Iran kuzidisha kasi ya urutubishaji wa madini ya Urani | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.09.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Iran kuzidisha kasi ya urutubishaji wa madini ya Urani

Iran imetangaza itachukua hatua nyingine mbali na mpango wa nyukilia wa 2015 kwa kuanza kutengeneza mashinepewa ili kuzidisha kasi ya urutubishaji madini ya Urani na kutoa muda wa miezi miwili kuunusuru mkataba. 

Iran imetangaza itachukua hatua nyingine mbali na mpango wa nyukilia wa 2015kwa kuanza kutengeneza mashinepewa ili kuzidisha kasi ya urutubishaji madini ya Urani huku ikiyapatia mataifa ya magharibi muda zaidi wa miezi miwili ili yaweze kuunusuru mkataba huo. 

Katika hotuba kwa njia ya Televisheni, rais Hassan Rouhani amesema kuanzia Ijumaa wiki hii, Irani itaanza kutengeneza mashinepewa au centrifuge kwa Kiingereza, kwa ajili ya kuharakisha urutubishaji wa Urani, ili kuzalisha mafuta kwa ajili ya vinu vya kinyukilia au mabomu ya atomiki, ikiwa ni hatua ya karibuni ya kukiuka makubaliano ya nyuklia.

Chini ya mkataba huo, Iran iliruhusiwa kubakisha kiwango fulani cha kizazi cha kwanza cha mashinepewa katika vinu vyake viwili vya nyuklia. Hatua hiyo ya kutengeneza mashinepewa kutawezesha kuzalisha nyenzo muhimu ya bomu la nyuklia kwa haraka sana.

"Tutashuhudia utafiti na maendeleo ya aina tofauti za mashinepewa na mashinepewa mpya na chochote kinachohitajika kwa ajili ya kurutubisha Urani ambayo itashughulikiwa na shirika letu la nishati ya Atomiki na tutafuatilia kwa umakini katika suala hili".

Iran inasema inarutubisha Urani kwa ajili ya mafuta ya vinu vyake vya nyuklia, lakini Marekani kwa muda mrefu inashuku kwamba mpango huo unakusudia kuunda silaha. Tangu Marekani ilipojiondoa katika mkataba huo, Tehran imechukua hatua mbili zinazokiuka mkataba huo, ingawa yenyewe inasema bado ina nia ya kunusuru makubaliano.

Iran Atomprogramm (picture-alliance/AP Photo/V. Salemi,)

Mfanyakazi katika mtambo wa Urani nchini Iran

Rouhani alikuwa ametishia kuchukua hatua zaidi ifikapo Septemba tano ikiwa Ufaransa na mataifa mengine ya Ulaya yaliyotia saini makubaliano hayo, hayatofanya juhudi zaidi kuilinda Iran dhidi ya athari za vikwazo vya Marekani ambavyo hado sasa vimepunguza mauzo ya mafuta ya Iran.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu ametaka shinikizo zaidi dhidi ya Tehran kutokana na hatua zake hizo. Netanyahu amesema "Huu si wakati wa kuzungumza na Iran, ni wakati wa kuzidisha shinikizo". Netanyahu anaelekea jijini London kukutana na waziri mkuu Boris Johnson na waziri wa ulinzi wa Marekani Mark Esper. Rais Donald Trump aliwaeleza waandishi wa habari Jumatano kwamba Iran inataka kuketi meza ya mazungumzo baada ya kuwekewa vikwazo.

Siku ya Jumatano Marekani iliorodhesha kile ilichokiita "mafuta kwa ugaidi", mtandao wa makampuni, meli na watu inaowatuhumu kuagizwa na jeshi la walinzi wa kimapinduzi kwa kusambaza mafuta Syria yenye thamani ya mamilioni ya dola. Marekani pia imetoa zawadi ya kitita cha Dola milioni 15 kwa ajili ya taarifa za operesheni za kifedha za jeshi la walinzi wa kimapinduzi pamoja na majeshi mengine ya Iran.

Hatua hizo zinazidisha kampeni ya Marekani ya kutaka kuondoa Iran katika mauzo ya mafuta kama njia ya kuishinikiza kuzuia mpango wake wa nyukila na makombora.

Reuters/dpa

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com