Iran yasherehekea Eid ul Fitr huku vita vikiendelea
21 Machi 2026
Kiongozi mkuu wa Iran kwa kawaida huongoza sala ya Eid lakini Ayatollah Mojtaba Khamenei, ambaye aliingia madarakani mapema mwezi huu baada ya baba yake kuuawa katika shambulio la Marekani na Israel, hakuonekana hadharani siku ya Jumamosi katika ibada hiyo muhimu kwa Waislam.
Badala yake, Jaji Mkuu wa Iran Gholam Hossein Mohseni Ejei, amehudhuria sala hiyo katika msikiti mkuu wa Imam Khomeini katikati mwa Tehran, ambao ulikuwa umefurika watu na waumini wengine wakishuhudiwa nje ya msikiti huo, licha ya mashambulizi makubwa ya anga jana jioni wakati wa maadhimisho ya "Nowruz", ambao ni Mwaka Mpya wa Kiajemi.
Salamu kutoka Moscow, mashambulizi Isfahan
Rais wa Urusi Vladimir Putin ambaye ni mshirika mkuu wa Iran, ametuma salamu kwa Khamenei, "akiwatakia watu wa Iran kuwa imara na kuyashinda majaribu hayo makubwa na akasisitiza kwamba katika kipindi hiki kigumu, Moscow inasalia kuwa rafiki wa kweli na mshirika wa dhati wa Tehran". Moscow imelaani pia shambulio katika kituo cha Natanz.
Kulingana na shirika la nishati ya atomiki la Iran, Marekani na Israel zilifanya mashambulizi na kukilenga kiwanda kilichopo huko Natanz katika jimbo la Isfahan, chenye mitambo ya chini ya ardhi ya kurutubisha madini ya urani kwa ajili ya mpango wa nyuklia wa Iran ambao ndio kiini cha mzozo huu. Kiwanda hicho kiliharibiwa katika vita vya mwezi Juni mwaka 2025. Shirika hilo limeongeza kuwa hakuna uvujaji wa chembechembe za nyuklia ulioripotiwa.
Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kudhibiti Nishati ya Atomiki (IAEA), Rafael Grossi, ametoa wito wa "kujiepusha na harakati za kijeshi eneo hilo ili kuepuka janga la nyuklia", lakini shirika hilo la Umoja wa Mataifa limethibitisha kwamba hakuna ongezeko la viwango vya mionzi nje ya eneo lililoripotiwa kushambuliwa. Walipohojiwa kuhusu Natanz, jeshi la Israel limekanusha na kusema "halina taarifa zozote za mashambulizi eneo hilo".
Mzozo wafukuta, msimamo tata wa Marekani
Israel imesema Iran imeendelea kufyatua makombora mapema Jumamosi, huku Saudi Arabia ikisema imedungua droni 20 ndani ya saa kadhaa katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo, kunakopatikana mitambo mikubwa ya mafuta. Wizara ya ulinzi ya nchi hiyo imesema hakukuwa na majeruhi wala uharibifu.
Hayo yakiarifiwa, Rais wa Marekani Donald Trump amesema utawala wake unafikiria kumaliza operesheni za kijeshi Mashariki ya Kati licha ya nchi hiyo kutangaza kutuma meli zaidi za kivita na jeshi la wanamaji katika eneo hilo huku Iran ikitishia kushambulia maeneo ya utalii duniani kote.
"Tunakaribia mno kufikia malengo yetu tunapofikiria kupunguza juhudi zetu kubwa za kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati," Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii. Pia Katibu wa habari wa Ikulu ya White House amesema Wizara ya ulinzi ya Marekani Pentagon imesema huenda operesheni yao hiyo ikamaliza ndani ya muda wa wiki nne hadi sita.
Taarifa hizo za mkanganyiko za Marekani zinajiri baada ya kupanda tena kwa bei ya mafuta huku pia utawala wa Trump ukisema pia kuwa utaondoa vikwazo dhidi ya mafuta ya Iran yanayopakiwa kwenye meli, hatua inayolenga kukabiliana na ongezeko hilo la bei ya mafuta ambalo limepelekea kushuka kwa soko la hisa la Marekani.
Hatua hiyo ya kukabiliana na ongezeka la bei ya mafuta kote duniani itaruhusu usafirishaji na uuzaji wa mafuta ghafi ya Iran na bidhaa zingine za petroli zilizopakiwa kwenye meli kabla ya Machi 20 na itaendelea hadi Aprili 19, 2026.
Vita hivi vya Iran vyaathiri ulimwengu mzima
Baada ya wiki tatu za mzozo ambao umesababisha bei za nishati kupanda kote duniani, kufuatia hatua ya Tehran kuufunga Mlango Bahari wa Hormuz ambayo ni njia muhimu ya usafirishaji wa mafuta, gesi na hata mbolea, eneo ambalo limezidisha pia msuguano kati ya Trump na washirika wake muhimu kutoka Jumuiya ya Kujihami ya NATO ambao wamekataa kujiingiza moja kwa moja katika mzozo huo licha ya wito wa Trump wa kuzitaka nchi hizo kumsaidia kuufungua mlango Bahari wa Hormuz.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Abbas Araghchi amesema Tehran imeziwekea vikwazo meli kutoka nchi zinazohusika na mashambulizi dhidi ya Iran lakini itaziruhusu meli nyengine. Mgogoro huo umesababisha bei ya mafuta ghafi kupanda maradufu, huku pipa la mafuta ghafi la "North Sea Brent" likipanda kwa zaidi ya asilimia 50 mwezi uliopita na kufikia sasa zaidi ya dola 105 kwa pipa.