Iran yaukataa mpango wa Marekani wa kumaliza vita
26 Machi 2026
Rais wa Marekani Donald Trump amesema yuko tayari "kuisambaratisha Iran" ikiwa haitakubali makubaliano ya kukomesha vita. Hayo yameelezwa Jumatano usiku na Msemaji wa Ikulu ya White House Karoline Leavitt alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari na kusema kuwa viongozi waliosalia wa utawala wa Iran wana fursa nyingine ya kushirikiana na Rais Trump, kuachana kabisa na mipango yao ya nyuklia na kuacha kuitishia Marekani na washirika wake. Leavitt ameendelea kuwa rais Trump anatoa kipaumbele kwa amani na hakuna haja ya kuwa na vifo na uharibifu zaidi huku akiionya Iran.
" Lakini ikiwa Iran itashindwa kukubali ukweli wa wakati huu, ikiwa haitaki kuelewa kwamba imeshindwa kijeshi na itaendelea kuwa hivyo, Rais Trump atahakikisha inapishambuliwa vikali zaidi kuliko ilivyowahi kushuhudiwa awali. Kauli ya rais Trump si maneno matupu na Iran haipaswi kukosea tena kama walivyofanya na kuwagharimu kuwapoteza viongozi wao wakuu, jeshi lao la anga na wanamaji pamoja na mfumo wao wa ulinzi wa anga. Vurugu zozote za baadaye zitashuhudiwa kwa kuwa Iran imekataa kukubali kuwa wameshindwa na hawataki kufikia makubaliano."
Tehran haikuchelewa kujibu ikisema inalipitia pendekezo hilo lakini haina nia ya kujadiliana. Licha ya baadhi ya maafisa wa Iran kutaja kuwa nchi hiyo ilipokea pendekezo la Marekani wa kuvimaliza vita vya Mashariki ya Kati . Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema Tehran haina nia hiyo.
"Kwa sasa, sera yetu ni mwendelezo wa upinzani na kuilinda nchi yetu. Kwa sasa, hatuna nia ya kujadiliana, hakuna mazungumzo yaliyofanyika, na naamini msimamo wetu una kanuni kamili. Niseme tu kuwa, jumbe zilizowasilishwa kupitia nchi rafiki au watu fulani haziwezi kutajwa kuwa ni majadiliano wala mazungumzo. "
Iran yasifu uwezo wake wa kijeshi
Kauli hii ya Araghchi imeondoa matumaini ya kupatikana kwa suluhisho huku vurugu zikiendelea bila kuonyesha dalili zozote za kupungua baada ya karibu mwezi mzima wa vita. Aidha Araghchi amesifu ushupavu wa jeshi la Iran na kusema kuwa kwa sasa nchi hiyo imejijingea hadhi ambayo itakuwa vigumu kushambuliwa tena.
" Ninaamini kwamba hakikisho la dhati tulilojijengea sasa ni kudhihirisha nguvu zetu katika eneo hili na sidhani kama kuna mtu yeyote atakayethubutu tena kuingia katika migogoro na vita na watu wa Iran. Yote haya, kwa maoni yangu, yameuonyesha ulimwengu wote, eneo lote, kwa Marekani na Wamarekani haiba yetu ya kutoshindwa, ustahimilivu, na utulivu wa Jamhuri ya Kiislamu."
Hayo yakiarifiwa, Kiongozi wa Hezbollah Naim Qassem, amesema kufanya mazungumzo na Israel wakati mashambulizi yakiendelea itakuwa sawa na Lebanon kukubali "kusalimu amri." Kauli hiyo imetolewa wakati Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, akisema vikosi vyake "vimetanua eneo la ulinzi na usalama" ndani ya Lebanon na kwamba vikosi vyake vya ardhini vinajaribu kusonga mbele.
Israel ililikalia eneo la kusini mwa Lebanon kwa takriban miongo miwili hadi mwaka 2000, imetuma tena vikosi vya ardhini nchini humo, ikisema inajaribu kuchukua udhibiti wa eneo hilo hadi Mto Litani, takriban kilomita 30 kutoka mpakani mwa nchi hizo mbili. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametahadharisha kuwa Lebanon haipaswi kugeuzwa kama Gaza.
Katika hatua nyingine, Kuwait kupitia Wizara yake ya mambo ya ndani imesema imewakamata watu sita wenye mafungamano na kundi la Hezbollah ambao walikuwa wakipanga "vitendo vya uhalifu na mauaji ya viongozi" wa mataifa ya Ghuba.