Brexit: Wabunge wa Uingereza wampinga Waziri Mkuu Theresa May | Matukio ya Kisiasa | DW | 26.03.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Uingereza

Brexit: Wabunge wa Uingereza wampinga Waziri Mkuu Theresa May

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May akiri kwamba haungwi mkono vya kutosha kuupitisha mpango wake wa Brexit. Wabunge wamepania kuunga mkono njia mbadala ili kuondosha mkwamo katika mchakato wa Brexit.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May amesema hakuna idadi ya kutosha ya wabunge wa kuunga mkono mpango wake juu ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya ambao umeshakatiliwa mara mbili. Waziri mkuu May alisema hayo jana jioni alipowahutubia wabunge wa nchi yake ili kuwapa taarifa juu ya mazungumzo yake na viongozi wa Umoja wa Ulaya wiki iliyopita.

Hata hivyo bibi May amesema anatumai hali inaweza kubadilika wiki ijayo. Mpango wa waziri mkuu huyo juu ya kujiondoa Umoja wa Ulaya unapaswa kupitishwa na wabunge mnamo wiki hii ili Uingereza iweze kuondoka kutoka kwenye Umoja huo.

Waziri mkuu May bado anaendelea na juhudi za kujaribu kuwashawishi wabunge wauunge mkono mpango wake. Kiongozi huyo wa Uingereza amesema ni muhimu kwa bunge la nchi yake kuyazingatia matokeo ya kura ya maoni iliyofanyika mnamo mwaka 2016 badala ya kutafakari wazo la kufanyika kura nyingine ya maoni juu ya Brexit. 

Akijibu tamko la Waziri Mkuu May kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Jeremy Corbyn amesema sasa wakati umefika kwa bunge kuudhibiti mchakato wa Brexit. Kiongozi huyo wa chama cha Labour amesema serikali ya May inaushughulikia mchakato wa Brexit kwa njia ya kufedhehesha.

Kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani nchini Uingereza Jeremy Corbyn(Reuters TV)

Kiongozi wa chama kikuu cha Upinzani nchini Uingereza Jeremy Corbyn

Corbyn pia amemlaumu Waziri Mkuu kwa kuwachonganisha wabunge na wananchi kwa kutoa kauli ambayo haikuwa ya busara wiki iliyopita. Kiongozi huyo wa chama kikuu cha upinzani amemtaka Waziri Mkuu May asikilize maoni ya wananchi waliofanya maandamano makubwa jijni London mwishoni mwa wiki iliyopita wakitoa mwito wa kufanyika kura nyingine ya maoni juu ya Brexit.

Hapo Jumatatu usiku wabunge wa Uingereza walipiga kura kadhaa za kuonyesha mwelekeo wa njia mbalimbali za kufanikisha lengo la Brexit. Wabunge wamepiga kura juu ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuudhibiti mchakato wa Brexit kwa ajili ya kupata idadi kubwa ya wabunge watakaoipigia kura njia mbadala ya kuuondosha mkwamo uliopo.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje Alistair Burt amejiuzulu ili aweze kupiga kura dhidi ya serikali na hivyo kuunga mkono pendekezo juu ya bunge kuudhibiti mchakato wa Brexit. Na siku ya Jumanne wabunge wataendelea kuyapigia kura mapendekezo kadhaa ya kuonyesha muelekeo wa hatua zinazoweza kupitishwa. 

Wakati huo huo Umoja wa Ulaya unaendelea kujitayarisha ili kuikabili hali, endapo Uingereza itaamua kujiondoa kutoka kwenye Umoja huo bila ya mkataba. Msemaji wa Umoja wa Ulaya Margaritis Schinas ameeleza kwamba uwezekano wa Uingezera kuondoka bila ya mkataba unazidi kuwa mkubwa.   

Wiki iliyopita Umoja wa Ulaya uliiongezea muda Uingereza hadi tarehe 12 mwezi Aprili ili kuamua juu ya utaratibu wa Brexit. Ikiwa mkataba wa Waziri Mkuu May hautapitishwa mnamo wiki hii, Umoja wa Ulaya umeipa Uingereza muda wa hadi hapo tarehe 22 Mei yaani siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa bunge la Umoja wa Ulaya.  

Vyanzo: RTRE/DPA//p.dw.com/p/3Fdc7

 

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com