CDU yamchagua Laschet kuwa mgombea wa ukansela | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.04.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

CDU yamchagua Laschet kuwa mgombea wa ukansela

Baraza Kuu la chama cha Christian Democratic Union, CDU nchini Ujerumani cha Kansela Angela Merkel limemchagua Armin Laschet kuwa mgombea wa ukansela katika uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika baadae mwaka huu. 

Uchaguzi huo wa kurithi kiti cha Kansela umefanyika mapema leo asubuhi baada ya mazungumzo yaliyodumu kwa takriban saa sita. Baada ya mazungumzo hayo, baraza hilo kuu la CDU lenye wajumbe 46 lilipiga kura ya siri mtandaoni.

Wajumbe 31 ambao ni sawa na asilimia 77.5 walimuunga mkono waziri mkuu wa jimbo lenye watu wengi la North Rhine-Westphalia, Armin Laschet.

Mpinzani wake, Markus Soeder, ambaye ni waziri mkuu wa jimbo tajiri la Bavaria na kiongozi wa chama ndugu cha CSU, alipata asilimia 22.5 baada ya kuchaguliwa na wajumbe tisa.

Utayari wa kuwania nafasi ya ukansela

Akizungumza baada ya uchaguzi huo, Laschet  kiongozi wa sasa wa CDU ameelezea utayari wake kusimama katika uchaguzi uliopangwa kufanyika mwezi Septemba.

''Niko tayari kuwania nafasi hii kwa niaba yetu. Kuna mengi ya kujadiliwa, Ulaya inaiangalia Ujerumani jinsi inavyoendelea, ulimwengu unatarajia kuiona Ujerumani iliyo tulivu na hivyo chama cha Democratic Union pia tuna jukumu maalum,'' alifafanua Laschet.

Deutschland PK Markus Söder Kanzlerkandidaten Union

Kiongozi wa CSU, Markus Soeder

Tangu awali, Soeder, ambaye ni maarufu zaidi kwenye kura za maoni kuliko Laschet, ameshasema kwamba ataheshimu uamuzi wa CDU na kujitoa kwenye kinyang'anyiro hicho bila kinyongo. Hata hivyo, kiongozi huyo wa CSU anatarajiwa kuzungumza badae kuhusu uchaguzi huo.

"Sisi kama CDU na pia mimi mwenyewe, tunaheshimu uamuzi wowote. Utayari wangu siku zote ni kuiunga mkono nchi yetu na kuufanya muungano wetu kuwa muhimu. Lakini uamuzi wa kukubali au kutokubali ni kitu ambacho CDU inaweza kufanya. Ni chama ndugu, siku zote itabakia hivyo," alibainisha Soeder.

Wajumbe sita hawakuhudhuria kikao

Msemaji wa chama cha CSU amesema wajumbe sita hawakuwepo katika kikao hicho cha usiku wa kuamkia leo ambacho kimehitimisha wiki kadhaa za kile kilichoonekana kama vita vya madaraka vya kumrithi Kansela Merkel.

Laschet aliitisha mkutano wa usiku uliofanyika kwa njia ya mtandao ili kufikia maamuzi ya suala la mgombea. Laschet mshirika wa muda mrefu wa Kansela Merkel tayari alipata kuungwa mkono na maafisa wa ngazi ya juu wa CDU, wiki iliyopita.

Soma zaidi: Kiongozi wa CSU yuko tayari kugombea ukansela

Kwa pamoja muungano wa vyama vya kihafidhina nchini Ujerumani ambao kwa sasa uko katika serikali ya mseto na chama cha Social Democratic, SPD, kwa kawaida humchagua mgombea mmoja kwa ajili ya kugombea nafasi ya ukansela. Lakini mwaka huu, mkuu wa kila chama alitaka kugombea nafasi hiyo.

(DPA, AP, AFP, Reuters)