1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bayern yajiandaa kwa msimu mgumu Bundesliga

Deo Kaji Makomba
8 Septemba 2020

Likizo tamu zimemalizika kwa washindi mara tatu timu ya Bayern Munich. Katika siku kumi kocha wa timu hiyo Hansi Flick lazima awe na kikosi kinachofaa, wakati maswali ya wafanyakazi bado hayajajibiwa kabla ya msimu.

https://p.dw.com/p/3iAnf
Champions League Finale 2020 Paris vs Bayern München | Hansi Flick
Picha: Imago Images/Panoramic

Zikiwa zimepita siku 16 tu mara baada ya ushindi wa kombe la ligi ya mabingwa barani Ulaya huko Lisbon na likizo fupi, nyota wa klabu ya soka ya Bayern Munich wamerudi kwenye majukumu yao ya soka. Vipimo vya virusi vya Corona na mafunzo ya kimtandao, yako kwenye ratiba ya kikosi cha Hansi Flick siku ya Jumanne.

Ijumaa wiki hii, Manuel Neuer na wenzake watafanya mazoezi ya pamoja tena katika viunga vya mitaa ya Saebener baada ya vipimo vya afya vya radiolojia.

"Kuanza msimu mpya mishale ya saa zote zimewekwa katika sifuri," alisema mwenyekiti wa klabu hiyo Karl-Heinz Rummenigge, akimaanisha ni kama wana aanza mwanzo.

Katika siku kumi kocha wa timu hiyo Hansi Flick lazima awe na kikosi imara
Katika siku kumi kocha wa timu hiyo Hansi Flick lazima awe na kikosi imaraPicha: Getty Images/AFP/M. Lopes

Kocha Flick ana siku kumi tu kupata wachezaji wake tayari kwa mechi yake ya kwanza ya ushindani ya msimu ya Bundesliga dhidi ya Schalke ,mnamo Septemba 18. "Kuna msemo huu mzuri: Mafanikio hayamilikiwi kamwe, yanakodishwa tu na kodi ni ya kila siku,” Flick amebainisha.

"Sote tunajua kwamba Bundesliga itakuwa na upinzani zaidi. Borussia Dortmund ilipata nguvu, Leipzig pia ni wapinzani wenye nguvu, Bayer Leverkusen na Borussia Moenchengladbach."

Niklas Suele na mchezaji mgeni Leroy Sane wanarudi kutoka katika majukumu yao katika timu ya taifa Ujerumani. Suele anataka kurejesha nafasi yake ya kuanza kwenye safu ya ulinzi baada ya kipindi kigumu alichokabiliana nacho kutokana na kuwa majeruhi.