Kenya kuwa na mawasiliano bora ya simu kuanzia mwaka 2008. | Masuala ya Jamii | DW | 01.08.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Kenya kuwa na mawasiliano bora ya simu kuanzia mwaka 2008.

Badala ya Bangalore nchini India, inawezekana wateja wa benki katika mataifa tajiri wakazungumza na wafanyakazi wa mjini Nairobi mwaka ujao. Kenya ambayo inakwazwa na mawasiliano duni katika shughuli za kuzungumza kwa simu na wateja hivi sasa duniani kote, inaweka matumaini yake katika uwekaji wa waya maalum wa matumizi ya internet na simu, katika Afrika mashariki utakaowekwa ifikapo katikati ya mwaka 2008 ambao unaimarisha hadhi yake kama nchi yenye uchumi imara katika eneo hilo.

Wafanyabiashara wengi nchini Kenya wanamatumaini kuwa hatua hiyo, pamoja na kuwa na gharama nafuu za wafanyakazi, lafudhi nzuri ya Kiingereza, pamoja na kuchoshwa kwa wateja na vituo vya huduma ya wateja nchini India inaweza kusaidia nchi hii ya Afrika mashariki kujiingiza katika biashara hii inayozidi kukua ya huduma ya wateja , inayofikia pato la dola bilioni 130 duniani kote.

Mara baada ya kupatikana teknolojia hiyo wanamatumaini kuwa Kenya inaweza kuchukua nafasi ya vituo ambavyo vimekwisha komaa nchini India pamoja na Philippines.

Cascade Global shirika la ushauri la shughuli za huduma ya wateja , linakadiria mapato ya dola milioni 5 na wafanyakazi wapatao 3,000 tangu kuanzishwa kwa mara ya kwanza kituo cha kwanza cha huduma za wateja miaka michache iliyopita.

Kitu muhimu kinachovutia kwa watu wanaohitaji huduma zetu ni lugha . Kila mahali tunapokwenda watu wanashangaa usahihi wa lafudhi yetu ya Kiingereza, amesema Peres Were, mkurugenzi mtendaji wa cascade Global.

Wanatambua kuwa India inahemewa na kazi na ubora sio mzuri sana. Wanataka kuijaribu Afrika.

Teknolojia ni kikwazo kikubwa kwa Kenya. Hata kama lafudhi ya Kiingereza itakuwa nzuri namna gani , kuna tatizo la kiufundi kwa upande wa masiliano ya simu, na hili ni tatizo katika biashara.

Wafanyabiashara hii ya vituo vya huduma kwa wateja katika Kenya wanategemea mfumo wa kizamani wa satalite ambako wakati wa kuzungumza na simu kunasikika mwangwi kutokana na mwanya uliopo wakati sauti inasafiri kiasi cha kilometa 36,000 katika anga na kurudi na huharibu ubora wa mazungumzo.

Kwa huduma hiyo wafanyabiashara hiyo wanalipa kiasi cha dola 7,000 kwa megabyte moja kila mwezi , ikilinganishwa na kiasi cha dola 500 kwa megabyte moja kwa mwezi kwa wenye vituo hivyo nchini India.

India ilijipatia pato la dola bilioni 39.6 katika mwaka wa fedha uliopita kutokana na vituo vya simu vya kutoa huduma kwa wateja, operesheni za msaada wa huduma za ofisi pamoja na utengenezaji wa vifaa vya mawasiliano ya kompyuta.

Sekta hii inaajiri kiasi cha watu milioni 1.5 nchini India na inachangia kiasi cha asilimia 5.2 ya pato jumla la taifa. Philippines ilipata kiasi cha dola bilioni 3.26 katika mwaka 2006 na inamatumani ya kuongeza mara dufu pato hilo hadi ifikapo mwaka 2010.

Mpango huo wa Kenya utakaogharimu kiasi cha dola milioni 100 wa waya huo maalum utakaotandikwa chini ya bahari utaunganisha mji wa Mombasa na Fujairah katika umoja wa falme za Kiarabu, Emarati.

Ukijulikana kama mfumo wa majini katika Afrika mashariki East African Marine Systems TEAMS, kwa kifupi, utarudisha chini gharama na kufikia katika viwango sawa na India. Kwa hivi sasa serikali imepata mkopo kutoka benki kuu ya dunia ili kutoa ruzuku kwa gharama za simu hadi pale waya huo utakawasili mjini Mombasa.

Lakini teknolojia ya kizamani sio kikwazo pekee ambacho kinakabili biashara hii changa ya vituo vya simu vya kiwahudumia wateja nchini Kenya. Tatizo letu kubwa ni kwamba bado tuwachanga na makampuni mengi katika mataifa tajiri hayafahamu kama tupo, amesema Gilda Odera mkurugenzi mtendaji wa Skyweb Evans, kituo kingine cha huduma za wateja. hApa Wakenya wanamatumaini kuwa kujiamini na lafudhi nzuri ya lugha ya Kiingereza inaweza kuleta tofauti.

 • Tarehe 01.08.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHjv
 • Tarehe 01.08.2007
 • Mwandishi Sekione Kitojo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHjv
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com