1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaChina

China yasisitiza juu ya kuendeleza uwekezaji wa kigeni

Sylvia Mwehozi
17 Januari 2023

Makamu kiongozi wa China Liu He amesema kwamba Beijing itaendelea kufanya uwekezaji wa kigeni wakati alipohutubia kongamano la kila mwaka la uchumi duniani linalofanyika mjini Davos Uswisi.

https://p.dw.com/p/4MKPd
Weltwirtschaftsforum in Davos, Liu He
Picha: Markus Schreiber/AP Photo/picture alliance

Makamu huyo kiongozi wa China amelieleza kongamano la kiuchumi mjini Davos kwamba nchi hiyo ina matumaini uchumi wake utarejea katika mwelekeo wa hali ya ukuaji wa kawaida mwaka huu na inatarajia ongezeko katika uagizaji, uwekezaji na matumizi. Ziara ya mwanauchumi huyo wa China katika kongamano la mjini Davos, inaashiria ziara ya kwanza ya kiongozi wa ngazi ya juu wa China nje ya nchi tangu Beijing ilipoanza mwezi uliopita kuondoa sera yake ya kutokomeza kabisa Covid-19.

Lakini sera hiyo pia iliitenga China na ulimwengu mwingine kwa kipindi cha miaka mitatu na hivyo kudhoofisha uwekezaji wa kigeni. Matamshi ya Liu yanaashiria dalili za wazi za China kujihusisha tena na masuala muhimu pamoja na kuvutia tena uwekezaji wa kigeni wakati ikijaribu kufufua uchumi wake ambao mwaka jana ulikua kwa asilimia 3, ikiwa ni rekodi mbaya katika kipindi cha miaka 50.

Schweiz WWF Davos | Ursula von der Leyen
Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Arnd Wiegmann/REUTERS

Naye rais wa halmshauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen ametangaza mpango kabambe wa kukabiliana na China na Marekani katika kinyang'anyiro cha viwanda vya teknolojia rafiki kwa mazingira, wakati mpambano juu ya nishati ya kijani ukijitokeza katika kongamano la Davos. Von der Leyen amesema China inatoa ruzuku kwa viwanda vyake na kuzuia ufikiaji wa soko lake kwa makampuni ya Ulaya.

"Tunaona majaribio makali ya kushawishi uwezo wetu wa viwanda kuelekea China au kwingineko. Tuna hitaji la lazima la kufanya mabadiliko haya ya kupunguza hewa chafu bila kuwa na utegemezi mpya, tumejifunza somo," alisema von der Leyen.

UK | Olena Selenska in London
Mke wa rais wa Ukraine Olena ZelenskaPicha: Imageplotter/Avalon/Photoshot/picture alliance

Aidha mkuu huyo wa Umoja wa Ulaya pia amesisitiza wasiwasi wa Ulaya juu ya sheria ya kupunguza mfumuko wa bei ya Marekani, mfuko wa ruzuku wa mazingira wenye thamani ya karibu dola bilioni 370, ingawa alisema pande zote mbili zimekuwa zikifanya kazi kutafuta "suluhu" ambayo inaweza kujumuisha kuruhusu magari ya umeme yaliyotengenezwa na Umoja wa Ulaya kufaidika na sheria hiyo. Soma pia : Vita vya Ukraine, mdororo wa uchumi kugubika kongamano la Davos

Katika hatua nyingine mke wa rais wa Ukraine Olena Zelenska amehutubia kongamano hilo mjini Davos katika jaribio la kutafuta uungwaji mkono zaidi wakati nchi yake ikijitayarisha kuingia mwaka wa pili wa vita. Olena amewaeleza wajumbe wa kongamano hilo kwamba uvamizi wa Urusi ambao haukuwa umechochewa "umezitia kiwewe" familia nyongo kote nchini humo, akitoa wito kwa wajumbe wa kongamano kufikiria vita hivyo kupitia "macho ya watu ambao maisha yao yameingizwa katika machafuko".

Kuna idadi kubwa ya maafisa wa Ukraine katika mkutano huo wa Davos mwaka huu akiwemo naibu waziri mkuu wa kwanza Yulia Svyrydenko.