Hali ya Usalama nchini Ugiriki yazidi kuzorota huku mazishi ya kijana aliyeuawa na Polisi yakipangiwa leo. | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.12.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Hali ya Usalama nchini Ugiriki yazidi kuzorota huku mazishi ya kijana aliyeuawa na Polisi yakipangiwa leo.

Leo ni siku yamazishi ya kijana wa umri wa miaka 15 aliyepigwa risasi na maafisa wa Polisi nchini Uguriki. Ghasia za maandamano ambazo zimekuwa zikiendelea kwa muda wa siku nne sasa, zinaongezeka katika miji mikubwa.

Polisi wa kukabiliana na ghasia waimarisha usalama mjini Athens wakati wa siku ya nne ya maandamano yanayokumba nchi hiyo.

Polisi wa kukabiliana na ghasia waimarisha usalama mjini Athens wakati wa siku ya nne ya maandamano yanayokumba nchi hiyo.

Maandamano tayari yamesababisha mamia ya watu kujeruhiwa, uporaji na uharibifu mkubwa wa mali.

Shughuli katika mji mkuu wa Athens na miji mingine 6 nchini humo, zimekwama kabisa kufuatia maandamano hayo ambayo yametajwa kuwa mabaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika miongo kadha iliyopita.

Moshi wa mali zinazoteketezwa na gasi ya kutoza machozi kutoka kwa maafisa wa usalama,vimezagaa katika barabara za miji hiyo, huku wanafunzi wa vyuo vikuu na waandamanaji wengine wakiteketeza maduka, magari na hata benki, kwa ufupi hakuna jengo ambalo halikupata hasara mjini Athens miongoni mwayo ofisi za serikali na ile ya shirika la kitaifa la safari za Ndege.


Hali ya wasi wasi inazidi kuongezeka hasa wakati wa mazishi ya kijana huyo Alexis Grigoro-poulos yanayotarajiwa kufanyika alasiri ya leo katika makaburi ya baraza la manispaa ya mji wa Palio Faliro, kitongojini mwa mji wa Athens.

Ingawa hali ya usalama imeimarisha katika miji hiyo, maafisa wa usalama nchini Ugiriki wanaonekana kuzidiwa nguvu na waandamanaji hao wanaowarushia,mabomu ya petroli na kuwasha moto kufunga barabara.

Maandamanao hayo tayari yamesambaa hadi nchi nyingine kama vile Ujerumani,ambako raia wa Ugiriki waliandamana nje ya ubalozi mdogo wa nchi yao mjini Berlin kupinga mauaji hayo.

Waziri mkuu wa nchi hiyo Costas Karamanlis, ameahidi kumaliza mzozo huo kwa njia ya amani, kinyume na hofi inayosambaa kwamba serikali inamipango ya kutangaza sheria za kijeshi ili kukabiliana na ghasia hizo.

Waziri huyo mkuu pia amepangiwa kukutana na rais na viongozi wengine wa kisiasa kujadilia mzozo huo ambao unatishia uthabiti wa taifa zima.

Hatibu wa serikali alitoa taarifa ya kukanisha uvumi huo akisema kuwa unaenezwa na wapinzani wanaotaka kuchochea ghasia hizo hata zaidi.

Waziri wa usalama wa ndani Prokopis Pavlo-poulos amesema kuwa tayari maafisa wawili waliohusika na mauaji hayo wamekamatwa na kushtakiwa kwa kosa la kuu bila ya kukusudia.

Bado haijabainika wazi kilichopelekea kuuawa kwa kijana huyo aliyekuwa miongoni mwa kundi la vijana 30, ambao maafisa wa usalama wanadai kuwa walirushia mawe gari la Polisi.
 • Tarehe 09.12.2008
 • Mwandishi Eric Kalume Ponda
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GCDJ
 • Tarehe 09.12.2008
 • Mwandishi Eric Kalume Ponda
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GCDJ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com