Israel yashambulia Syria | Matukio ya Kisiasa | DW | 31.01.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Israel yashambulia Syria

Jumuiya ya nchi za kiarabu hii leo imeishutumu Israel kwa kuishambulia Syria kwa makombora ya angani ikisema hatua hiyo ni dhahiri na ya wazi kuwa Israel inaingilia maswala ya mamlaka ya nchi za kiarabu.

Shambulizi la angani

Shambulizi la angani

Nabil al-Arabi mkuu wa Jumuiya ya nchi za kiarabu amesema ukimya wa jumuiya ya kimataifa juu ya mashambulizi ya hapo nyuma ya Israel nchini Syria ndio ulioipa nguvu nchi hiyo kufanya shambulizi jengine kufuatia hali ya kiusalama na ya kisiasa nchini Syria inayozidi kudorora.

Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Nabil Al-Arabi

Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu Nabil Al-Arabi

Wakati huo huo Urusi imeonesha wasi wasi wake juu ya shambulizi la Israel katika taasisi ya utafiti ya kijeshi nchini Syria, ikisema kuwa shambulizi kama hilo kamwe halikubaliki. Kulingana na wizara ya mambo ya nje ya Urusi, shambulizi hilo litakapothibitishwa, Israel itakuwa imekiuka kwa kiwango kikubwa mkataba wa Umoja wa Mataifa.

Hapo jana serikali ya Syria ilitangaza kuwa ndege za kijeshi za Israel zililenga taasisi yake ya utafiti wa kijeshi kaskazini magharibi mwa mji mkuu, Damascus. Watu wawili waliuwawa na wengine watano wamejeruhiwa katika shambulizi hilo. Hata hivyo Syria ilikanusha ripoti kuwa Israel ililenga msafara wa magari yaliyokuwa na silaha za kivita karibu na mpaka wa Lebanon.

Israel haijatoa tamko rasmi juu ya shambulizi

Hadi sasa hakuna tamko lolote rasmi juu ya tukio hilo kutoka kwa serikali ya Israel. Nchi hiyo mara kwa mara imekuwa na hofu kwamba silaha mbali mbali zimekuwa zikisafirishwa kutoka Urusi hadi Syria na kwamba huenda silaha hizo zikaangukia mikononi mwa kundi la Hezbolla ambalo ni washirika wa Syria.

Rais wa Syria Bashar al-Assad

Rais wa Syria Bashar al-Assad

Hezbollah kwa upande wake imelaani shambulizi la Israel na kusema ni hatua ya nchi hiyo kuiharibu Syria.

Israel ilinukuliwa na vyombo vya habari nchini humo ikisema haitakubali silaha zozote zinazotoka Iran, Korea kaskazini, na Urusi kufikia makundi ya kigaidi kama Hezbollah ambayo ni washirika wakubwa wa Syria, Iran. Hii ni kulingana na Tzahi HaNegbi ambaye ni mbunge kutoka chama cha Likud anayejulikana kuwa karibu sana na waziri mkuu Benjamin Netanyahu.

Baadhi ya kambi za wakimbizi wa Syria

Baadhi ya kambi za wakimbizi wa Syria

Kando na hilo Urusi imekuwa ikikosolewa na jamii ya Kimataifa pamoja na Jumuiya ya nchi za kiarabu kwa kukataa kujiunga na wito wa kimataifa wa kumtaka rais Bashar al Assad kuondoka madarakani ili kukomesha umwagikaji wa damu unaoendelea kwa miezi 22 sasa tangu kutokea kwa maandamano ya kutaka mabadiliko nchini humo.

Urusi inasemekana kuwa bado inaendelea kupeleka silaha nchini Syria. Takriban watu 60,000 wameuwawa tangu kuanza kwa ghasia hizo mwezi machi mwaka wa 2011.

Mwandishi Amina Abubakar/dpa/AFP

Mhariri: Daniel Gakuba

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com