1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vita vya Urusi, Ukraine vyatawala sherehe za Carnival

Saumu Mwasimba
16 Februari 2023

Mvutano wa Kansela Scholz na waziri wa kigeni Annalena Baerbock kuhusu hatua za kuchukua kuelekea Ukraine wagubika jukwaa la tamasha la Carnival

https://p.dw.com/p/4NZsO
BG Ukraine Krieg Flucht Zivilisten Reaktionen
Picha: LISI NIESNER/REUTERS

Hapa Ujerumani katika eneo zima linalopakana na mto Rhine linafanyika tamasha kubwa la kila mwaka la Karnival, ambalo pamoja na kusheheni viroja, na mavazi ya vituko, ni jukwaa pia linalotumika kutoa ujumbe kuhusu masuala ya kisiasa yanayoikabili nchi na ulimwengu kwa ujumla wake.

Tamasha la mwaka huu, limeangazia  ujumbe kuhusu vita vya Urusi nchini Ukraine na namna Ujerumani inavyoshughulikia suala hilo.

BG Köln Rosenmontag - Friedensdemonstration für Ukraine
Picha: AFP via Getty Images

Sherehe hizi zinajumuisha tafrija mbali mbali bendi za muziki, kula na kunywa, mavazi ya vituko, magwaride ya kila aina yanayofanywa na makundi mbali mbali ya watoto na watu wazima.

Na kawaida katika msimu wa sherehe hizo maarufu kabisa Ujerumani masuala mbali mbali huangaziwa na mwaka huu suala linalochukuwa nafasi kubwa ni vita vya Ukraine na hatua zinazochukuliwa na Ujerumani kuelekea mgogoro huo.

Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amekiri kwamba katika sherehe hizo alifikiria kujitokeza akiwa na vazi la duma,lakini akasema alihofia kwamba kansela Olaf Scholz atamnyima ruhusa ya kusafiri kwa wiki kadhaa.

Kauli yake hiyo ni fumbo la Carnival lililotafsiriwa moja kwa moja kwamba ililenga hasa kuonesha namna ambavyo Kansela Scholz anachelewesha kuidhinisha kutuma vifaru vya kivita chapa Leopard kuelekea nchini Ukraine.

Deutschland Ukraine Krieg l Rosenmontag - Friedensdemonstration in Köln
Picha: Ina Fassbender/AFP

Msimu wa sherehe za Karnival ni muda wa vichekesho na burudani  nchini Ujerumani huku wakikusanyika maelfu ya watu kwenye sherehe hizo katika miji mbali mbali wakiwa na mavazi ya kuchekesha ya vituko na kujiiunga kwenye magwaride lakini kwa upande mwingine wanasiasa huangaziwa kwa kiasi kikubwa na hotuba zao mara nyingi zinazowa ishara ya mambo yalivyo nchini.

Na kwahivyo haishangazi kwamba watangazaji wamechukuwa fursa hii kuiangazia kauli hiyo ya Baerbock kama mfano unaoonesha kuwepo mpasuko mkubwa kati ya waziri huyo wa mambo ya nje  na Kansela,wakionya kwamba ni mvutano unaoiumiza Ujerumani katika jukwaa la ulimwengu.

Na hata gazeti maarufu hapa Ujerumani liliwahi pia kuandika mwanzoni kabisa mwa mwezi huu kwamba uhusiano mbaya kati ya viongozi hao wawili  unaikwamisha serikali ya muungano pamoja na sera ya nje ya Ujerumani

Carnival Opening In DÃ_sseldorf
Picha: Ying Tang/NurPhoto/picture alliance

Gazeti hilo lilibaini kwamba wakati migogoro na vita vikijitokeza kila mahala Kansema na waziri wake wa mambo ya nje mpaka sasa wameshindwa kukubaliana kuhusu miongozo juu ya sera yao ya mambo ya nje.

Mbali na mgogoro wa Ukraine suala jingine la mvutano kati ya Kansela na waziri wa mambo ya nje ni uhusiano wa Ujerumani na China.Waziri Baerbock anaunga mkono msimamo mkali dhidi ya China na amekosoa ziara ya Kansela Scholz aliyoifanya Beijing mnamo mwezi Novemba.

Wakati viongozi wa dunia wakielekea kwenye mkutano wa usalama wa Munich wiki hii baadhi wanawasiwasi kwamba ikiwa serikali mjini Berlin inagubikwa na mivutano ,hapana shaka itazuia uwezo  wake wa kuchukuwa dhima kubwa katika masuala ya kidunia.

BdTD | Deutschland Köln | Das Kölner Dreigestirn tauft ICE Rheinland
Picha: Christoph Hardt/Panama Pictures/IMAGO

Na katika sherehe za Karnival yote hayo yanawashughulisha waandaaji wanaofuatilia matukio ndani na nje ya Ujerumani,na wanasema wanawajibu wa kuwa kioo cha jamii.Kilele cha sherehe hizo ni Jumatatu inayotambuliwa kama Jumatatu ya mawardi.