Vikosi vya jeshi vyapelekwa Jos, Nigeria | Matukio ya Kisiasa | DW | 08.03.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Vikosi vya jeshi vyapelekwa Jos, Nigeria

Watu kadhaa wakamatwa kufuatia mauaji yaliyoibuka jana huko Jos

default

Rais anayekaimu madaraka nchini Nigeria, Goodluck Jonathan.

Serikali ya Nigeria imepeleka vikosi vya jeshi katika mji wa Jos baada ya kutokea mapigano ya kidini hapo jana yanayodaiwa kusababisha vifo vya kiasi watu 500. Wanajeshi wameonekana wakifanya doria katika mji huo kwa lengo la kuzuia kuenea zaidi kwa mapigano hayo.

Kwa mujibu wa kamishna wa habari wa jimbo la Plateau, Gregory Yenlong, wanajeshi wanafanya doria hii leo katika mji wa Jos na kwamba watu kadhaa wamekamatwa wakihusishwa na mauaji hayo. Rais anayekaimu madaraka, Goodluck Jonathan, ameitisha mkutano wa dharura, na wakuu wa vikosi vya usalama vya Nigeria wanajadiliana kuhusu mikakati ya kuweka ili kuzuia kuenea kwa mapigano hayo katika majimbo ya karibu. Wakaazi wa vijiji vitatu vinavyokaliwa na Wakristo karibu na Jos wamesema wafugaji wa Kiislamu kutoka maeneo ya milimani yanayouzunguka mji huo walianzisha kile kinachoonekana kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi mapema jana, Jumapili, kufuatia mapigano mengine ya kidini yaliyotokea mwezi Januari, mwaka huu, ambapo inadaiwa kuwa zaidi ya watu 300 waliuawa.

Mtu aliyeshuhudia amesema alihesabu zaidi ya maiti 100 jana katika kijiji cha Dogo Nahawa, moja ya vijiji vitatu vilivyoshambuliwa, lakini watu wengine waliojeruhiwa walipelekwa hospitali mjini Jos na maiti nyingine zilizikwa mara moja hivyo kuwapa wakati mgumu maafisa kujua idadi kamili ya watu waliouawa. Hata hivyo, msemaji wa polisi wa Jimbo la Plateau, Mohammed Lerama, amesema idadi rasmi ya watu waliouawa hadi sasa ni 55. Lerama alisema ''Hadi sasa watu waliokamatwa ni 93, hao ni watu waliokamatwa mara moja baada ya mauaji kutokea katika eneo hilo na watu waliouawa ni 55 na tayari tumeshatoa taarifa kwa vyombo vya habari na uchunguzi wa awali umeonyesha kuwa haya ni mauaji ya kulipiza kisasi kufuatia mauaji ya mwezi Januari.''

Vurugu kubwa zilitawala zaidi katika kijiji hicho cha Dogo Nahawa ambako wafugaji wa kabila la Fulani, ambao wengi wao ni Waislamu, walianzisha mapigano hayo ambapo inadaiwa kuwa walitumia mapanga na mashoka dhidi ya wakulima wa kabila la Berom, ambao wengi wao ni Wakristo. Walioshuhudia mapigano hayo wamesema kuwa wanawake na watoto ni miongoni mwa idadi kubwa ya watu waliouawa.

Mauaji hayo yalaaniwa kimataifa

Wakati huo huo, serikali ya Ufaransa imelaani vikali mapigano hayo huku ikiwaunga mkono maafisa wa serikali ya Nigeria kwa hatua waliyochukua ya kurejesha hali ya utulivu katika mji wa Jos. Taarifa iliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ufaransa, Bernard Kouchner, imeeleza kuwa watu waliohusika na mauaji hayo lazima wachukuliwe hatua kali za kisheria. Katika hatua nyingine, Kanisa Katoliki duniani limeelezea masikitiko yake kufuatia mauaji hayo nchini Nigeria. Msemaji wa Vatikani, Federico Lombardi, amelaumu mauaji hayo, akisema kuwa vitendo hivyo ni vya kutisha. Aidha, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Abuja, Mhasham John Onaiyekan, ameiambia Radio Vatikani kuwa mapigano hayo hayajasababishwa na masuala ya kidini, bali ni kwa sababu ya tofauti katika masuala ya kiuchumi, kikabila, kijamii na kiutamaduni.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE)

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 08.03.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MNCp
 • Tarehe 08.03.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/MNCp
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com