1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanasiasa watajwa katika kashifa ya "Paradise Papers"

Isaac Gamba
6 Novemba 2017

Uchunguzi wa kimataifa uliofanywa na waandishi wa habari za uchunguzi umewezesha kufichua zaidi ya nyaraka za siri milioni 13 zinazo onesha ukwepaji kodi katika kashifa iliyopewa jina Paradise Papers.

https://p.dw.com/p/2n594
USA Handelsminister Wilbur Ross
Picha: picture-alliance/dpa/A. Harnik

Kwa mujibu wa gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung lililofanikiwa kupata taarifa za nyaraka hizo zilizofichuliwa,  waandishi wa habari wapatao 400 kutoka nchi 67 waliokuwa wakifuatilia uchunguzi wa suala hilo wamefanikiwa kufichua nyaraka za siri  milioni 13.4 ambapo pia waliweza kufichua  mbinu zinazotumiwa na matajiri wakubwa pamoja na wanasiasa wa ngazi za juu katika kukwepa kodi. Nyaraka hizo zilizopewa jina la "Paradise Papers" zinaaanzia kipindi cha mwaka 1950 hadi mwaka 2016 zikihusisha barua pepe, mikataba ya kibiashara pamoja na taarifa za kibenki.

Majina ya wanasiasa zaidi ya 120 kutoka karibu mataifa 50 wakiwemo maafisa wa serikali ya rais wa Marekani  Donald Trump na makampuni ya Urusi  yametajwa katika nyaraka hizo.

Nyaraka hizo zinaonesha pia kuwa kwa kutumia makampuni yasiyofanya biashara, makampuni kama vile Nike, Apple, Uber na Facebook yanaweza kupunguza  viwango vyao vya kodi kuwa vya chini zaidi.

Kwa mujibu wa gazeti hilo la Süddeutsche Zeitung makampuni ya Rock star Bono pamoja na  kampuni binafsi ya Malkia Elizabeth wa pili wa Uingereza nayo pia yamehusishwa katika kashifa hiyo.  Gabriel Zucman ambaye ni mchumi amelieleza gazeti la Suddeutsche Zeitung kuwa wanasiasa pamoja na watu hao maarufu ulimwenguni wameficha kiasi cha dola trilioni 9.1 katika akaunti za nje.

 

Jina la Malkia Elizabeth latajwa katika kashifa ya Paridise

Deutschlandbesuch Königin Elisabeth II
Malkia Elizabeth wa IIPicha: Getty Images/M. Ukas

Kuhusina na suala linalomuhusu Malkia Elizabeth kumiliki makampuni binafsi nje ya nchi, wakosoaji wanaweza wakahoji iwapo ni sawa kwa kiongozi mkuu wa nchi kujihusisha kukwepa kodi kupitia makampuni aliyowekeza nje ya nchi.

Taarifa hizo zilizofichuliwa zimechapishwa  pia na mashirika kadhaa ya habari kwa kushirikiana na taasisi ya waandishi wa habari inayohusika na habari za uchunguzi yenye makao yake nchini Marekani (ICJ).

Taarifa hizo pia zimemuanika waziri wa masuala ya biashara wa Marekani Wilbur Ross,  anayedaiwa kushirikiana na  washirika wa karibu wa rais wa Urusi Vladimir Putin akiwemo mkwe wa kiume wa rais huyo. 

Katika ripoti yake gazeti la Suddeutsche Zeitung limeandika kuwa " Bilionea Wilbur Ross anatengeneza pesa  kutokana na biashara anayofanya na Urusi na kuongeza kuwa  licha ya kuwa katika baraza la mawaziri la rais Donald Trump hilo tu halimfanyi ajiondoe katika kashifa hiyo.

 

Ross anaripotiwa kuwa mmoja wa wanaomiliki kampuni ya usafirishaji mizigo kwa njia ya bahari ijulikanayo kama Navigator ambayo imetumia zaidi ya dola milioni 68 ikilihusisha shirika la masuala ya nishati nchini Urusi tangu mwaka 2014. Aidha gazeti la New York Times limeripoti kuwa sehemu ya utajiri alionao Ross inatokana na mbinu anazotumia kukwepa kodi katika masuala yake ya kibiashara.

 

 Ukimuacha Ross,  washauri kadhaa wa rais Donald Trump, mawaziri na wafadhili wakati wa kampeni yake nao pia majina yao yanaonekana katika nyaraka hizo za Paradise zilizofichuliwa na waandishi wa habari za uchunguzi.

Washington, US-Präsident Donald Trump spricht während einer Kabinettssitzung im Weißen Haus
Rais Donald Trump wa MarekaniPicha: Reuters/K.Lamarque

 

Kashifa hii pia imekumbusha ujumbe ulioandikwa katika ukurasa  wa twitter na rais Donald Trump Juni 18,2013 wakati aipoandika  kuwa shindano la urembo la "Miss Universe" litatangazwa moja kwa moja kutoka mjini Moscow Novemba 9 na kusema ni biashara kubwa itakayozileta nchi hizo mbili pamoja na kuhoji iwapo rais Vladimir Putin angekwenda katika shindano hilo basi angekuwa rafiki yake? Oktoba 17,2013 Trump alikieleza kipindi flani cha charti za muziki kuwa amefanya biashara ya kutosha na warusi.

Taarifa zinazohusiana na nyaraka hizo za Paradise Papers zinaonesha kuwa Kansella wazamani wa Ujerumani Gehard Schrouder alikuwa akiliongoza kampuni moja nje ya nchi.  Mwaka 2009 alikuwa sehemu ya bodi huru ya ushauri ya kampuni yenye ubia kati ya Uingereza na Marekani ijulikanayo kama TNK-BP huku fedha za urusi zikiendelea kuingia nchini Ujerumani licha ya vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Urusi.

 

Gazeti la  Suddeutsche Zeitung nalo pia limewahi kuandika taarifa  za kashifa nyingine inayofanana na hiyo ijulikanayo kama Panama Papers.

 

 

Mwandishi: Isaac Gamba/dw/afpe

 

Mhariri  : Iddi Ssessanga