1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wamarekani wasubiri kwa hamu kujua mshindi wa urais

5 Novemba 2020

Matokeo ya urais nchini Marekani yangali yanasubiriwa. Kwenye majimbo yaliyokuwa yakisubiriwa, mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden ameshinda katika jimbo la Michigan.

https://p.dw.com/p/3ku0o
Kombobild | US-Wahlen 2020 - Donald Trump und Joe Biden
Picha: Rourke/Semansky/AP/dpa/picture alliance

Mshindi anahitajika kupata kura 270. Pande zote mbili Democratic na Republican zinajiandaa kwa uwezekano wa kuanza mapambano ya kisheria. 

Kura zinaendelea kuhesabiwa na zoezi hilo huenda likachukuwa muda kutokana na kiwango cha watu waliopiga kura ya mapema ambacho hakijawahi kushuhudiwa.

Kuna majimbo matano ambayo mpaka sasa matokeo hayajatangazwa ambako mamilioni ya kura hazizahesabiwa. Rais aliyeko madarakani Donald Trump jana usiku alituma kwenye ukurasa wake wa Twitter taarifa iliyoandikwa na tovuti ya habari ya Breitbart ambayo iliandamana na vidio inayoonesha maafisa wa uchaguzi katika mji wa Detroit ulioko kwenye jimbo la Michigan wakiyafunika madirisha wakati watu waliokuwa nje wakijaribu kuchungulia kutazama kura zinavyohesabiwa.

Nini kitatokea kama matokeo ya uchaguzi wa Marekani yatapingwa?

Polisi waliwasukuma watu waliojazana walioanza kugonga milango na madirisha na kupiga kelele wakidai maafisa wa uchaguzi wasimamishe zoezi la kuhesabu kura.

Lakini taarifa hiyo ya tovuti ya Breitbert hakieleza kwamba maafisa wa uchaguzi walisea watu hawaruhisiwi kuingia kwenye chumba cha kuhesabu kura kutokana na wasiwasi wa kiusalama kufuatia kiwango cha watu.

Kila chama kiliruhusiwa kuwa na waangalizi wake 134 wakufuatilia na kuhoji katika mchakato huo wa kuhesabu kura.

Rais Trump ametishia kuwasilisha kesi katika mahakama ya juu ili kusitisha hesabu ya kura
Rais Trump ametishia kuwasilisha kesi katika mahakama ya juu ili kusitisha hesabu ya kuraPicha: Chip Somodevilla/Getty Images

Vyombo vya habari na wanasheria pia walikuwepo ndani ya chumba cha kuhesabu kura. Kufikia saa 5.56 jioni shirika la habari la The Associated Press lilitangaza kwamba ushindi wa Jimbo la Michigan umenyakuliwa na Joe Biden.

Matokeo ya mwisho kwa sasa yanayosubiriwa kutangazwa ni katika majimbo ya Georgia, Nevada, North Carolina na Pennsylvania huku pia wachambuzi wakifuatilia kwa karibu ujumuishaji wa mwisho wa matokeo katika jimbo la Arizona.

Ushindi wanukia kwa Biden

Mgombea wa Democrat Joe Biden anaongoza hadi sasa katika kura za wajumbe akishikilia kura 264 na Donald Trump akiwa na 214 kwa mujibu wa matokeo ya awali ya makadirio ya shirika la habari la Associated Press. Kwa maneno mengine Biden anachohitaji ni kupata ushindi kwenye jimbo moja tu zaidi abishe hodi kwenye milango ya ikulu ya White House.

Kwa rais aliyeko madarakani Donald Trump mambo hayajamkalia vizuri mpaka sasa na wafuasi wake chungunzima walikusanyika kwenye vituo vya kuhesabu maeneo mbali mbali ikiwemo Detroit na Phoenix wakati matokeo yalipoonesha kumpa ushindi Joe Biden kwenye majimbo mawili muhimu.

Kwa upande mwingine ya maelfu ya waandamanaji wanaompinga Trump wajitokeza katika miji mbali mbali ya Marekani kutaka majumuisho ya kura zote yafanyike katika uchaguzi huo ambao hadi sasa mshindi hajapatikana

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW