Idadi ya vifo yaongezeka maradufu mjini Moscow kutokana na moto | Masuala ya Jamii | DW | 10.08.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Idadi ya vifo yaongezeka maradufu mjini Moscow kutokana na moto

Urusi inaendelea na harakati zake za kukabiliana na moto wa msituni na kuuzuia usiteketeze maeneo muhimu ya nyuklia. Tahadhari imetolewa juu ya madhara ya kiafya kutokana na moshi wa sumu uliotanda katika anga ya Moscow

Wazima moto wakijaribu kuuzima moto karibu na kijiji cha Dolginino katika eneo la Ryazan kusini mashariki mwa Moscow

Wazima moto wakijaribu kuuzima moto karibu na kijiji cha Dolginino katika eneo la Ryazan kusini mashariki mwa Moscow

Baada ya takriban wiki mbili toka kutokea kwa moto huo wa msituni, ambao umeua zaidi ya watu 50 na pia kuteketeza maeneo ya kuhifadhia vifaa vya kijeshi, mamlaka nchini humo zimesema kuwa zinapiga hatua katika kupambana na moto huo ambao tayari umeteketeza maelfu ya hekari.

Mamlaka katika mji mkuu wa nchi hiyo Moscow, zimekiri kuwa kwa mara ya kwanza jana kiwango cha vifo, vinavyotokea kila siku katika mji huo, imeongezeka maradufu na kwamba vyumba vya kuhifadhia maiti vimelemewa kutokana na kuwepo kwa maiti nyingi, lakini hata hivyo serikali bado haijathibitisha takwimu hizo.

Msemaji wa kitengo cha serikali nchini humo kinachopambana na uchafuzi wa hewa Alexei Popikov amesema uchafu unaotokana na hali hiyo umepungua lakini tatizo bado liko palepale kutokana na kwamba moto huo wa msituni unaendelea kuwaka.

Imeelezwa kuwa kiwango cha hewa ya carbon katika mji huo wa Moscow imeongezeka mara 1.6 juu zaidi ya kiwango kilichotarajiwa mapema leo, ikiwa imeimarika kidogo ya siku moja kabla.

Moto huo wa msituni unaoendelea kuwaka nchini Urusi ambao pia umeathiri sana sekta ya kilimo nchini humo, ambapo hekari milioni 10 za ardhi zimeteketea.

Akisisitizia umuhimu wa sekta hiyo na pia kuhusiana na umuhimu wa misitu hiyo inayoteketea kwa moto kwa ajili ya upatikanaji wa chakula cha binadamu na wanyama, wakati alipotembelea jamhuri ya Mari El, mashariki mwa Moscow, eneo ambalo halijaathiriwa na moto huo Rais wa Urusi Dmitry Medvedev aliwaeleza wakulima katika eneo hilo kwamba mwaka huu mazao yatapungua kutokana na tatizo hilo lililopo.

"Kwetu sisi muhimu sio tu kubakia na fafaka tu, lakini kuwa na malisho kwa ajili ya wanyama kwa mwaka ujao, ili tuweze kubakia na idadi ya wanyama walioko sasa''

Russland Brandkatastrophe Medwedew

Rais wa Urusi, Dmitry Medvedev, kushoto, akizungumza na waziri wa majanga, Sergei Shoigu

Aidha moto huo mkali wa msituni umesababisha pia kifo cha mwanajeshi ambaye alikufa jana baada ya kuangukiwa na mti uliokuwa ukiwaka moto, akiwa katika jitihada za kuzima moto huo uliokuwa ukiwaka katika maeneo yaliyoko kituo kikubwa cha utafiti wa nyuklia katika mji wa Sarov.

Wakati huo huo, Urusi imeanza kutathmini hasara iliyopata kutokana na wimbi kali la joto kuwahi kutokea katika historia ya nchi hiyo, huku wanauchumi wa nchi hiyo wakisema kwamba hali hiyo ya hewa ya ujoto inaweza kuleta hasara ya mabilioni ya dola kwa uchumi wa nchi hiyo.

Hata hivyo itachukua miezi kwa serikali ya nchi hiyo kutoa makadirio rasmi ya athari zilizotokana na hali hiyo ya joto, lakini wanauchumi wengi wanasema janga hilo litaigharimu nchi hiyo kati ya asilimia 0.5 hadi asilimia moja ya pato la mwaka la ndani ya nchi.

Mwandishi: Halima Nyanza(afp)

Mhariri: Josephat Charo

 • Tarehe 10.08.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OgjJ
 • Tarehe 10.08.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/OgjJ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com