1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa ya Ulaya kujadili kuhusu kuijenga upya Ukraine

25 Oktoba 2022

Viongozi wa Mataifa ya Ulaya wanakutana mjini Berlin nchini Ujerumani ili kujadili mpango kabambe wa kuijenga upya Ukraine.

https://p.dw.com/p/4Ifdp
EU-Gipfel in Prag 7.10.2022
Picha: Petr David Josek/dpa/AP/picture alliance

Viongozi wa Mataifa ya Magharibi wanakutana mjini Berlin nchini Ujerumani ili kujadili kuhusu mpango kabambe wa kuijenga upya Ukraine.

Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz amesema leo kuwa lengo la mkutano huo ni kujadili namna ya kuhakikisha muendelezo wa ufadhili na ujenzi wa Ukraine kwa miaka na miongo kadhaa ijayo.

Deutschland | Ukraine-Konferenz in Berlin | Mateusz Morawiecki
Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki akihutubia katika Mkutano huoPicha: Anna Widzyk/DW

Waziri Mkuu wa Poland Mateusz Morawiecki amesema Urusi inapaswa kulipa fidia kwa vita vyake nchini Ukraine na kubaini kuwa ikiwa Ulaya haita vishinda vita hivyo, si tu itaipotoza Ukraine bali pia itajishushia hadhi.

" Ulaya ina nguvu zaidi kuliko Urusi. Lakini kuona haijaweza kumzuia Putin hii inathibitisha kwa kiasi fulani, tulikuwa kama chui wa kuchorwa. Inabidi tuimarishe sera zetu ili kupambana na matatizo ambayo tunakabiliwa kwayo."

Soma zaidi:UN yataka ukanda salama kwenye kinu cha Zaporizhzhia 

Waziri mkuu wa Ukraine Denys Shmyhal amesema katika Mkutano huo wa mjini Berlin kuwa nchi yake imepokea vyema misaada ya silaha na mafunzo ya askari wake, lakini bado inahitaji silaha zaidi na risasi ili kuvishinda vita dhidi ya Urusi.

Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula Von der Leyen amesema Benki ya Dunia inakadiria hadi sasa gharama ya uharibifu nchini Ukraine kufikia dola bilioni 345. Pamoja na msaada wa muda mrefu, Von der Leyen amesema Ukraine inahitaji ukarabati wa haraka.

Onyo la Urusi kwa matumizi ya "bomu chafu"

Der russische Pressesprecher Dmitry Peskov
Msemaji wa Ikulu ya Urusi-Kremlin, Dmitry PeskovPicha: Elena Palm/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Msemaji wa ofisi ya rais wa Urusi,Kremlin Dmitry Peskov amesema kitendo cha mataifa ya Magharibi kupinga Onyo la Urusi hakikubaliki kwa kuzingatia uzito wa hatari waliyoitaja, ambayo amesema inatokana na mipango ya watu wa Ukraine.

Waziri wa Ulinzi wa Urusi Sergei Shoigu aliwaambia Jumapili hii mawaziri wenzake wa Uingereza, Ufaransa, Uturuki na Marekani kwamba vikosi vya Ukraine vilikuwa vikiandaa "uchokozi'' aliodai unahusisha silaha zenye mionzi na zijulikanazo kama bomu chafu. Uingereza, Ufaransa, na Marekani zilipinga madai hayo na kuyataja kuwa "uongo mtupu.''

Bomu chafu hutumia vilipuzi kutawanya taka zenye mionzi katika jitihada za kuzusha hofu. Silaha kama hizo hazisababishi uharibifu kama wa mlipuko wa nyuklia, lakini zinaweza kuyaweka maeneo mapana zaidi katika hali mbaya ya uchafuzi wa mionzi.

Soma zaidi: IAEA kuchunguza maeneo ya nyuklia Ukraine

Kampuni ya nishati ya nyuklia ya Ukraine imesema wakati Moscow ikiishutumu Kiev kwa kujiandaa kulipua bomu chafu, kinyume chake kinaweza pia kuwa kweli. Kampuni ya Energoatom imefahamisha leo kwamba jeshi la Urusi liliendesha shughuli za siri na zisizoruhusiwa katika kiwanda cha nyuklia cha Zaporizhzhia, ambazo zinaweza kusababisha tukio la nyuklia.