1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

China na Marekani zaungana kupambana na virusi vya Corona

Amina Mjahid
27 Machi 2020

Rais wa China amesema nchi yake na Marekani lazima ziungane kupambana na janga la Corona, huku mawaziri wa fedha wa Umoja wa Ulaya wakitakiwa kufikia mpango wa kuuokoa uchumi wao uliodhoofishwa kutokana na janga hilo.

https://p.dw.com/p/3a7U3
US Präsident Donald Trump in China
Picha: picture-alliance/dpa/TASS/A. Ivanov

Rais Xi Jinping wa China pia ameitolea wito Marekani kuimarisha uhusiano wa nchi hizo mbili hasaa baada ya kutupiana maneno katika wiki za hivi karibuni kufuatia virusi hivyo. Kulingana na shirika la habari la China,  Xi alimuambia Trump kupitia njia ya simu kwamba anatumai Marekani itachukua hatua madhubuti za kuimarisha uhusiano huo.

Xi pia ametoa wito kwa mataifa hayo mawili kufanya kazi pamoja kukabiliana na virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID 19.  Katika kuonesha mafanikio ya mazungumzo hayo rais Trump aliandika katika mtandao wake wa twitter kuwa walikuwa na mazungumzo ya kufana na Xi na kwamba viongozi wote wawili wamelijadili kwa kirefu janga la Corona.

Trump ameendelea kusema kuwa China imepitia mengi na inavielewa vyema virusi hivyo, na anaheshimu hatua ya nchi hizo mbili kufanya kazi pamoja kukabiliana na virusi vya Corona.

Trump pamoja na waziri wake wa mambo ya nje Mike Pompeo waliikasirisha China mwezi huu kwa kuvielezea virusi vya Corona kama "virusi vya China” wakati wakizungumzia mripuko wa virusi hivyo vilivyogundulika kwa mara ya kwanza mjini Wuhan nchini China mwezi Desemba mwaka jana.

Marekani kwa sasa ina idadi kubwa ya maambukizi ya ugonjwa wa COVID 19 kuliko nchi nyengine yoyote duniani huku kukiwa na idadi kubwa zaidi ya watu waliokosa ajira wakati janga la virusi vinavyosababisha ugonjwa huo likiendelea kuitafuna dunia.

Virusi vya Corona vinaendelea pia kuuvuruga uchumi wa dunia

Coronavirus in Mexiko Herstellung von Scxhutzmasken (Reuters/J.L. Gonzalez)
Picha: Reuters/J. L. Gonzalez

Mifumo ya afya katika mataifa yaliyoendelea inaendelea kulemewa huku ikikadiriwa kuwa watu milioni 1.8 duniani huenda wakafariki mwaka huu kutokana na virusi hivyo. China ambayo awali ilionekana kujaribu angalau kuvidhibiti virusi hivyo hii leo imeripoti maambukizi 65 mapya hali inayoonesha  ugumu wa kuvidhibiti virusi hivi .

Zaidi ya watu 530,000 wameambukizwa virusi vya Corona duniani. Uhispania, Ufaransa, Italia na Marekani zinabakia kuwa nchi zilizoathirika zaidi na virusi hivyo.

Sio tu athari za kiafya zinazoshuhudiwa kutokana na janga hili lakini pia athari za kiuchumi nazo zinaonekana kuanza kuiyumbisha dunia. Viongozi wa Umoja wa Ulaya hapo jana, waliwaambiwa mawaziri wa wa fedha kuwa wana wiki mbili za kufikia mpango wa kuufufua uchumi uliodhoofishwa na mgogoro wa virusi vya Corona.

Katika mkutano uliodumu saa sita kupitia njia ya video, viongozi wa nchi wanachana 27 wa Umoja huo walishindwa kupata hatua ya pamoja ya kukabiliana na virusi hivyo.

Mataifa tisa ikiwemo Italia na Uhispania  walipendekeza kutolewa msaada waliouita "dhama ya Corona” utakaowawezesha kukopa ili kuokoa uchumi wa mataifa yao, lakini wito huo ulikataliwa na mataifa tajiri katika umoja huo ikiwemo Ujerumani.

Vyanzo: dpa, ap, reuters