Xi Jinping ziarani Korea Kaskazini | Matukio ya Kisiasa | DW | 20.06.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Xi Jinping ziarani Korea Kaskazini

Viongozi wa China na Korea Kaskazini wamekuwa na mazungumzo katika mji mkuu wa Korea Kaskazini Pyongyang,huku ajenda kubwa inayotajwa ikiwa ni mazungumzo ya nyuklia yaliokwama na Marekani

Pasipo kutoa maelezo ya kina shirikia la habari la China Xinhua limesema Rais Xi Jinping na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un wamekutana kwa mazungumzo mjini Pyongyang.  Awali Xi na mkewe Peng Liyuan na maafisa waandamizi wa China walikaribishwa kwa mizinga 21, katika gwaride kubwa la heshima lililofanyika katika uwanja wa ndege wa Pyongyang.

Takribani watu 10,000 walijipanga vyema, huku wakipunga maua hewani na kuimba kwa sauti karibu Xi, karibu Xi. Kim na mkewe Ri Sol Ju, walikutana na ujumbe wa wapokeaji kwenye uwanja wa ndege huo. Xi yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili nchini Korea Kaskazini, ambapo inaelezwa kuwa ni ziara ya kwanza kwa kiongozi wa china kuwasili nchini humo katika kipindi cha miaka 14.

Migogoro ya Korea Kaskazini na China

Nordkorea Raketentest

Maroketi yanayoporomoshwa na Korea ya Kaskazini

Mkutano huo unafanyika wakati Xi na Kim wanakabiliwa na migogoro tofauti na Marekani. Xi wa kibiashara na Kim kuhusu silaha za nyuklia. Kwa mujibu wa Xinhua China inaweza kucheza karata ya kipekee na ya kujijenga kwa kuondosha hali ya kutoaminiana kati ya Korea Kaskazini na Marekani ili waweze kufanya kazi pamoja kufanikisha jitihada za kuondosha matumizi ya nyuklia.

Marekani inaitaka Korea Kaskazini kuachana na kuendeleza silaha za nyuklia kabla ya kuondoshewa vikwazo vya kimataifa ilivyowekewa taifa hilo. Lakini Korea Kaskazini imetaka muda wa hatua kwa hatua katika kulitekeleza hilo, huku ikihimiza kupata unafuu wa vikwazo vya kiuchumi ilivyowekewa. Katika suala hilo China inataka uwiano sawa wa kila upande na si kuwepo kwa shinikizo la upande mmoja na matakwa yasio akisi hali halisi.

Mwanadiplomasia wa zamani wa Korea Kaskazini Thae Yong Ho aliyetoroka mwaka 2016 anasema, anadhani Kim anataka kumpa ujumbe Xi wa kuuwakilisha kwa Rais Trump, pale ambapo viongozi hao wawili watakapokutana katika mkutano wa kilele wa mataifa ya nchi za G20 wa juma lijalo unaotarajiwa kufanyika nchini Japan.

Lakini pia alionya kuwa hatua ya namna hiyo inaweza kuwa ya kuvuta muda tu na sio kuachana na matumizi ya nyuklia.

Mazungumzo ya Marekani na Korea Kaskazini yamekwama tangu Kim na Trump wafanye mkutano wao wa kilele wa mara ya pili Februari mjini Hanoi, Vietnam.

Mwandishi: Sudi Mnette APE
Mhariri: Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com