1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Cruz na Sanders washinda Wisconsin

6 Aprili 2016

Ted Cruz wa chama cha Republican, katika kinyang'anyiro cha kuwania kuteuliwa mgombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa Marekani na mgombea wa Democratic, Bernie Sanders, wameshinda katika uchaguzi wa jimbo la Wisconsin.

https://p.dw.com/p/1IQU0
Picha: Reuters/K. Krzaczynski

Ushindi huo ni pigo kubwa kwa wagombea wengine wa vyama vya Republican, Donald Trump na chama cha Democratic, Hillary Clinton ambao wanaongoza kwa kuwa na wajumbe wengi hadi sasa. Trump amepungukiwa wajumbe 500 ili kuweza kufikia idadi ya wajumbe 1,237 wanaotakiwa ili kuweza kuidhinishwa na chama chake moja kwa moja kuwa mgombea.

Trump ana wajumbe 737 ikilinganishwa na Ted Cruz mwenye wajumbe 481. Ushindi wa Cruz ni njia kwa chama cha Republican kupambana ili kumzuia Trump, bilionea wa New York kuidhinishwa kugombea urais wa Marekani kupitia chama hicho, katika mchakato wa mwisho utakaofanyika mwezi Julai. Akizungumza baada ya ushindi huo, Cruz amewaambia waandishi wa habari kwamba usiku wa jana ulikuwa wa mabadiliko.

''Kama matokeo ya usiku yalivyoonyesha, ninaamini kwamba kampeni yetu itapata wajumbe 1,237 wanaohitajika kushinda kuteuliwa na chama cha Republican. Aidha, kabla ya mchakato wa mwisho wa Cleveland au katika machakato huo, kwa pamoja tutashinda wajumbe wengi na kwa pamoja tutamshinda Hillary Clinton mwezi Novemba,'' alisema Cruz.

Trump anasema atashinda

Kwa upande wake Trump amesema ana imani atafanikiwa licha ya kushindwa kwenye jimbo la Wisconsin, na amemshambulia mpinzani wake akisema Ted Cruz ni mbaya kuliko kikaragosi anayetumiwa na viongozi wa chama kujaribu kuwapokonya uteuzi wao.

Mgombea wa Democratic, Bernie Sanders
Mgombea wa Democratic, Bernie SandersPicha: Reuters/M. Kauzlarich

Wakati huo huo, Bernie Sanders amepata ushindi dhidi ya Hillary Clinton, ingawa bado yuko nyuma sana ya Clinton katika idadi jumla ya wajumbe muhimu. Ushindi wa Gavana huyo wa Vermont, umefikisha majimbo sita aliyoshinda.

Sanders bado anakabiliwa na kibarua kigumu cha kuwania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic, katika uchaguzi wa jimbo la New York, Aprili 19 na majimbo mengine matano ya Mashariki, Aprili 26.

Akizungumza na waandishi wa habari, Sanders amesema anaamina wana nafasi kubwa ya kushinda katika jimbo la New York ambalo lina wajumbe wengi zaidi na kumtaka Clinton kutokuwa na wasiwasi. Sanders pia anatarajiwa hivi karibuni kuelekeza nguvu zake katika majimbo ya Oregon na California, ambako timu yake ya kampeni inaamini kuwa anaweza kupata ushindi mkubwa.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTR,AFP
Mhariri: Iddi Ssessanga