Viongozi mbalimbali waomboleza kifo cha Winnie Mandela | Matukio ya Kisiasa | DW | 03.04.2018
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Viongozi mbalimbali waomboleza kifo cha Winnie Mandela

Viongozi mbalimbali duniani wameendelea kutoa salamu zao za rambirambi kufuatia kifo cha Winnie Madikizela-Mandela, aliyekuwa mke wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson Mandela.

Winnie amefariki dunia jana akiwa na umri wa miaka 81, baada ya kuugua kwa muda mrefu. Msemaji wa familia yake, Victor Dlamini amesema Winnie alifariki akiwa amezungukwa na familia yake. Dlamini amesema mama huyo wa taifa la Afrika Kusini amekuwa akilazwa hospitali mara kwa mara tangu kuanza kwa mwaka huu.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema amesikitishwa na kifo cha Winnie na amemuelezea kama mwanamke shupavu na imara katika harakati za ukombozi wa Afrika Kusini.

Akizungumza baada ya kuizuru nyumba ya Winnie mjini Soweto, Ramaphosa amesema mwanamama huyo ameacha urithi mkubwa na aliyagusa maisha ya mamilioni ya Waafrika Kusini katika kipindi cha giza cha utawala wa kibaguzi wakati chama cha ANC kilipopigwa marufuku.

Südafrika - neuer Präsident Cyril Ramaphosa

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa

''Aliendelea kuonyesha ujasiri dhidi ya mifumo yote ya kutisha. Ni mtu ambaye amepitia mateso na misukosuko mingi na kifo chake ni pigo kubwa. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kuwaunganisha Waafrika Kusini wengi wa rangi na itikadi tofauti za kisiasa,'' alisema Ramaphosa.Ameongeza kusema kuwa Winnie ni shujaa wa haki na usawa na sauti kwa wasio na sauti.

Askofu Mkuu mstaafu wa Afrika Kusini Desmond Tutu, amesema Winnie ni jasiri katika historia ya vizazi vya wanaharakati ambaye alikataa kuwasujudia waliomfunga mumewe.

Umoja wa Afrika waomboleza

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat amesema umoja huo unaungana na bara lote la Afrika kuomboleza kifo cha Winnie ambaye siku zote atakumbukwa kama mwanaharakati asiye na woga na aliyejitoa maisha yake kwa ajili ya kupigania uhuru wa Afrika Kusini na wanawake wote kwa ujumla.

Aidha, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres ameelezea kusikitishwa na kifo hicho akisema kuwa mama huyo alikuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini. Guterres amesema Winnie alizungumza bila kuwa na hofu katika kutetea haki sawa.

Kwa upande wake, Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari amesema Winnie atabakia kuwa tunu sio tu ya mwanamke wa Kiafrika, bali Waafrika wote kwa ujumla.

Naye kiongozi wa upinzani nchini Kenya, Raila Odinga, amesema Winnie aliongoza mapambano dhidi ya utawala wa kikatili wa ubaguzi wa rangi na aliwahamasisha wanawake ulimwenguni kote kuingia katika maeneo ya mapambano kudai haki na uhuru.

Watu mashuhuri waliotoa salamu za pole ni pamoja na mwanaharakati wa haki za kiraia, Jesse Jackson, mwigazaji maarufu Idris Elba na mwanamitindo wa kimataifa Naomi Campbell.

Nelson und Winnie Mandela

Nelson na Winnie Mandela wakati walipofunga ndoa 1957

Ramaphosa amesema ibada rasmi ya kumbukumbu itafanyika Aprili 11 na mazishi ya kitaifa yatafanyika Aprili 14. Tangu kifo hicho kilipotokea, umati wa watu umekusanyika nje ya makaazi ya Winnie wakiimba na kucheza nyimbo za kuomboleza.

Winnie aliolewa na Nelson Mandela kwa miaka 38, ambapo miaka 27 alikuwa mwenyewe bila mumewe ambaye alikuwa amefungwa gerezani. Wawili hao walitengana miaka miwili baada ya Nelson kuachiwa huru mwaka 1990 na waliachana rasmi mwaka 1996.

Winnie pia alitumikia vipindi kadhaa gerezani kutokana na harakati zake za kupinga utawala wa ubaguzi wa rangi na hata kuteswa na vikosi vya usalama vya serikali.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, AP, Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga