1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kwa Waarabu 'Marekani haitaiacha Mashariki ya Kati'

Zainab Aziz Mhariri: Chilumba Rashid
16 Julai 2022

Rais Joe Biden amewaambia viongozi wa Kiarabu kwamba Marekani itaendelea kushiriki kikamilifu katika maswala ya Mashariki ya Kati na haitaruhusu ushawishi wa mataifa mengine kwenye eneo hilo.

https://p.dw.com/p/4EEqS
Saudi Arabien Ankunft US-Präsident Biden
Picha: EVELYN HOCKSTEIN/REUTERS

Rais wa Marekani Joe Biden alisema katika mkutano wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba (GCC) mjini Jeddah, Saudi Arabia kwamba Marekani haiko tayari kuacha nafasi itakayojazwa na China, Urusi au Iran katika eneo la Mashariki ya Kati.

Rais Joe Biden na viongozi wa Kiarabu kwenye mkutano wa kilele wa GCC
Rais Joe Biden na viongozi wa Kiarabu kwenye mkutano wa kilele wa GCCPicha: Mandel Ngan/AFP/Getty Images

Biden aliwataka viongozi waliokusanyika kwenye mkutano wa kilele wa nchi za Kiarabu kuzingatia haki za binadamu kama nguvu kubwa ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.

Biden aliwaambia viongozi wa Kiarabu katika hotuba ya kuanza mkutano huo kwamba Marekani imewekeza katika kujenga mustakabali mzuri wa eneo la Mashariki ya Kati, kwa ushirikiano na washirika wote wa eneo hilo na aliwahakikishia kuwa Marekani haiendi popote bali itashiriki kikamilifu katika maswala ya Mashariki ya Kati.

Mkutano huo wa Jumamosi umefanyika katika siku ya mwisho ya ziara ya Biden huko Mashariki ya Kati na uliwaleta pamoja viongozi wa mataifa sita ya Ghuba pamoja na wale wa nchi za Misri, Jordan na Iraq.

Rais huyo wa Marekani aliangazia zaidi juu ya mkutano huo na kuliweka kando swala la mkutano wake na mirithi wa mfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman. Kukutana kwake na kiongozi huyo kumekosolewa mno nchini Marekani juu ya vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu nchini Saudi Arabia.

Rais wa Marekani Joe Biden
Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Evan Vucci/AP/picture alliance

Shirika la Habari la Reuters limeandika kwamba Biden anatafuta kuanzisha sura mpya katika ushiriki wa Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, kwa matumaini ya kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi na ulinzi na mataifa ya Kiarabu.

Rais wa Marekani Joe Biden alikwenda Saudi Arabia akitarajia kufanikisha makubaliano juu ya hatua za kuongeza uzalishaji wa mafuta ili kusaidia katika kupunguza bei ya petroli ambayo imepanda mno na kusababisha kuongezeka kwa mfumuko wa bei katika kipindi cha zaidi ya miaka 40 jambo linaloathiri umaarufu wake nchini Marekani.

Hata hivyo, rais huyo wa Marekani ameondoka kwenye eneo hilo mikono mitupu ila tu kuwa na matumaini kwamba juhudi zake za kidiplomasia zitasaidia katika kulisukuma kundi la nchi wanachama wa nchi zinazozalisha mafuta OPEC+ katika kuamua kuongeza uzalishaji wa mafuta watakapokutana Agosti 3.

Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia Mrithi wa Mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.
Kushoto: Rais wa Marekani Joe Biden. Kulia Mrithi wa Mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman.Picha: BANDAR ALGALOUD/REUTERS

Biden alikutana siku ya Ijumaa na Mrithi wa Mfalme, Mohammed bin Salman ambaye kwa upande wake amesema Saudi Arabia imechukua hatua za kuzuia kurudiwa kwa makosa kama mauaji ya Khashoggi lakini Marekani pia inapasa kujua kuwa nayo imefanya makosa kama hayo nchini Iraq na kwengineko na kwamba kwa Marekani kujaribu kulazimisha maadili fulani kwa nchi zingine jambo hilo linaweza kuleta matokeo mabaya.

Nembo ya OPEC
Nembo ya OPECPicha: Pavlo Gonchar/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Rais huyo mwenye umri wa miaka 79 hapo awali alimtenga mwana mfalme mwenye umri wa miaka 36 kutokana na vitendo vya ukiukaji wa haki za binadamu, hasa mauaji ya mwandishi Habari Jamal Khashoggi, ambaye maafisa wa ujasusi wa Marekani wanamtuhumu kuwa aliiidhinsiha mauaji hayo.

Viongozi wa Kiarabu na nchi ziungine 3 pamoja na Rais wa Marekani Joe Biden mjini Jeddah kwenye mkutano wa GCC+3.
Viongozi wa Kiarabu na nchi ziungine 3 pamoja na Rais wa Marekani Joe Biden mjini Jeddah kwenye mkutano wa GCC+3.Picha: Mandel Ngan/Pool/REUTERS

Hata hivyo Biden ametafakari na kutambua kuwa anahitaji kurekebisha uhusiano kati ya Marekani na Saudi Arabia ili kukabiliana na kupanda kwa bei ya gesi na pia kuleta utulivu katika eneo tete la Mashariki ya Kati.

Vyanzo:AP/DPA/RTRE