1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Duru ya nne ya mazungumzo ya mpango wa nyuklia kuanza Vienna

John Juma
7 Mei 2021

Maafisa wa Marekani wanaelekea Vienna kushiriki awamu ya nne ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kuhusu mkataba wa nyuklia wa Iran. 

https://p.dw.com/p/3t5hH
Österreich | Treffen zum iranischen Atomabkommen in Wien
Picha: EU Delegation in Vienna/REUTERS

Afisa wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani asema kuna uwezekano wa kupatikana makubaliano kunusuru mkataba wa mpango ya nyuklia wa Iran katika wiki zijazo kabla ya uchaguzi wa Iran mwezi Juni.

Afisa wa Marekani amethibitisha pia kwamba kuna mazungumzo ya kina yanayoendelea pamoja na mazungumzo ambayo si ya moja kwa moja na Tehran ili kuwaachilia raia wa Marekani wanaoshikiliwa na Iran. Hata hivyo hakueleza ikiwa hilo ni sharti kwa Marekani kurejea katika mkataba huo wa mpango w anyuklia wa Iran.

Soma pia: Mazungumzo ya mpango wa nyuklia wa Iran yaahirishwa

Mashauriano yasiyo ya moja kwa moja yalianza mwanzo wa mwezi Aprili mjini Vienna kati ya Marekani na Iran, huku washirika wengine kwenye mkataba huo Uingereza, China, Ufaransa, Ujerumani, Urusi na Umoja wa Ulaya wakiwa kama wapatanishi.

Mazungumzo ya Vienna yanalenga kuirudisha Marekani kwenye mkataba wa Iran kuhusu nyuklia ambayo Marekani ilitoka ikiwa chini ya rais wa zamani DOnald Trump.
Mazungumzo ya Vienna yanalenga kuirudisha Marekani kwenye mkataba wa Iran kuhusu nyuklia ambayo Marekani ilitoka ikiwa chini ya rais wa zamani DOnald Trump.Picha: Carlos barria/AFP/Getty Images

Soma pia: Iran yaonya hujuma zinaathiri mazungumzo ya Vienna

Madhumuni yakiwa ni kuiwezesha Marekani kurejea katika mkataba huo unaojulikana pia kama JCPOA, ambao rais wa zamani wa Marekani Donald Trump aliiondoa nchi yake, lakini ambayo mrithi wake Joe Biden anataka kufufua.

 Ili hilo litimie, ni sharti Marekani na Iran zikubaliane kuhusu kuondolewa kwa vikwazo dhidi ya Iran vilivyorudishwa na Donald Trump, na vilevile Iran ikubali kutekeleza masharti ya mkataba huo.

Punde tu Trump aliiondoa Marekani kwenye makubaliano hayo yaliyosainiwa mwaka 2015, Iran iliachana na masharti iliyowekewa kuhusu uzalishaji wa zana za nyuklia.

Awamu tatu zilizopita za mazungumzo zilitajwa na afisa wa Marekani ambaye hakutaka kutambulishwa kuwa nzito au muhimu na zenye tija.

Urusi imesema inataka makubaliano yaafikiwe katika muda wa majuma mawili, kabla ya kampeni kuanza kuelekea uchaguzi wa Iran wa Juni 18, akisema kampeni hizo zinaweza kuyagubika mazungumzo hayo. Marekani haijaondoa uwezekano wa hilo kutimia.

Afisa huyo wa Marekani amekiri kwamba suala kuu kwenye mazungumzo hayo ni kwa kiwango gani uongozi wa Iran unataka makubaliano yatimie.

Roketi zaonekana katika kambi ya chini ya ardhini katika pwani ya Uajemi kusini mwa Iran Januari 8, 2021.
Roketi zaonekana katika kambi ya chini ya ardhini katika pwani ya Uajemi kusini mwa Iran Januari 8, 2021.Picha: Sepahnews/AA/picture alliance

"Ikiwa Iran itafanya uamuzi wa kisiasa kwamba kwa hakika inataka kurejea kwenye mkataba wa JCPOA kulingana na maafikiano ya awali, basi mapatano yatatimia haraka na utekelezaji pia utafanywa haraka. Lakini kwa sasa hatujui ikiwa Iran imeshafanya uamuzi huo,” amesema afisa huyo wa Marekani.

Kulingana na afisa huyo, swali hilo huenda likajibiwa kwenye mazungumzo ya Ijumaa.

Mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya amesema Marekani tayari imetoa pendekezo kabambe linalojumuisha kuondoa vikwazo kwa Iran katika sekta za Mafuta, gesi na benki, na imeonyesha nia ya kuwa na uwazi ili kulegeza vikwazo kuhusiana na ugaidi na masuala ya haki za binadamu.

Mwandiplomasia huyo ambaye hakutaka kutambulishwa, amesema Iran haijaonyesha utayari wowote wa kupunguza utaalamu wowote ambao imepata katika kazi kwenye kinu zakeau hata kuziharibu.

Tehran imekana kuwa na nia ya kutengeneza zana za nyuklia.

APE, AFPE; RTRE