka hazina budi kulitazama hilo na kuwa na uwezo wa kusema ni nini hasa kinachoendelea na kwamba vyombo vya sheria vinapaswa kuchukua hatua.

Mashirika ya kutetea vyombo vya habari na baadhi ya mataifa ya Magharibi yamekosoa hatua ya uvamizi wa ofisi hizo na kukamatwa kwa wahariri na kusema hiyo ni ishara ya kuendelea kuingiliwa kwa uhuru wa habari tangu China ilipoipitisha sheria ya usalama wa taifa kwa ajili ya Hong Kong mwaka uliopita.

Hongkong | PK Carrie Lam
Kiongozi wa Hong Kong, Carrie LamPicha: Tyrone Siu/REUTERS

Katika hatua nyingine, China hii leo imelaani vikali ukosoaji unaoelekezwa kwa hatua ya kukamatwa kwa waandishi saba wa Hong Kong baada ya Marekani, Canada na Umoja wa Ulaya kuikosoa hatua hiyo.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa China Zhao Lijian katika mkutano wake na waandishi wa habari alisema kuwa baadhi ya mataifa ya kigeni yamekuwa yakitoa maoni yasiyoonesha uwajibikaji kuhusu vyombo sheria vya Hong Kong chini ya mwamvuli wa uhuru wa habari.  Lijian ameongeza kuwa hali hiyo inaleta mkanganyiko wa kile kilicho sahihi na kisicho sahihi na hilo linaupotosha umma.