1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Blinken ataka msimamo wa G7 kuhusu vita vya Israel na Hamas

7 Novemba 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken amesema ni muhimu kuwepo tamko la wazi kuhusu vita kati ya Israel na kundi la Hamas.

https://p.dw.com/p/4YWMs
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken akiwa Jordan
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony BlinkenPicha: Jonathan Ernst/Reuters Pool/AP/dpa/picture alliance

Blinken ameutoa wito huo alipokuwa akifungua mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa mambo ya nje wa Kundi la mataifa ya Magharibi yaliyoendelea kiviwanda G7 huko nchini Japan.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan Yoko Kamikawa ameelezea vipengee muhimu vitakavyojadiliwa kuhusu mzozo huo wa Mashariki ya Kati:

"Kuhusu hali ya dharura huko Palestina na Israel, tulisisitiza dhamira yetu ya kuachiliwa mara moja kwa mateka, kuhakikisha usalama wa raia, uheshimishwaji wa sheria za kimataifa kwa pande zote zinazohusika, kuwepo utulivu wa haraka katika mzozo huu, kuboresha hali ya kibinadamu na kutoa wito wa kusitishwa mapigano kwa sababu za kiutu," alisema Kamikawa.

Mawaziri hao wa mahusiano ya kigeni wa G7 wanatarajia pia kujadili uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, suala la mahusiano na Asia ya Kati yenye utajiri wa rasilimali, lakini pia ushawishi wa China unaozidi kuimarika duniani.