1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Zelensky: Musiisahau Ukraine wakati wa vita dhidi ya Iran

18 Machi 2026

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amewatolea wito washirika wa Magharibi kutoisahau nchi yake wakati huu macho yakielekezwa Mashariki ya Kati kufuatia vita vilivyoanzishwa na Marekani na Israel dhidi ya Iran.

https://p.dw.com/p/5AbG5
Uingereza London 2026 | Keir Starmer na Volodymyr Zelensky wakiwa Downing Street
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (kulia) akizungumza na mgeni wake, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine jijini London siku ya Jumanne (Machi 17, 2026).Picha: Suzanne Plunkett/AFP

Akizungumza akiwa ziarani nchini Uingereza siku ya Jumanne (Machi 17), Zelensky alijaribu kuonesha mfanano baina ya tawala za Urusi na Iran, ambazo kwa maneno yake ni "ndugu wanaounganishwa na chuki zao", na kwamba tawala za aina hiyo "kamwe haziwezi kuachiwa zikashinda."

Hata hivyo, rais huyo wa  Ukraine ambaye alikuwapo London kusaka uungaji mkono zaidi wa Waziri Mkuu Keir Starmer, alisema mbele ya mwenyeji wake huyo kwamba bado juhudi za kidiplomasia ni muhimu kumaliza vita nchini mwake.

"Pia, bila kusahau kuhusiana na juhudi zetu za kidiplomasia na mazungumzo na pale tulipo na Wamarekani na Warusi, tunapaswa kujadili mada hii tete. Na bila shaka kuhusu Mashariki ya Kati. Hili lina athari kubwa kwetu Ukraine na kwa Ulaya nzima." Alisema Zelensky.

Akiunga mkono maneno ya mgeni wake,  Starmeralisema licha ya vita kwenye Mashariki ya Kati kubeba uzito mkubwa kutokana na kuhusisha kwake pande nyingi kwa wakati mmoja, dunia inapaswa kuendelea kulishughulikia suala la vita vya Urusi nchini Ukraine na kulimaliza haraka iwezekanavyo.

"Hapana shaka kuna mgogoro wa Iran unaoendelea kwenye eneo la Mashariki ya Kati, lakini hatuwezi kupoteza umakini wetu kwa kile kinachoendelea nchini Ukraine na haja ya kuunga mkono huko. Na pili, ni muhimu sana kuwa wawazi kwamba Putin hawezi kuwa mfaidikaji wa mgogoro wa Iran, ama iwe ni kwenye bei za mafuta ama kuondoshwa kwa vikwazo." Alisema Starmer.

Marekani yakosolewa

Mkutano huu wa London unafanyika siku chache baada ya Marekani kuondosha kwa muda vikwazo vyake dhidi ya mauzo ya mafuta ya Urusi ili kupunguza shinikizo kwenye usambazaji wa bidhaa hiyo duniani linalotokana na vita vinavyoendelea sasa kwenye Mashariki ya Kati vilivyoanzishwa na uchokozi wake na Israel dhidi ya Iran kwa wiki ya tatu sasa.

Uingereza London 2026 | Mfalme Charles III na Volodymyr Zelensky wakiwa Kasri la Buckingham
Mfalme Charles wa Tatu wa Uingereza (kulia) akimkaribisha mgeni wake, Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, katika Kasri la Buckingham siku ya Jumanne (Machi 17, 2026).Picha: Aaron Chown/Avalon.red/IMAGO

Zelensky na baadhi ya viongozi wa Ulaya waliikosowa hatua hiyo ya Marekani kulegeza vikwazo dhidi ya Urusi, wakisema inaipa Urusi fursa na fedha za kuendeleza na mashambulizi yake dhidi ya Ukraine.

Zelensky alikutana pia na Mfalme Charles wa Tatu kwenye Kasri la Buckhingham kabla ya kukutana na baadhi ya wajumbe wa mabaraza mawili ya Bunge la Uingereza, ambao aliwaambia mataifa mengine yanaweza kujifunza teknolojia ya droni na akili bandia kwa ajili ya ulinzi kutoka nchi yake.