Wanaanga wa Artemis II wanarejea duniani kutoka mwezini
8 Aprili 2026
Katika safari hiyo ya kihistoria, wamezunguka Mwezi na kukusanya picha pamoja na taarifa muhimu zinazosaidia kuelewa zaidi anga. Mafanikio haya yamevuta hisia za watu duniani kote, yakionyesha hatua kubwa ya sayansi na teknolojia ya anga.
Wanaanga hao Reid Wiseman, Christina Koch, Victor Glover na Jeremy Hansen kutoka shirika la anga la Marekani, NASA, walifanikiwa kuuzunguka Mwezi na kushuhudia mambo ambayo kwa kawaida hayaonekani kirahisi na binadamu. Miongoni mwa picha walizopiga ni ile ya Dunia ikizama nyuma ya Mwezi, tukio linaloitwa "Earthset”.
Picha hii imefananishwa na ile maarufu ya "Earthrise” ya mwaka 1968, lakini safari hii inaonesha maendeleo ya teknolojia ya kisasa. Jared Isaacman, ni msimamizi wa shirika la anga la Marekani, NASA, na anasema. "Hii ni mara ya kwanza kwa binadamu kurekodi baadhi ya maeneo ya upande wa mbali wa Mwezi. Picha hizi zitapatikana kwa umma kupitia tovuti ya NASA, majukwaa yetu ya kidijitali, na pia Ikulu ya White House tayari imetoa picha maarufu ya "Earthset” mapema leo." Mbali na hilo, wanaanga walielezea kwa kina walichokiona kwenye uso wa Mwezi, ikiwemo mashimo makubwa, nyufa za ardhi na mwanga wa ghafla uliosababishwa na vimondo kugonga uso wa Mwezi. Pia walishuhudia tukio la kupatwa kwa jua wakiwa angani, jambo ambalo ni nadra na la kuvutia sana kwa utafiti wa kisayansi.
Taarifa hizi zinatarajiwa kuwasaidia wanasayansi kupanga safari zijazo, ikiwemo lengo la kumpeleka binadamu kutua Mwezini katika miaka ijayo.
Safari hii pia imeweka rekodi mpya kwa kufika umbali mkubwa zaidi kutoka duniani kuliko safari nyingine yoyote ya binadamu hapo awali. Kwa sasa, chombo hicho kinaendelea na safari ya kurejea duniani kwa kutumia njia maalum inayokirudisha moja kwa moja bila kutumia mafuta mengi. Kinatarajiwa kutua baharini karibu na pwani ya California, ambapo timu za uokoaji tayari zimejiandaa kuwapokea wanaanga hao.
Msimamizi mwenza wa NASA, Amit Kshatriya, amesema furaha na mshangao mkubwa vinaonekana kwa watu wengi kutokana na mafanikio ya safari hii ya Artemis II, na kwamba mafanikio hayo yanawachochea vijana kuwa wanasayansi, wahandisi na wabunifu wa kesho. Ameongeza kuwa: "Kitu kimoja cha kushangaza kuhusu safari za anga za binadamu ni kwamba zinamfanya mtu aione dunia kwa mtazamo tofauti kabisa—kama dunia isiyo na mipaka, ambapo watu wote tuna historia moja na tunashiriki mustakabali mmoja. Kila anayepata nafasi ya kuona hali hiyo hubadilika moyo na mawazo yake. Wanaanga kutoka mataifa yote—iwe ni Warusi, Wamarekani au Wakanada—wanarudi na mtazamo huo huo wa umoja wa dunia."
Glover alikuwa mtu wa kwanza mwenye asili ya rangi nyingine kuzunguka Mwezi, Koch alikuwa mwanamke wa kwanza, na Mkanada Hansen alikuwa mtu wa kwanza asiye Mmarekani. Safari ya Artemis II imefungua ukurasa mpya katika utafiti wa anga na imeonyesha wazi kuwa bado kuna mengi ya kujifunza kuhusu Mwezi na ulimwengu kwa ujumla.
AP, AFP