1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Gaza vyatishia mzozo mkubwa Mashariki ya Kati

Tatu Karema
4 Machi 2024

Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk, amesema vita vya Gaza kati ya Israel na kundi la wanamgambo la Hamas vimefikia hali tete inayoweza kuzua mzozo mkubwa kabisa katika Mashariki ya Kati

https://p.dw.com/p/4d9X2
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk akizungumza na waandishi habari mjini Cairo Misri mnamo Novemba 8, 2023 baada ya ziara katika mpaka wa Rafah ulioko kati ya Misri na ukanda wa Gaza
Mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Turk,Picha: KHALED DESOUKI/AFP

Akitoa taarifa yake kuhusu hali ulimwenguni kwa Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa, Turk amesema kuwa vita katika Ukanda wa Gaza tayari vimeenea katika nchi jirani, akielezea wasiwasi wake kwamba hali hiyo huenda ikachochea mzozo mkubwa zaidi utakaokuwa na athari kwa kila nchi katika Mashariki ya Kati na kwingineko.

Turk ahimiza kuchukuliwa kwa hatua za kuzuia mzozo zaidi

Akisisitiza juu ya umuhimu wa kuchukua hatua zote zinazowezekana ili kuzuia mzozo zaidi, mkuu huyo wa Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa amesema kuna mengi yanayoingiliana kwenye mzozo huo ambayo yanafanya muonekano wa kuenea kwa mgogoro kuwa halisi, akitaja mifano ya Yemen na Lebanon kama maeneo ambayo vita vya Gaza vina athari kubwa zaidi.

Soma pia:Mazungumzo ya usitishaji vita Gaza kuanza tena Cairo Jumapili

Turk ameongeza kuwa kuenea kwa operesheni za kijeshi Kusini mwa Lebanon kati ya Israel, Hezbollah na makundi mengine yenye silaha kunatia wasiwasi sana.

Wafanya kazi wa kigeni washambuliwa

Shambulizi la kombora limewalenga wafanyakazi wa kigeni waliokuwa wakifanya kazi kwenye shamba moja kaskazini mwa Israel na kumuua mtu mmoja na kuwajeruhi wengine saba.

Soma pia:Marekani yasisitiza wito wa kusimamisha mapigano Gaza

Haya ni kwa mujibu wa taarifa ya shirika la huduma za dharura la Magen David Adom.

Wapalestina wafanya ibada ya Ijumaa karibu na vifusi vya msikiti mmoja mjini Rafah, Kusini mwa Gaza baada ya shambulio la Israel mnamo Machi 1 2024
Wapalestina wafanya ibada ya Ijumaa karibu na vifusi vya msikiti mmoja mjini Rafah, Kusini mwa GazaPicha: Mohammed Salem/REUTERS

Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa waathiriwa wote walikuwa wanaume katika miaka ya thelathini bila ya kutaja uraia wao.

Kijana wa Kipalestina auawa

Kijana mmoja wa Kipalestina wa umri wa miaka 16 ameuawa na jeshi la Israel katika Ukingo wa Magharibi hii leo.

Soma pia:Dunia yalaani shambulizi la Israel dhidi ya Wapalestina Gaza

Hayo ni kwa mujibu wa wizara ya afya ya Palestina mjini Ramallah.

Wizara hiyo imesema kuwa kijana huyo alipigwa risasi kifuani na kwenye shingo.

Jeshi la israel limesema kuwa lilifanya operesheni hiyo ya masaa sita dhidi ya ugaidi katika kambi ya wakimbizi ya Amari karibu na Ramallah na kwamba ghasia mbaya zilizuka wakati wa operesheni hiyo.

Wanajeshi wa Israel wajibu mashambulizi ya mawe kwa risasi moto

Kulingana na jeshi la Israel, wanajeshi wake walishambuliwa kwa mawe na wakajibu kwa kutumia risasi moto.

Jeshi hilo limeendelea kusema kuwa vikosi vya usalama vya Israel pia viliwakamata washukiwa wawili waliokuwa wakisakwa wakati wa operesheni hiyo.

Watuhumiwa wengine walihojiwa na vijakaratasi vya uchochezi vilivyosambazwa na Hamas kuchukuliwa.