1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

CONAKRY: Hali ya hatari yatangazwa Guinea

13 Februari 2007
https://p.dw.com/p/CCSg

Rais wa Guinea, Lansana Conté, ametangaza hali ya hatari nchini mwake. Katika hotuba yake kwa taifa iliyoonyeshwa moja kwa moja katika runinga, rais Conté ameliamuru jeshi kuchukua kila hatua inayohitajika kurejesha utulivu kufuatia maandamano mapya dhidi ya serikali yake.

Watu takriban tisa wameuwawa katika machafuko yaliyozuka katika mji mkuu Conakry.

Machafuko ya hivi punde yalitokea wakati vyama vya wafanyakazi vilipoanza tena mgomo wa kitaifa kuipinga serikali. Mgomo wa kazi uliitishwa kupinga uamuzi wa rais Conté kumteua mshirika wake wa karibu, Eugene Camara, kuwa waziri mkuu wa Guinea.

Viongozi wa vyama vya wafanyakazi wanasema rais Conté mwenye umri wa miaka 72 hafai tena kuiongoza nchi hiyo baada ya kuwa madarakani kwa zaidi ya miongo miwili.