Iran yaitaka Marekani kurudi katika mkataba | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.06.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Iran yaitaka Marekani kurudi katika mkataba

Rais wa Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran, Hassan Rowhani ameishauri Marekani kurudi katika makubaliano ya mkataba wa nyuklia wa mwaka 2015 uliofikiwa kati ya Iran na mataifa makubwa.

Akizungumza katika kikao cha baraza lake la mawaziri, rais Rowhani alisema Marekani inafaa kutimiza wajibu wake katika makubaliano hayo iliyoyatilia sahihi na kwamba kurudi katika makubaliano hayo ndio njia fupi kabisa ya kutimiza maslahi ya pande zote - Iran na Marekani na vile vile itakuwa jambo zuri kwa ulimwengu na kuzuia kuenea kwa silaha za nyuklia kikanda na kimataifa.

Katika tovuti yake, aliionya Marekani dhidi ya kutumia nguvu za kijeshi kwa Iran na kwamba watakapokiuka mipaka ya Iran basi Iran haitakuwa na budi kuchukua hatua. Hata hivyo rais Rowhani hakusema iwapo Iran itashiriki katika mazungumzo endapo Marekani itarudi kwenye mkataba huo na pia kuondoa vikwazo ilivyowawekea viongozi wa Iran.

Mzozo baina ya Marekani na Iran ulianza mwaka mmoja uliopita baada ya Marekani kujitoa katika makubaliano ya mkataba wa Nuklia baina yake na Iran na mataifa mengine yaliyo na nguvu duniani na kisha kuanza kuiwekea vikwazo Iran. Hivi karibuni Iran ilizidisha mara nne utengenezaji wa silaza zilizo na kiwango cha chini cha madini ya Ureniam kwa lengo la kuvunja mojawapo ya makubaliano ya mkataba huo na pia kutishia kwamba itaongeza kutengeneza silaha nyengine zilizo na kiwango cha juu cha Ureniam kufikia Julai 7, iwapo mataifa ya Ulaya yaliyotia sahihi mkataba huo hawatatoa makubaliano mengine mapya.

Iran | Hassan Rohani | Ayatollah Ali Khamenei (AFP/Getty Images/B. Mehri)

Kiongozi wa Kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei

Kiongozi wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei amesema Iran kamwe haitabadilisha msimamo wake kwa vikwazo vya Marekani.

"Marekani ni nchi iliyo na uovu mkubwa duniani. Imesababisha vita, umwagikaji wa damu na mgawanyiko. Imekuwa ikifanya ulanguzi na wizi katika mataifa mengine. Imekuwa hivyo kwa muda mrefu sana, sio kwa miaka kumi ama ishirni iliyopita. Watu wanaochukiwa zaidi katika utawala huo wanaishutumu Iran, siku haipiti bila ya kuilaani ama kuitukana Iran. Hatutarudi nyuma kwa kutulaani na kutudhalilisha," alisema Khamenei.

Mkuu wa jeshi la mapinduzi la Iran Hossein Salami alinukuliwa na shirika la habari la Iran akisema kwamba vikwazo vya Marekani kwa Iran ni hatua za kukosa matumaini baada ya Iran kudengua ndege yao isiyokuwa na rubani katika ghuba ya Omani. Hossein ameongeza kwamba baada ya ndege hiyo kudenguliwa, Marekani imekuwa ikijiziba aibu kwa kutoa kauli zisizokuwa na maana.

(RTRE/DPA/AFP)

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com