Chaguzi za Majimbo Ufaransa zahanikiza Magazetini | Magazetini | DW | 07.12.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Chaguzi za Majimbo Ufaransa zahanikiza Magazetini

Ushindi wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia-FN katika chaguzi za majimbo nchini Ufaransa wahanikiza magazetini.Sawa na mabadiliko ya tabianchi na ripoti ya shirika la upelelezi la Ujerumani kuhusu Saud Arabia

default

Kiongozi wa chama cha kibaguzi cha FN nchini Ufaransa Marine Le Pen

Tuanzie lakini Ufaransa ambako chama kinachoeneza chuki dhidi ya wageni Front National kimeupindua wezani wa kisiasa kwa kunyakua zaidi ya asili mia 30 ya kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa majimbo. Gazeti la Rheinpfalz linaandika:"Mbinu za Front National zimefanikiwa. Kueneza hofu na kuwaahidi kinga watu walioingiwa na wasi wasi dhidi ya ulimwengu uliosalia-hizo ndizo karata walizocheza wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia. Kundi hilo la ukoo wa Le Pen wakitanguliwa na Marine na mtoto wa nduguye anaeona mbali Marion Maréchal wamefanikiwa katika uchaguzi huo wa majimbo kuwahadaa watu kwa kueneza picha za uadui na hofu. Wanajulikana pia linapohusika suala la kueneza hisia za chuki dhidi ya wahamiaji,waislam na Ulaya. Hawakuhitaji mengi na mengi ya kupendekeza Front National hawana pia. Mwongozo wa chama hicho cha siasa kali za mrengo wa kulia haujalengwa kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayotokana na woga naiwe mapambano dhidi ya vitisho vya kigaidi au jinsi ya kuhimiza ukuaji wa kiuchumi."

Gazeti la "Badische Neuste Nachrichten" linalinganisha madaraka ya majimbo ya Ufaransa na yale ya Ujerumani na kuandika:"Madaraka ya majimbo ya Ufaransa si makubwa yakilinganishwa na madaraka ya majimbo nchini Ujerumani. Hata hivyo duru ya kwanza ya uchaguzi wa majimbo imesababisha kishindo kilichopindukia mipaka ya Marseille au Lille. Kwasababu inaonyesha jinsi wapigakura waliovunjia moyo wanavyoweza kuvutiwa kwa wingi na siasa kali za mrengo wa kulia. Kizingiti kilichokuwa kikiwazuwia wananchi kutokiunga mkono chama kinachoeneza hisia za chuki dhidi ya Ulaya na wahamiaji kinaonyesha kimevunjika.

Athari za siasa kali za mrengho wa kulia barani Ulaya

Gazeti la "Der Neue Tag" linahofia siasa kali za mrengo wa kulia zisije zikaenea katika Umoja wa ulaya.Gazeti linaendelea kuandika:"Kupata nguvu vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia barani Ulaya ni kishindo kwa Umoja wa Ulaya kwasababu hisia hizi mpya za kizalendo haziambatani na wazo la mshikamano wa ulaya. Kwa bahati nzuri uchaguzi wa Ulaya hautofanyika kabla ya msimu wa kiangazi mwaka 2019. Hadi wakati huo,mwenyekiti wa baraza la ulaya Donald Tusk,mwenyekiti wa halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya Jean-Claude Juncker na spika wa bunge la ulaya Martin Schulz watabidi wawe wameshakubaliana kuzungumza kwa kauli moja. La sivyo wazo la kuwepo Ulaya moja litafikia kikomoni.

Matokeo ya Mkutano wa Mabadiliko ya Tabianchi

Mada yetu ya mwisho magazetini inatufikisha Paris ambako mkutano wa mabadiliko ya tabianchi umeingia awamu yake muhimu na ya mwisho.Gazeti la "Main Post" linaandika:"Kitakachotokea?Hakuna chochote.Mambo si mabaya eti. Mwishoni mwa mkutano huo wa kilele watu watashangiria na kutia saini makubaliano-washiriki kila mmoja atafuata njia yake na mataifa yataendelea na shughuli zao kama kawaida. Lakini maafa yatakapopiga tena na kuangamiza kila kilichoko,maeneo yakiwa hayakaliki-pale idadi ya wakimbizi wa mabadiliko ya tabia nchi itakapoongezeka kwa nguvu na kuyafanya mataifa tajiri kiviwanda kutojua tena la kuanya,hapo pengine ndipo kitakapopatikana cha kufanya. Pengine lakini maji yatakuwa yameshazidi unga.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri . Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com