1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

IMF: Uchumi wa dunia unakuwa kwa kasi ndogo

13 Oktoba 2021

Shirika la Fedha Duniani IMF limetahadharisha kwamba kutatizwa kwa njia za usambazaji bidhaa duniani kunasababisha ongezeko la bei na kutatiza ukuaji wa chumi zinazoanza tena kukua baada ya janga la Covid-19.

https://p.dw.com/p/41d24
IWF Report Logo
Picha: Yuri Gripas/REUTERS

Katika ripoti yake ya hivi majuzi ya kuangazia uchumi wa dunia, IMF imesema athari inayoendelea kukumba chumi kutokana na janga la virusi vya corona na usambazaji usio sawa wa chanjo, ni mambo yanayozidi kupanua zaidi pengo la kiuchumi baina ya nchi mbalimbali na kuvunja matumaini ya maendeleo katika nchi zenye chumi zinazokua.

Tobias Adrian, ni mshauri wa masuala ya fedha na mkurugenzi katika idara ya fedha na soko la mitaji katika Shirika la Fedha Duniani IMF.

"Kwanza kabisa, deni limeongezeka. Nchi zilipokuwa zinapambana na janga la virusi vya corona, zilipunguza sera za fedha, zikaongeza matumizi na matokeo yake, madeni yakaongezeka kwa serikali na katika nchi zengine madeni yameongezeka hata katika familia," alisema Tobias.

Takwimu hazitoi picha kamili ya hali katika baadhi ya nchi

Ripoti hiyo inasema uchumi wa dunia unatarajiwa kukua kwa asilimia 5.9mwaka huu, hiyo ikiwa umeshuka kidogo ikilinganishwa na mwezi Julai. Mwaka ujao wa 2022 kasi ya ukuaji wa uchumi duniani itapungua hadi asilimia 4.9.

Pfizer-BioNTech COVID-19 Impfstoff
Chanjo za virusi vya coronaPicha: Pfizer/AP Photo/picture alliance

Mchumi mkuu wa Shirika la Fedha Duniani Gita Gopinath anasema takwimu hizi lakini haizoti picha kamili ya jinsi hali ilivyo mbaya kwa baadhi ya nchi zikiwemo Marekani, Ujerumani na Japan ambazo zinaathirika mno kutatizika kwa njia za usambazaji bidhaa.

Ripoti hiyo inadai kwamba uhitaji wa bidhaa uko juu kwa sasa ingawa usambazaji ndio tatizo yote yakitokana na kuwa wafanyakazi wengi bado hawajarudi makazini kutokana na kuenea kwa aina ya kirusi cha Delta. Ukosefu huu wa wafanyakazi ni mambo yanayoziwekea shinikizo chumi za mataifa makuu duniani na kushusha matumaini ya ukuaji wa uchumi katika nchi hizo mwaka huu.

Ukuaji wa uchumi hautokuwa katika nchi zinazoendelea

Chumi zilizokuwa zinatarajiwa ukuaji wake wa kawaida kama ilivyokuwa kabla ya janga la virusi vya corona mnamo mwaka 2022 na ifikiapo mwaka 2024 zitakuwa zimekivuka kiwango hicho cha ukuaji kwa asilimia 0.9.

Tanzania yapata mkopo wa IMF wa kuukomboa uchumi wake

Lakini katika nchi zinazoendelea ukuaji unatarajiwa kusalia asilimia 5.5 hiyo ikiwa ni chini ya kile kiwango cha ukuaji kilichokuwa katika nchi hizo kabla mwaka 2024.

Ukuaji wa uchumi wa Marekani ambao ndio uchumi mkubwa zaidi duniani, utapungua na utakuwa kwa asilimia sita mwaka huu kulingana na IMF. Kulingana na Gopinath, mfumuko wa bei unatarajiwa kurudi hali ya kawaida ifikiapo mwaka ujao wa 2022 katika nchi nyingi ila nchini Marekani, inaweza kuchukua muda mrefu zaidi.