1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Chama cha Die Linke kina matumaini ya kuwa serikalini

Josephat Charo
24 Agosti 2017

Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia nchini Ujerumani, Die Linke, kinaelekea katika uchaguzi mkuu wa mwezi Septemba kikishawishika kwa utendaji wa sera zake.

https://p.dw.com/p/2ijQn
Vorstellung der Wahlplakate der Partei Die Linke
Picha: Picture alliance/Gregor Fischer/dpa

Matokeo ya kura za maoni za hivi karibuni yanaonyesha kuwa chama hicho kinaungwa mkono kwa asilimia kati ya 8 na 10 na msimamo wake wa kukataa kuwa mojawapo ya vyama vinavyoweza kushirikishwa katika serikali ya mseto, unakiweka katika hali ya kuwa katika kambi ya upinzani kwa mara nyingine tena.

Baada ya miaka ya malumbano ya ndani, chama cha upinzani cha siasa kali za mrengo wa kulia Die Linke kiliadhimisha miaka 10 tangu kuasisiwa kwake hivi majuzi katika mazingira yasiyo ya kawaida. Kila mtu katika sherehe za maadhimisho hayo alikuwa akizungumzia mawazo sawa. Swali ni je, wanaweza kuuendeleza msimamo huo hadi Septemba 24 siku ya uchaguzi mkuu? Na hata wakifanya hivyo, je kutakuwa na thawabu?

Chama cha Die Linke kiliundwa mwaka 2007 na warithi wa chama kilichoitawala Ujrumani Mashariki hadi mwaka 1990 na wanasiasa walioasi chama cha Social Democratic, SPD upande wa Ujerumani Magharibi. Chama hicho kwa muda mrefu kimekuwa kikidhibitiwa na viongozi mashuhuri wenye ushawishi mkubwa na tofauti za kiitikadi.

Uchaguzi wa mwaka 2009 ulishuhudia chama hicho kipya kikijishindia asilimia 11.9 ya kura, nyingi kutoka eneo la mashariki ya Ujerumani. Miaka minne baadaye uungwaji mkono huo uliporomoka hadi kufikia asilimia 8.6. Hata hivyo, chama hicho kwa sasa kinashikilia nafasi ya tatu kwa ukubwa katika bunge la Ujerumani, Bundestag, hivyo kukifanya kuwa chama kikubwa cha upinzani dhidi ya serikali ya mseto ya kansela Angela Merkel.

Lafontaine atoa mwito wa mabadiliko Ujerumani

Na licha ya kuganda kati ya asilimai 8 hadi 10 katika kura za maoni za hivi karibuni, bado kuna hali ya kujiamini katika uongozi wa juu wa chama kwamba Ujerumani huenda iko tayari kwa mabadiliko baada ya miaka karibu 12 chini ya utawala wa kansela Merkel.

"Tunalazimika kubadili mawazo yetu, vinginevyo hakutakuwa na muelekeo katika vuguvugu letu," alisema mwanasiasa mkongwe Oskar Lafontaine wakati alipowahutubia wajumbe katika sherehe ya maadhimisho ya miaka 10 tangu kuundwa kwa chama cha Die Linke, ambapo mada kuu ilihusu kujiandaa kwa uchaguzi mkuu.

Oskar Lafontaine Sahra Wagenknecht
Oskar Lafontaine (kulia) na Sahra Wagenknecht, mgombea ukansela wa Die LinkePicha: picture-alliance/dpa

Wanachama wa chama Die Linke wamekuwa wakimkosoa kansela Merkel na chama chake cha siasa za wastani zinazoegemea mrengo wa kulia cha Christian Democratic Union, CDU wakati wanapokiona chama hicho kikiwasilisha sera ambazo Die Linke kinasema zitaiharibu Ujerumani.

"Ahadi hizi zote haziungwi mkono na ushahidi na huenda zikayeyuka baada ya uchaguzi kukamilika," alisema Mwenyekiti wa chama Katja Kipping, baada ya chama cha CDU kutoa ilani yake ya uchaguzi mapema mwezi huu.

Chama cha Die Linke kinadai ndicho chama chenye uwezo wa kusimamia vyema masuala ya fedha, kikisisitiza kwamba mipango iliyowasilishwa na vyama viwili vikubwa haiingii akilini. Mgombea wa chama cha Die Linke katika uchaguzi wa Septemba ni Sahra Wagenknecht.

Ufanisi wa chama cha Die Linke katika chaguzi za Ujerumani umeshuhudiwa sana eneo la mashariki lililokuwa zamani chini ya utawala wa kikomunisti, na pia katika jimbo la Berlin na jimbo dogo la kusini magharibi la Saarland, nyumbani kwa Oscar Lafontaine.

Katika jimbo la Thuringia chama cha Die Linke kimekuwa chama pekee chenye nguvu katika serikali ya mseto na chama cha Social Democratic, SPD tangu mwaka 2014. Katika jimbo la Brandenburg na jimbo la Berlin, chama cha Die Linke kimekuwa mshirika mdogo wa chama cha SPD tangu mwaka 2009 na 2016 mtawalia.

Kuna shauku ya mabadiliko na kuwa na siasa tofauti na tunatakiwa kubeba jukumu la kuleta mageuzi hayo, anasema Oscar Lafontaine, aliyewahi kuwa waziri wa fedha katika serikali ya chama cha Social Democratic, SPD, kabla kujiuzulu mwaka 1999 na baadaye kusaidia kukiasisi chama cha Die Linke.

Mwandishi:Josephat Charo/dpae

Mhariri:Iddi Sessanga