ISLAMABAD:Ndege ya Rais Musharraf yakoswa na risasi | Habari za Ulimwengu | DW | 06.07.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

ISLAMABAD:Ndege ya Rais Musharraf yakoswa na risasi

Milipuko miwili na milio ya risasi inasikika nje ya msikiti wa Lal mjini Islamabad uliozingirwa na polisi kwa siku tatu sasa.Majeshi yaliyojihami yanaripotiwa kuelekea kwenye msikiti huo japo maafisa wa serikali wanakanusha kuwa wanashambulia rasmi eneo hilo.Mapigano hayo yanatokea saa chache baada ya naibu kiongozi wa msikiti huo wa Lal Abdul Rashid Ghazi kuapa kuwa afadhali apoteze maisha yake badala ya kujisalimisha. Wafuasi hao wanalazimisha kutumiwa kwa sheria ya Taleban jambo lililosababisha ghasia kutokea na kusababisha vifo vya watu 19.Hata hiyo serikali inakataa kufanya mazungumzo zaidi.Tariq Azeem Khan ni naibu waziri wa habari na mawasiliano nchini Pakistan

‘’Serikali kamwe haitafanya mazungumzo mengine yoyote.Muda mwingi umeshapita sasa wakati tunajaribu kuwashawishi waliojificha msikitini kujisalimisha.Wakati wote tumesisitiza kupatikana suluhu kwa njia ya amani ya majadiliano.Kwahiyo sharti wajisalimishe bila masharti yoyote ‘’

Wakati huohuo jeshi la Pakistan linakanusha ripoti kuwa ndege ya Rais Pervez Musharraf wa Pakistan imekoswa na risasi baada ya kupaa angani.Kwa mujibu wa duru za usalama milio ya risasi ilisikika dakika chache karibu na uwanja wa ndege wa kijeshi wa Chaklala ulio nje ya mji wa Islamabad.Duru hizo zinaeleza kuwa Rais Musharraf aliwasili salama katika mji wa Turbat ulio kusini mwa Pakistan ili kuwatembelea wahanga wa mafuriko ya hivi karibuni.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com