1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wapalestina kuanza Ramadhan katika kivuli cha vita Gaza

Bruce Amani
10 Machi 2024

Wapalestina wanajiandaa kwa mfungo wa Ramadhan katika hali ya huzuni na hatua zilizoimarishwa za usalama na polisi ya Israel. Mazungumzo ya kupatikana muafaka wa kusitishwa mapigano yamekwama.

https://p.dw.com/p/4dMJK
Msikiti wa Al-Aqsa katika eneo la Mji Mkongwe wa Jerusalem
Eneo la Mlima wa Hekalu au Temple Mount, ni kitovu cha msuguano kati ya Israel na WapalestinaPicha: Saeed Qaq/APAimages/IMAGO

Maelfu ya polisi wamewekwa katika mitaa ya Mji Mkongwe wa Jerusalem, ambako maelfu ya waumini wanatarajiwa kila siku kufika katika eneo la Msikiti wa Al Aqsa, mojawapo ya maeneo takatifu zaidi katika dini ya kiislamu.

Eneo hilo, linalozingatiwa kuwa takatifu zaidi na Wayahudi wanaoliita Mlima wa Hekalu au Temple Mount katika Kiingereza, limekuwa kitovu cha msuguano kati ya Israel na Wapalestina.

Mashambulizi ya mfululizo ya Israel huko Gaza yamesababisha wasiwasi mkubwa kote duniani wakati hatari inayoongezeka ya njaa ikitishia kuongeza idadi ya vifo ambayo tayari imepindukia watu 31,000.

Ufuo wa Ukanda wa Gaza
Marekani itajenga gati ya muda kwenye ufuo wa Gaza kwa ajili ya meli za misaadaPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Mwezi wa Ramadhan utaanza Jumatatu au Jumanne wiki ijayo kwa kutegemea muandamo wa mwezi.

Lakini tofauti na miaka iliyopita, mapambo ya kawaida katika Mji Mkongwe hayajawekwa na hali ni kama hiyo ya huzuni katika miji ya eneo lote linalokaliwa la Ukingo wa Magharibi. Karibu Wapalestina 400 wameuawa katika makabiliano na vikosi vya usalama, au walowezi wa Kiyahudi tangu kuanza vita vya karibuni kati ya Israel na Hamas Oktoba 7.

Polisi imesema wanakikisha kuwa mfungo wa Ramadhan unaendelea salama na kuwa imefuchukua hatua za ziada za kuzuia kile ilichosema ni Habari za uchochezi na potofu kwenye mitandao ya kijamii na imewakamata watu 20 wanaoshukiwa kuchochea ugaidi.

Matumaini ya usitishwa mapigano

Matumaini ya kusitishwa mapigano, ambayo yangeruhusu mfungo wa Ramadhan kumalizika kwa amani na kuwezesha kuwachiwa kwa angalau baadhi ya mateka 134 wa Israel wanaoshikiliwa Gaza, yanaonekana kudidimia, baada ya mazungumzo ya mjini Cairo kukwama.

Katika magofu ya Gaza yenyewe, ambako nusu ya watu milioni 2.3 wamefurika katika mji wa kusini wa Rafah, wengi wanaishi katika mahema ya plastiki na wanakumbwa na uhaba mkubwa wa chakula, hisia ni za huzuni.

Meli ya hisani ya Uhispania iliyobeba msaada wa chakulailitarajiwa kuondoka taifa la kisiwa cha Bahari ya Mediterania la Cyprus kusaidia kupunguza mateso ya watu wa Gaza.

Mapacha vichanga wauwawa Gaza

Shirika lisilo la kiserikali la Open Arms limesema meli yake itapeleka tani 200 za chakula, ambazo mshirika wake, shirika la hisani la Marekani la World Central Kitchen kisha litazipakua kwenye fukwe za Gaza ambako lilijenga gati ya muda.

Wakati huo huo, Jeshi la Marekani limesema meli inayopeleka misaada ya kiutu katika Ukanda wa Gaza iko njiani baada ya Rais Joe Biden kuahidi kujenga gati ya muda kwa ajili ya kuingiza misaada kwenye eneo hilo lililozingirwa.

Kamandi Kuu ya kijeshi ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati, CENTCOM imesema meli hiyo imeondoka Langley-Eustis huko Virginia. Meli hiyo imebeba vifaa vya kwanza vya kujenga gati hiyo ya muda.

Marekanim Jordan na ndege nyingine zimekuwa zikidondosha msaada wa chakula huko Gaza, lakini mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaonya kuwa hiyo haitoshi kuyatosheleza mahitaji ya wakazi milioni 2.4.

Reuters, AFP