1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa Nje wa Marekani Antony Blinken awasili Israel

Sudi Mnette
3 Novemba 2023

Vikosi vya Israel vimeripotiwa kuimarisha mzingiro dhidi ya mji wa Gaza, katika kipindi hiki ambacho pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwasili Israel kwa mara ya tatu.

https://p.dw.com/p/4YMZ0
Israel | US-Außenminister Antony Blinken in Tel Aviv
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken akiwasili IsraelPicha: Jonathan Ernst/AP/picture alliance

Ziara ya Blinken inalenga kile kinachotajwa kuwa kushinikiza usimamishaji wa mapigano kwa misingi ya kiutu na kutolewe nafasi ya misaada kuruhusiwa kuingia katika eneo hilo lililozingirwa la Gaza.

Kwa wakati huu kuna habari ya kuongezeka kwa mvutano katika maeneo ya mpaka wa kaskazini na Lebanon, ikiwa ni kabla ya hotuba iliyopangwa kutolewa baadaye Ijumaa hii na Hassan Nasrallah, kiongozi wa kundi la Hezbollah, mshirika wa Hamas. Ni hotuba yake ya kwanza kwa umma tangu Hamas iliposhambulia Israel mwezi uliopita, na kuzua hofu juu ya mzozo huo kuwa unaweza kuwa wa kikanda.

Dhima ya ziara ya Antony Blinken

Waziri Blinken kwa sasa anafanya safari yake ya tatu ya Israel tangu shambulizi la Hamas, ziara hii itamfikisha Tel Aviv na Amman, Jordan akiwa na lengo kubwa la kulitilia mkazo pendekezo la Rais Joe Biden la kusitishwa kwa operesheni za kivita, lengo likiwa kutoa msaada kwa Wapalestina na kufanikisha kuondoka zaidi nje ya eneo hilo kwa raia wa kigeni waliojeruhiwa.

Gazastreifen Nach dem Angriff Jabaliya
Majengo yaliovunjwa kwa mashambulizi ya Israel huko kaskazini mwa GazaPicha: Abed Khaled/AP Photo/picture alliance

Katika hatua nyingine Shirika la Afya Duniania WHO limetoa wito wa hakikisho la usalama kwa watoa misaada ya matibabu katika eneo la Gaza. Akiwa mjini Geneva Meneja Mkuu mwenye dhima ya kutoa huduma za dharura za matibabu, Mike Ryan amesema usafirishaji wa vifaa vya misaada ndani ya ardhi ya Palestina umekuwa ukizuliwa na pande zote hasimu. Zaidi anasema "Kuyavusha malori katika eneo la mpaka ni jambo moja, lakini kuyafikisha sehemu yanayohitajika ni jambo jingine. Na hilo halijawezeshwa, halijaungwa mkono. Imekuwa kinyume kabisa. Kwa hivyo kuna pengo kubwa kati ya baadhi ya yanayotamkwa na ukweli halisi kwa wahudumu wetu wa afya katika maeneo husika. Hilo linapaswa kubadilika."

Umoja wa Mataifa umesema Gaza inahitaji dola bilioni 1.2

Nayo ofisi ya Umoja wa Mataifa yenye kuhusika misaada ya kiutu inasema ili kukidhi mahitataji ya msingi kwa wakazi wa Gaza na Ukinga wa Magharibi kunahitajika kisa cha dola bilioni 1.2.

Inakadariwa watu 800, wakiwemo mamia ya Wapalestina wenye pasi za kusafiria za kigeni na majeruhi kadhaa wamepata ridhaa ya kuondoka Gaza kupitia kivuko cha Rafah. Hatua hiyo ilikuwa chini ya makubaliano ya mataifa ya Marekani, Misri, Israel na Qatar, yenye kufanya upatanishi na Hamas.

Kupitia kivuko hicho Israel imeruhusu zaidi ya malori 260 yanayobeba chakula na dawa, lakini watoa huduma ya msaada wanasema bado haitoshi. Mamlaka ya Israel imekataa kuruhusu mafuta kuingia. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya iliyo chini ya Hamas katika eneo hilo la Gaza ni kwamba idadi ya vifo vya Wapalestina katika vita vya Israel na Hamas imefikia 9,061.

Soma zaidi:Jeshi la Israel limetangaza kuuzingira kikamilifu Mji wa Gaza

Kimsingi pia rekodi zinaeleza zaidi ya watu 1,400 nchini Israel wameuawa, wengi wao vifo vyao vimetokana na shambulio la Oktoba 7 la Hamas na kadhalika mateka 242 wamewekwa kizuizini na kundi hilo.

Vyanzo: AP/DPA