Viwanda Ujerumani vyageukia uzalishaji wa vifaa vya ulinzi
3 Aprili 2026
Shirika la kusimamia maslahi ya Viwanda na Biashara nchini Ujerumani (DIHK) limesema sekta ya viwanda nchini Ujerumani katika kipindi hiki imegeukia zaidi kwenye uzalishaji wa vifaa vya ulinzi.
Utafiti uliofanywa na jarida moja la habari za biashara nchini Ujerumani umebaini kwamba karibu theluthi moja ya makampuni ya viwanda yameona fursa katika mifumo yao ya kibiashara kwenye sekta ya usalama na ulinzi.
Rainer Kambeck ambaye ni mtaalam katika shirika hilo amesema kwamba utafiti huo umeonyesha wazi ukuaji katika sekta ya ulinzi na hali hiyo imechangiwa na migogoro ya kikanda na ya kisiasa inayoendelea duniani.
Uchambuzi maalum wa DIHK unaonyesha kuwa kampuni moja kati ya sita za viwanda nchini Ujerumani tayari imeunganishwa katika mnyororo wa thamani kwenye sekta ya ulinzi.
Sekta ya utengenezaji wa magari ndiyo inayoongoza kwa asilimia 36.