Hukumu ya kifo imebadilsihwa kuwa kifungo cha maisha kwa wauguzi wa Ki-Bulgaria nchini Libya | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.07.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hukumu ya kifo imebadilsihwa kuwa kifungo cha maisha kwa wauguzi wa Ki-Bulgaria nchini Libya

Jopo kuu la Mahakama ya Libya jana liliibadilisha hukumu ya kifo iliotolewa hapo kabla kwa wauguzi watano wa Ki-Bulgaria na daktari wa Kipalastina kuwa adhabu ya kifungo cha maisha gerezani.

Kiongozi wa Libya, Muammar al-Gaddai

Kiongozi wa Libya, Muammar al-Gaddai

Waziri wa mambo ya kigeni wa Libya, abdel Rahman Schalkam, alisema serekali yake iko tayari kulizingatia ombi la serekali ya Bulgaria kwamba watu hao waliohukumiwa wapelekwe kwao Bulgaria. Wuguzi hao walituhumiwa kwamba waliwaambukiza kwenye hospitali zaidi ya watoto 400 virusi vya UKIMWI. Inasemekana kila familia ya watoto hao italipwa fidia ya dola milioni moja kutoka fedha zilioko kwenye mfuko ambao umeanzishwa.

Kesi yote ilikuwa sarakasi ya mchezo wa kubinyana, raia hao wa kigeni kutoka Bulgaria na daktari Wa-Kipalastina wakiwa kama mahabusu. Utawala wa Libya, chini ya Muammar al-Ghaddafi, haujaweza kutunga sura ya mashtaka ilio ya kuvutia. Hata katika tawala nyingi nyingine za kidikteta ni taabu kufikiria kwamba tuhumu kama hiyo ingekubaliwa na hukumu kadhaa za mahakama. Hukumu yenyewe iliotolewa ni kifo dhidi ya wauguzi walio raia wa kigeni ambao waliwaambukiza zaidi ya watoto wa Ki-Libya 400 na virusi vya UKIMWI. Tena kwa makusudi. Hamna jambo lisiloaminika kama hili.

Hata hivyo, sasa ni wazi kwamba hukumu hiyo ya kifo haitotekelezwa. Kuna matumaini kwamba wauguzi hao karibuni watakabidhiwa kwa Bulgaria.

Huenda tena hili lilikuwa ni suala la bei gani ya kulipa. Wazi kwa sasa ni kwamba familia za watoto hao walioambukizwa na visrusi vya UKIMWI watalipwa fidia. Na licha ya kukanushwa mara nyingi, fidia hiyo itagharimiwa kwa fedha kutoka nchi za Ulaya. Sasa mtu anaweza kuwaza na kupumua kwamba angalau mwishoni wale wote waliohusika na sakata hili watafaidika. Lakini hayo sio hakika bado, licha ya kwamba inaonekana vingine. Mambo sio rahisi hivyo, kama tunavofikiri.

Familia za watoto hao wa Ki-Libya wasionewe gere kwa msaada wowote watakaopewa. Lakini mtu haifai kusahau kwamba hali ya wauguzi hao bado sio wazi, na kwamba wao wamekaa gerezani kwa muda wa miaka minane huko Libya, huenda wakiwa hawana hatia yeyote. Kuna mabingwa wa kimataifa waliohakikisha kwamba Wa-Bulgaria hao hawana hatia. Wanasema upungufu wa hali ya usafi katika hospitali walizokuweko watoto hao huko Libya ndio sababu ya kuambukizwa na virusi hivyo.

Kwanini maoni ya mabingwa hao yanadharauliwa, ni jambo lisillofahamika. Hakuna hakimu wa Ki-Libya angeyeweza kusema kwamba makosa ya kuambuziwa virusi vya Ukimwi watoto 400 yanatokana na mfumo wa afya wa Libya, hivyo kuilaumu tabaka inayotawala nchini humo, chini ya mdikteta Muammar Ghaddafi. Kwa hivyo kumetafutwa njia ya kujitoa kimasomaso, na badala yake kuwabadikia hatia wauguzi hao wa kigeni.

Muammar al-Ghaddafi anajuwa thama vipi nchi za Ulaya zinavomhiatji yeye na nchi yake. Libya inafungua wazi milango yake sio tu kwa biashara inayoongezeka kutoka Ulaya, lakini pia ina hifadhi kubwa ya mafuta. Nchi hiyo inahitajiwa na Ulaya kuwa kama ukuta wa kuzuwia uhamiaji wa haramu wa watu wanaotokea Afrika kutaka kwenda Ulaya. Nchi za Magharibi zinapumua kwamba Libya imeachana na ugaidi, na hiyo ndio maana Ghaddafi ameweza kuwa na ujabari wa kuwashikilia kama mateka wauguzi hao wa kigeni ili kuendeleza maslahi yake. Na pale raia hao wa kigeni watakapoachwa huru sio muda mrefu kutoka sasa, hakutakuweko kizingiti tena cha kuweko uhusiano mzuri na nchi za Magharibi. Tawala nyingine zinaweza kujifunza kutoka mfano huu: vipi mtu anavoweza, kwa mafanikio, kuzibinya nchi za Magharibi.

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com