1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi wa G7 waionya China dhidi ya kujitanua kijeshi

20 Mei 2023

Viongozi wa kundi la mataifa tajiri la G7 wameionya China dhidi ya kutanua shughuli zake za kijeshi kwenye kanda ya Asia na Pasifiki lakini wamesisitiza pia dhamira ya kuwa na mahusiano imara na utawala wa Beijing.

https://p.dw.com/p/4RbVg
G7 Gipfel in Japan, Hiroshima
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Kwenye tamko la mwisho lililotolewa baada ya mkutano wa kilele wa kundi la G7 uliofanyika kwenye mji wa Hiroshima nchini Japan, viongozi wa mataifa hayo wameorodhesha masuala kadhaa yanayowatia wasiwasi kutokana na shughuli za kijeshi na kiuchumi za China.

Soma zaidi:Viongozi wa G7 kujadili "mabavu ya kiuchumi" ya China

Wametahadharisha dhidi ya kujitanua kijeshi kwa China kwenye eneo la bahari ya kusini na kurejea msimamo wao kwamba "amani na uthabiti" kwenye ujia wa bahari wa Taiwan ni suala muhimu kwa usalama wa dunia.

Hata hivyo wamesema wako tayari kushirikiana na Beijing na kwamba misimamo wanayochukua hailengi kuidhuru China wala kulemaza maendeleo ya kiuchumi ya dola hiyo ya mashariki ya mbali.

Tamko la pamoja la kundi hilo la G7 limeitaka pia China iishinikize Urusi kuacha uchokozi wa kijeshi na iviondoe vikosi vyake Ukraine mara moja. Kupitia tamko hilo viongozi wa G7 wameihimiza China iunge mkono  amani ya kudumu na haki kwa kuzingatia uadilifu wa kieneo, kanuni na makusudi ya mkataba wa Umoja wa Mataifa, ikiwemo mazungumzo ya moja kwa moja na Ukraine.  

Wakitoa wito wa kufanya kazi pamoja katika changamoto zinazoikabili dunia kama vile mabadiliko ya tabia nchi, madeni mahitaji ya ufadhili wa kifedha kwa mataifa masikini, masuala ya afya yanayohusu dunia na uthabiti wa kiuchumi, viongozi wa kundi hilo la mataifa saba tajiri duniani wamesema, ushirikiano na China unahitajika kutokana na nafasi ya taifa hilo duniani na kiuchumi.

Biashara isitumike kama silaha

Viongozi hao wametahadharisha pia nchi zinazojaribu kutumia biashara kama silaha na kusema kuwa zitakabiliwa na matokei kauli ambayo imeipa China ishara kuhusu mienendo ambayo Marekani inasema ni uonevu wa kiuchumi 

Viongozi wa G7, mashirika ya kimataifa  na washirika katika picha ya pamoja
Viongozi wa G7, mashirika ya kimataifa na washirika katika picha ya pamojaPicha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

G7 kwa kauli moja limeonesha wasiwasi kuhusu hali ya haki za binadamu nchini China hasa katika majimbo ya Tibet, Hong Kong na Xijiang ambako watu wengi wanakabiliwa na tatizo la kushurutishwa kufanya kazi 

Kundi la G7 linaundwa na mataifa ya Japan,Marekani, Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Canada, na Italia bila kuusahau Umoja wa Ulaya.

Wakati huohuo, Rais wa Ukraine Volodymyr amepeleka wito wake wa kutaka kuungwa mkono dhidi ya Urusi kwenye mkutano wa G7 unaofanyika Hiroshima, Japan. 

Amefika Hiroshima ikiwa ni muda mfupi baada ya Ikulu ya marekani kutangaza uamuzi iliyouita wa kihistoria wa kuipatia Ukraine ndege za kivita chapa F 16. Wakati alipowasili mapema leo mjini Hiroshima Zelensky alisema kuwa mkutano wa G7 ungeongeza ushirikiano utakaoipa ushindi Ukraine.