1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nini kitatokea kama matokeo ya uchaguzi Marekani yatapingwa?

Josephat Charo
4 Novemba 2020

Wamarekani wanaendelea kusubiri matokeo ya jumla ya uchaguzi wakati Rais Donald Trump akichuana vikali na mpinzani wake Joe Biden. Je ni kitu gani kinachoweza kutokea iwapo kutatokea mvutano mkubwa kuhusu matokeo? 

https://p.dw.com/p/3krnp
US Wahl 2020 Deutschland Protest Berlin
Picha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Data za awali zinaonyesha wafuasi wa chama cha Democratic wanapiga kura kwa njia ya barua kwa idadi kubwa kuliko wale wa chama cha Republican. Katika majimbo kama Pennsylvania na Wisconsin ambayo hayahesabu kura za aina hiyo mpaka siku yenyewe ya uchaguzi, matokeo ya awali yalionekana kumpendelea Donald Trump kwa sababu hawakuhesabu kwa haraka kura zilizopigwa kwa njia ya posta. Wafuasi wa chama cha Democratic walielezea wasiwasi kwamba Trump angejitangaza mshindi kabla kura kukamilika kuhesabiwa kama alivyofanya leo.

US Wahl 2020 | Wahlen in Kalifornien
Kinyang'anyiro ni kikali mno kati ya Biden na TrumpPicha: Mike Blake/REUTERS

Matokeo yatakayoonesha wagombea wameachana kwa kura chache yanaweza kusababisha kufunguliwa kesi mahakamani kuhusu upigaji kura na utaratibu mzima wa kuhesabu kura katika majimbo yenye ushindani mkubwa. Kesi zitakazowasilishwa katika majimbo mbalimbali huenda hatimaye zikafika katika mahakama ya juu kabisa ya Marekani, kama ilivyotokea mwaka 2000 katika uchaguzi wa jimbo la Florida, wakati mgombea wa chama cha Republican, George W. Bush alipompiku mgombea wa chama cha Democratic, Al Gore, kwa kura 537 tu jimboni Florida baada ya mahakama kuu kusitisha shughuli ya kuhesabu upya kura.

Trump alimteua Amy Coney Barrett kuwa jaji wa mahakama ya juu kabisa ya Marekani siku chache kabla uchaguzi, na hivyo kuifanya mahakama hiyo kuwa na idadi kubwa ya mahafidhina sita kwa tatu, hali ambayo inaweza kumpendelea yeye kama rais iwapo mahakama zitakuwa na jukumu la kuamua mvutano kuhusu matokeo ya uchaguzi yanayozozaniwa.

US Wahl 2020 | Wahllokal in Wisconsin
Marekani ilishuhudiwa kinachotajwa kuwa idadi kubwa kabisa ya wapigakura tangu 1908Picha: Joel Lerner/Xinhua News Agency/picture-alliance

Jopo maalumu la wapiga kura wa majimbo

Rais wa Marekani hachaguliwi kwa kura nyingi za wananchi. Kwa mujibu wa sheria mgombea anayeshinda idadi kubwa ya kura kati ya kura 538 za jopo maalumu la wapiga kura wa majimbo, anakuwa rais mpya wa Marekani. Mwaka 2016, Trump alishindwa na Hillary Clinton, mgombea wa chama cha Democratic, lakini akapata kura 304 za jopo hilo la wapiga kura wa majimbo, huku Clinton akipata 227.

Mgombea anayeshinda idadi kubwa ya kura za Wamarekani katika kila jimbo, kimsingi anapata kura za jopo la wapiga kura wa jimbo hilo. Mwaka huu, wapiga kura hao wa jopo maalumu watakutana Desemba 14 kupiga kura. Baraza la wawakilishi na baraza la seneti watakutana Januari 6 kuzihesabu kura hizo na watamtangaza mshindi.

Bildergalerie US Wahl 2020 | Interesse weitweit | Taipeh, Taiwan
Wananchi wanasubiri kwa hamu kumjua mshindiPicha: Ann Wang/REUTERS

Kwa kawaida magavana huhakiki na kuidhinisha matokeo katika majimbo yao na kuwasilisha taarifa kwa bunge la Marekani, Congress. Lakini baadhi ya wasomi wameainisha mazingira ambapo gavana na bunge katika jimbo lililozozaniwa wanawasilisha matokeo tofauti. Majimbo yenye mchuano mkali ya Pennsylvania, Michigan, Wisconsin na North Carolina yote yana magavana kutoka chama ha Democratic na mabunge yanayodhibitiwa na chama cha Republican.

Kwa mujibu wa wataalamu wa sheria, haijabainika wazi ikiwa katika hai hii bunge linatakiwa kuyakubali matokeo yaliyohakikiwa na gavana wa jimbo au kutohesabu kabisa kura za jopo maalumu la wapiga kura wa majimbo. Kwa mujibu wa sheria, baraza la wawakilishi na bara za seneti yatatakiwa kuamua, kila baraza kivyake, matokeo yapi kuyakubali. Kwa sasa baraza la seneti linadhibitiwa na chama cha Republican na baraza la wawakilishi linadhibitiwa na chama cha Democratic, lakini kura za jopo la wapiga kura wa majimbo, zitahesabiwa na bunge jipya, litakaloapishwa Januari 3 mwakani. Iwapo mabaraza yote mawili hayatakubaliana, haijulikani bayana kitakachotokea.

US Wahl 2020 Deutschland Protest Berlin
Kura nyingi zilipigwa pia kwa njia ya postaPicha: Fabrizio Bensch/REUTERS

Uchaguzi maalumu

Iwapo itabainika kwamba hakuna mgombea aliyepata kura nyingi za jopo la wapiga kura wa majimbo, kutafanyika uchaguzi maalumu kwa mujibu wa mageuzi ya sheria ya Marekani. Hii ina maana baraza la wawakilishi litamchagua rais mpya na baraza la seneti litamchagua makamu wa rais.

Kila ujumbe wa jimbo utapata kura moja. Kwa sasa chama cha Republican kina wajumbe 26 kati ya 50 wa majimbo, huku chama cha Democratic kikiwa na wajumbe 22; kura moja imegawanyika na nyingine ina wajumbe 7 wa Democratic, 6 wa Republican na moja ya chama cha Libertarian.

Uchaguzi maalumu unaweza kufanyika pia ikiwa wagombea wote wawili watapata kura sawa za wajumbe wa majimbo kwa maana 269 kwa 269 baada ya uchaguzi. Kuna dalili zinazoashiria kwamba Marekani inaelekea katika mkwamo huo mwaka huu 2020.

Reuters