1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Matumaini ya kupata msaada kwa watu wa Gaza yapata nguvu

Saumu Mwasimba
8 Machi 2024

Umoja wa Ulaya wasema unasikitishwa na janga la kibinadamu linaloshuhudiwa Gaza. Mashirika kadhaa yameshindwa kuingiza msaada wa kibinadamu Gaza kupitia kivuko cha Rafah.

https://p.dw.com/p/4dJq3
Rais Nikos Christodoulides na rais wa Halmashauri kuu ya EU Ursula von der Leyen
Rasi wa Cyprus na mkuu wa Halmashauri ya Umoja wa UlayaPicha: Andreas Loucaides/PIO/AFP

Hali ya kibinadamu inazidi kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza huku jumuiya ya kimataifa ikiendelea na juhudi za kutaka kufikisha msaada kwa watu wa eneo hilo linalokabiliwa na vita. Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema njia ya kusafirisha msaada Gaza kutokea Cyprus kupitia baharini inatarajiwa kufunguliwa mwishoni mwa wiki hii.

Kwa hakika kauli zinazotolewa hivi sasa na viongozi barani Ulaya na Marekani zinafanana kuhusu namna wanaovyoitazama hali ya kibinadamu inayoendelea katika Ukanda wa Gaza.

Msaada wa kibinadamu ukidondoshwa Gaza
Msaada ukidondoshwa Gaza kutoka anganiPicha: Jordanian Armed Force Website/dpa/picture alliance

Wasiwasi wa Ulaya kuhusu Gaza

Rais wa Cyprus Nikos Christodoulides  na rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen wakifanya mkutano na waandishi wa habari wamesema kwa ujumla Ulaya ina wasiwasi na hali inayowakabili raia wa kawaida katika Ukanda wa Gaza na kwahivyo wanaamini wanawajibu wa kuchukuwa hatua ya kuwasaidia Wapalestina walioko kwenye eneo hilo la vita.

Von der Leyen amesema wako karibu kabisa kufunguwa njia ya kupelekwa misaada hiyo na wanatarajia hilo linaweza kufanyika Kesho Jumamosi au Jumapili.

"Licha ya changamoto zote, na hili linatia moyo sana, kwamba hivi sasa tunakaribia kabisa kufungua njia ya kupeleka msaada tunarajia Jumamosi au Jumapili na nina furaha sana kuona kwamba mpango mwa mwanzo wa majaribio  utaanzishwa leo. Na kwahivyo ni ushirikiano ulioanzisha juhudi hizo leo na shirika la kimataifa la msaada wa chakula la World Central Kitchen  ambao nataka kuwashukuru kwa dhati kwa kufanya kazi muhimu na  bila kuchoka."

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo hatua hiyo ya suhirikiano ya kusafirisha msaada kwa njia ya bahari kutoka Cyprus kwenda Gaza itajumuisha kujengwa kwa bandari ya muda  katika pwani ya Ukanda wa Gaza ambako meli zitaruhusiwa kutia nanga.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo mpango huo wa kupeleka msaada ni juhudi za pamoja kati ya Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya,Ujerumani,Ugiriki,Itali,Uholanzi, Cyprus,Umoja wa Falme za kiarabu,Uingereza na Marekani.

Soma pia:Mashirika ya misaada yatahadharisha juu ya kuzuka baa la njaa kaskazini mwa Gaza

Von der Leyen na rais wa Cyprus wote wamezungumzia juu ya kuwepo changamoto kubwa ya kupelekwa msaada ndani ya Gaza kupitia kivuko cha Rafah licha ya hali ya kibinadamu kuonesha kuwa mbaya katika Ukanda wa Gaza.

"Wakati wa mazungumzo yetu na rais wa halmashauri kuu tumezungumzia wasiwasi wetu wa pamoja kuhusiana na hali ya kibinadamu inayozidi kuwa mbaya Ukanda wa Gaza. Kinachojitokeza mbele ya macho yetu ni janga la kibinadamu. Ni suala la wazi kabisa kwamba kuna haja ya kuchukuliwa hatua ya dharura kupeka msaada kwa raia haraka iwezekanavyo.

Jeshi la Marekani kuongoza ujenzi wa bandari Gaza

Wanajeshi wa Israel wakiwa katika eneo la pwani ya Gaza walikoshambulia
Pwani ya Gaza katika bahari ya MediterraniaPicha: Jim Hollander/picture-alliance/dpa

Hata jana katika hotuba yake kwa taifa rais wa Marekani Joe Biden alizungumzia kuhusu hali ya kibinadamu inayojitokeza Gaza na kutangaza ushirikiano huo pamoja na Umoja wa Ulaya na mataifa ya Mashariki ya kati kupeleka msaada kwenye Ukanda huo wa vita akisema Jeshi la Marekani litaongoza ujumbe wa dharura wa kuweka bandari ya muda katika bahari ya Meditarania katika pwani ya Gaza.

Bandari hiyo  itakuwa na uwezo wa kupokea meli nyigi za chakula maji dawa na makaazi ya muda.

Rais Biden pia aliitaka Israel kuruhusu misaada zaidi iingie Gaza na kuhakikisha wafanyakazi wa mashirika ya kiutu hawashambuliwi.

Mpaka sasa zaidi ya Wapalestina 30,800 wameuwawa Gaza katika mapigano kwa mujibu wa mamlaka ya Gaza iliyoko chini ya kundi la Hamas. Kwa upande mwingine Israel inasema msaad zaidi hivi sasa unaingia Ukanda wa Gaza ikilinganishwa na kabla ya vita hivyo vilivyoanza Oktoba 7.