IS yauharibu msikiti wa kihistoria Mosul | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

IS yauharibu msikiti wa kihistoria Mosul

Kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS, limeuharibu msikiti wa kihistoria wa karne ya 12 wa al-Nuri ulioko Mosul, pamoja na mnara wake maarufu uitwao al-Hadba, baada ya kuulipua  msikiti huo usiku wa kuamkia Alhamis.

Irak al-Nuri Moschee in Mossul (Reuters/Iraqi Military )

Msikiti wa al-Nuri ulioharibiwa huko Mosul

Haya ni kulingana na wizara ya ulinzi ya Iraq. Waziri Mkuu Haider al-Abadi aliandika katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter mapema Alhamis akisema, uharibifu huo, ni ishara ya wanamgambo hao kukiri kushindwa katika mapambano ya kuuwania mji wa Mosul- wa pili kwa ukubwa nchini Iraq.

Msikiti huo ambao pia unaitwa Msikiti Mkuu wa Mosul, ndiyo sehemu ambayo kiongozi wa hilo kundi la Dola la Kiislamu Abu bakr al-Baghdadi, alipotoa tangazo mwaka 2014 kwamba mji wa Mosul ni eneo linaloongozwa na kiongozi wa Kiislamu, muda mfupi baada ya mji huo kutwaliwa na wanamgambo wa kundi hilo. Mnara huo ulioharibiwa ambao ulikuwa unaonekana kama ule mnara wa Italia wa Pisa, ulikuwa umesimama kwa zaidi ya miaka 840.

Dola la Kiislamu lanalaumu shambulizi la Marekani kwa uharibifu wa msikiti huo

IS iliulipua msikiti huo, wakati wa sherehe za Laylat al Qadr, ambao ni usiku mtakatifu zaidi kwa Waislamu. Usiku wenye nguvu kama unavyoitwa, unaadhimisha usiku ambao kitabu  tukufu cha Quran, kilipofichuliwa kwa Mtume Muhammad katika kipindi cha mwezi mtukufu wa Ramadhani, kipindi kinachoendelea kwa sasa.

Irak Mossul al-Nuri Moschee (Getty Images/AFP/A. Al-Rubaye)

Mnara wa al-Hadba kabla haujaharibiwa

Taarifa ya kundi hilo la kigaidi iliyowekwa mtandaoni muda mfupi baada ya wizara ya ulinzi ya Iraq kutangaza kuharibiwa kwa msikiti huo, ililaumu shambulizi la hewani lililofanywa na jeshi la Marekani, ingawa muungano unaoongozwa na Marekani kupambana na magaidi hao, umekanusha kama alivyosema Brett McGurk, mjumbe maalum wa rais wa Marekani katika muungano huo wa kupambana na IS.

"Mwezi Juni 2014, mji wa karibu watu milioni 2 ulitwaliwa na IS na kiongozi wake Abu bakr al-Baghdadi, kutoka ndani ya msikiti, msikiti mkuu wa Al Nuri katika mji wa kale wa Mosul, alitangaza mji huo kama eneo linaloongozwa na kiongozi wa Kiislamu," alisema McGurk, "na jana jioni wakati ambapo kikosi cha Iraq kilipokuwa kinaukaribia msikiti huo, karibu mita 100 hivi, IS ikaulipua msikiti huo, msikiti ambao umekuwa hapo tangu karne ya 12, IS ikaulipua."

Wanajeshi wa Iraq wamefanikiwa kuyachukua maeneo kadhaa yaliyokuwa yanamilikiwa na IS

Wapiganaji wa kundi hilo walijaribu kuuharibu mnara wa msikiti huo mwezi Julai mwaka 2014 baada ya kusema, jinsi ulivyojengwa unakwenda kinyume na tafsiri yao ya Uislamu lakini wakaazi wa Mosul walikusanyika katika eneo hilo na kuunda nyororo wa binadamu ili kuulinda mnara huo. Kundi hilo limeyaharibu maeneo ya kihistoria nje na ndani ya Mosul, wakisema ni mambo yanayopigia debe kuabudu sanamu.

Irakische Soldaten in der Anbar Provinz August 2014 (AFP/Getty Images/A. Shallal)

Vikosi vya keshi la Iraq vikiwa katika doria

Katika wiki chache zilizopita, wanajeshi wa Iraq, wamefanikiwa kuchukua umiliki ya maeneo kadhaa magharibi mwa Mosul, na kuwalazimu wanamgambo hao wa Dola la Kiislamu kusonga katika eneo la mji huo ambalo ni dogo, ila kulingana na Umoja wa Mataifa ni eneo ambalo ni makao ya kiasi ya watu 100,000.

Mapambano ya kuuchukua tena mji wa Mosul yalianzishwa zaidi ya miezi minane iliyopita na yamesababisha  zaidi ya watu 850,000 kuachwa bila makao.

Mwandishi: Jacob Safari/APE/DPAE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com