1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kukutana na Mrithi wa Ufalme wa Saudia MBS

Bruce Amani
15 Juni 2022

Rais Joe Biden wa Marekani atakutana na mrithi wa kiti cha Ufalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman mwezi ujao. Uamuzi huo unaweka pembeni juhudi za kumtenga mwanamfalme huyo kuhusiana na mauaji ya Jamal Khashoggi

https://p.dw.com/p/4CjA4
USA Tornado Kentucky | Besuch des US-Präsidenten Joe Biden
Picha: Gemunu Amarasinghe/AP Photo/picture alliance

Ikulu ya White House imeuwekea kikomo uvumi wa wiki kadhaa kwa kutangaza kuwa Biden atakwenda Israel, Ukingo wa Magharibi wa Wapalestina, na Saudi Arabia kuanzia Juali 13 hadi 16, ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya Mashariki ya Kati tangu alipongia madarakani.

Kando na mikutano na viongozi wa maeneo hayo matatu, atahudhuria mkutano wa kilele wa Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Ghuba nchini Saudia.

Biden anatarajiwa kushinikiza kuongezwa uzalishaji mafuta, kwa matumaini ya kudhibiti kupanda kwa gharama za amfuta na mfumuko nchini Marekani kabla ya kufanyika uchaguzi wa katikati ya muhula ambao chama chake cha Democratic kinakabiliwa na hatari ya kushindwa vibaya.

Saudia Arabien Kronprinz Mohammed bin Salman
MBS anatuhumiwa kupanga mauaji ya KhashoggiPicha: Saudi Royal Court/REUTERS

Lakini mkutano wake na mwanamfalme wa Saudia, anayefahamika kama MBS, utaashiria mabadiliko makubwa ya utata.

Watetezi wa haki za binaadamu na baadhi ya washirika wa chama cha Democratic walimtahadharisha Biden dhidi ya kuzuru Saudia, wakisema ziara ya aina hiyo bila ya kwanza kupewa uhakikisho wa kuheshimu haki za binaadamu inaweza kutuma ujumbe kwa viongozi wa Saudia kwamba hakuna madhara yoyote kwa ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu. Msemaji wa  wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Ned Price amesema suala la haki za binaadamu mara zote linakuwa meza. ''Huu ni uhusiano ambao maslahi mengi yanahusika. Bila shaka kuna suala la itikadi kali, la ugaidi. Tumeshirikiana kwa karibu na washirika wetu wa Saudia kwa miaka mingi katika kupambana na ugaidi. Kuna suala la Yemen.''

Soma pia: Saudi Arabia yadai aliyekamatwa na Ufaransa hahusiki na mauaji ya Khashoggi

Wasaudia wametuhumiwa kwa ukamataji wa watu wengi, mauaji na kuwatesa wapinzani. Wakati akiwa mgombea wa urais, Biden alisema mauaji ya mwaka wa 2018 na kukatwakatwa vipande Jamal Khashoggi – mkaazi wa Marekani na mzaliwa wa Saudia aliyefahamika kwa kuandika Makala za ukosoaji kuhusu watawala wa ufalme huo katika gazeti la Washington Post – yaliifanya nchi hiyo kutengwa kabisa na jamii ya kimataifa.

Matokeo ya uchunguzi wa kijasusi wa Marekani yaliyotolewa na utawala wa Biden yalionyesha kuwa MBS ndiye aliyepanga operesheni hiyo.

Saudi Arabia imethibitisha ziara ya Biden kupitia ujumbe wa moja kwa moja, ikisema kuwa Biden atakutana na Mfalme Salman na kisha mrithi wa kiti chake.

afp, ap