1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

HRW: Israel ilifanya uhalifu dhidi ya Wapalestina

Josephat Charo
20 Novemba 2025

Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limesema hatua ya Israel kuwafukuza maelfu ya Wapalestina kutoka kambi za wakimbizi Ukingo wa Magharibi 2025 ni uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

https://p.dw.com/p/53vjy
Jeshi la Israel limebomoa makazi na nyumba katika kambi ya wakimbizi ya Jenin na hakuna mahali ambapo wakimbizi wanaweza kurudi.
Jeshi la Israel limebomoa makazi na nyumba katika kambi ya wakimbizi ya Jenin na hakuna mahali ambapo wakimbizi wanaweza kurudi.Picha: Issam Rimawi/Anadolu/picture alliance

Shirika la Human Rights Watuch HRW limetoa wito wa hatua za haraka zichukuliwe na jumuiya ya kimataifa kuwawajibisha maafisa wa Israeli na kukomesha dhuluma zaidi. Wakati haya yakiarifiwa watu mashambulizi mapya ya Israel yamewaua watatu katika Ukanda Gaza mapema leo.

Shirika hilo limesema takriban wakazi 32,000 wa kambi za Jenin, Tulkarm na Nur Shams walilazimishwa kwa nguvu kuyahama makazi yao na vikosi vya Israeli wakati wa operesheni iliyopewa jina "Operation Iron Wall"  - "Operesheni ya Ukuta wa Chuma" iliyofanyika mnamo mwezi wa Januari na Februari. Ripoti ya shirika hilo yenye kurasa 105, yenye kichwa "Ndoto Zangu Zote Zimefutwa", inasema waliohamishwa wamezuiliwa kurudi, na mamia ya nyumba zilibomolewa.

Akizungumza na shirika la habari la Reuters jana Jumatano, Milena Ansari, mtafiti wa Human Rights Watch aliyefanya kazi ya kuiandaa ripoti hiyo, alisema, walichambua video na picha za setilaiti huria, na wakazungumza na watu wapatao 31 waliohojiwa, wakazi wa kambi hizi za wakimbizi ambao waliwaambia kuhusu ukatili wa kuhamishwa kwao kutoka kambini, kile ambacho vikosi vya ardhini vya Israeli vilikuwa vikikifanya kama vile kubomoa nyumba na majengo, kuharibu miundombinu katika kambi na wao kutojua pa kwenda na jinsi ya kutafuta makazi.

"Miezi 10 baada ya kuhamishwa kwao, hakuna hata mmoja wa wakazi wa familia aliyeweza kurudi majumbani mwao, kwa kuwa baadhi ya nyumba zao zimeharibiwa kabisa na kubomolewa. Kwa hivyo, kwa kweli hakuna nyumba ya kurudi." Aliongeza kusema.

Jeshi la Israeli lilisema katika taarifa kwa shirika la Reuters Jumatano kwamba lilihitaji kuibomoa miundombinu ya raia ili isiweze kutumiwa na wanamgambo. Halikusema ni lini wakazi wanaweza kurejea katika makazi yao.

Mikataba ya Geneva inakataza kuhamishwa kwa raia kutoka eneo linalokaliwa, isipokuwa kwa muda kwa sababu muhimu za kijeshi au usalama wao. Human Rights Watch ilisema maafisa wakuu waliohusika wanapaswa kushtakiwa kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Wakimbizi wa kipalestina wakiondoka kambi ya wakimbizi wa Jenin kufuatia operesheni ya jeshi la Israel, Januari 23, 2025.
Wakimbizi wa kipalestina wakiondoka kambi ya wakimbizi wa Jenin kufuatia operesheni ya jeshi la Israel, Januari 23, 2025.Picha: Majdi Mohammed/AP Photo/picture alliance

Ripoti hiyo inaelezea wanajeshi wakivamia nyumba, wakipora mali na kuamuru familia kutoka nje kupitia vipaza sauti vilivyowekwa kwenye ndege zisizo na rubani. Ilisema wakazi waliripoti kwamba matingatinga yaliharibu majengo walipokuwa wakikimbia na kwamba vikosi vya Israeli havikutoa makazi wala msaada, na kuziacha familia zikikusanyika katika nyumba za jamaa au kutafuta hifadhi katika misikiti, shule na mashirika ya kutoa misaada.

"Tunaishi maisha magumu sana"

Hisham Abu Tabeekh, ambaye alifukuzwa kutoka kambi ya wakimbizi ya Jenin, alisema kwamba familia yake haikuweza kuchukua chochote walipofukuzwa. Akizungumza na shirika la habari la Reuters Jumatano.Tabeekh alisema, "Tuliondoka nyumbani kwetu bila chochote, bila makazi, na tukahamia hapa mjini Burqin na tukakodisha nyumba. Hatuwezi kumudu kununua chakula, vinywaji, dawa, na hatuwezi kuendelea kumudu gharama, hatuwezi kumudu chochote, tunaishi maisha magumu sana."

Human Rights Watch ilisema iliwahoji Wapalestina 31 waliofukuzwa kutoka kambi hizo tatu na kuchanganua picha za setilaiti, maagizo ya ubomoaji na video zilizothibitishwa. Shirika hilo liligundua kuwa zaidi ya majengo 850 yalivunjiliwa mbali kabisa au kuharibiwa sana, huku tathmini ya Umoja wa Mataifa ikiweka idadi hiyo kuwa majengo 1,460. Kambi hizo, zilizoanzishwa miaka ya 1950 kwa ajili ya Wapalestina waliohamishwa baada ya dola ya Israelikuanzishwa mwaka wa 1948, zilikuwa na vizazi vingi vya wakimbizi.

Human Rights Watch ilisema kwamba katika kujibu maafisa wa Israeli waliandika kwamba operesheni hiyo ililenga kile walichokiita vipengele vya kigaidi, lakini haikutoa sababu ya kufukuzwa kwa watu wengi au marufuku ya kurudi.

HRW ilisema kufukuzwa huko, kulikofanyika huku umakini wa kimataifa ukielekezwa Gaza, ni sehemu ya uhalifu dhidi ya ubinadamu wa ubaguzi wa rangi na mateso.

Watu watatu wauwawa Gaza

Wakati haya yakiarifiwa, mashambulizi mapya ya Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, ulinzi wa raia wasema watu watatu wamekufa. Shirika la ulinzi wa raia la Gaza limesema Israel ilizindua mashambulizi mapya ya anga katika eneo la Palestina mapema Alhamisi na kuwaua watu watatu. Shirika hilo, ambalo linafanya kazi chini ya mamlaka ya Hamas, lilisema kulikuwa na "mashahidi watatu na 15 waliojeruhiwa" baada ya vikosi vya Israeli "kulipua jengo la makazi katika eneo la Bani Suheila, mashariki mwa Khan Yunis", yapata saa kumi alfajiri, huku Hamas na Israel zikishutumiwa kwa kukiuka makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutumika Oktoba 10.

Chanzo kutoka wizara ya mambo ya ndani ya Gaza inayoongozwa na Hamas, ambacho hakikutaka kutambuliwa, kilisema hakukuwa na mashambulizi mengine ya anga katika eneo hilo baada ya saa kumi na moja alfajiri lakini kilisema milio ya mizinga inaendelea kusikika katika eneo la Khan Yunis.

Kwa upande mwingine, Umoja wa Ulaya unajiandaa kutanua ujumbe wake wa polisi na ulinzi wa mpaka huko Gaza katika jitihada ya kusaidia mpango wa amani wa Marekani.