1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Vifo vinavyotokana na mafuriko Ulaya vyaongezeka

Yusra Buwayhid
16 Julai 2021

Idadi ya vifo vilivyotokana na mafuriko ya maji katika maeneo ya magharibi mwa Ujerumani na Ubelgiji imeongezeka na kupindukia watu 100, huku mchakato wa kuwatafuta mamia wengine wasiojulikana waliko ukiwa unaendelea.

https://p.dw.com/p/3wZHX
Deutschland Schäden nach Starkregen in Ahrweiler
Picha: Abdulhamid Hosbas/AA/picture alliance

Mamlaka ya jimbo la Ujerumani la Rhineland-Palatinate imesema watu zaidi ya 50 wamepoteza maisha kwenye jimbo hilo, tisa wakiwa ni wakazi kutoka kituo cha kuhudumia watu wenye ulemavu.

Katika jimbo jirani la North Rhine-Westphalia, maafisa wamesema waliokufa wamefika 30, lakini wameonya kuwa idadi hiyo inaweza kuongezeka.

Hali kadhalika watu wengine wapatao 1,300 bado hawajulikani waliko nchini Ujerumani. Lakini maafisa wanasema juhudi za kuwatafuta zinakwamishwa na barabara zilizoharibika pamoja na mawasiliano mabaya ya simu.

Soma zaidi: Mvua kubwa na mafuriko yasababisha maafa nchini Ujerumani

Kwa upande wa Ubelgiji, idadi ya vifo imeongezeka hadi watu 14, huku wengine 5 wakiwa hawajulikani waliko hadi hivi sasa, kulingana na takwimu za awali zilizoripotiwa IjumaaI na maafisa pamoja na vyombo vya habari nchini humo.

Mafuriko hayo yametokana na mvua kubwa iliyonyesha siku kadhaa wiki hii, na kuzoa magari barabarani pamoja na kusababisha nyumba kadhaa kuporomoka.

Bad Neuenahr | Malu Dreyer und Olaf Scholz im Hochwassergebiet
Bad Neuenahr | Malu Dreyer katika eneo la mafuriko UjerumaniPicha: Thomas Frey/dpa/picture alliance

Nchini Ujerumani hali hiyo imepelekea maelfu ya watu kupoteza makazi yao kutokana na nyumba zao kuharibiwa na maji au wengine kuhamishwa kwenye nyumba zinazoonekana kuwa ziko hatarani kuanguka katika kipindi cha mvua hiyo kubwa.

Maafisa wameonya kwamba majanga ya aina hiyo yanaweza kuwa kitu cha kawaida kutokana na mabadiliko ya tabia nchini.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Marekani Joe Biden wameeleza jinsi walivyohuzunishwa na vifo hivyo katika mkutano na waandishi habari katika Ikulu ya Marekani White House Alhamisi ambako kansela huyo yuko ziarani.

Merkel amewahakikishia Wajerumani kuwa serikali iko pamoja nao.

""Naomba niwaambie watu wa Ujerumani: kuwa hatutawaacha peke yenu katika wakati huu mgumu na mbaya sana. Na tutawasaidia pia wakati wa ujenzi," amesema Merkel.

Aidha waziri mkuu wa jimbo la North Rhine-Westphalia Armin Laschet, ameitisha mkutano wa dharura na Baraza la Mawaziri hii Ijumaa. 

Mafuriko Ujerumani

Naye Malu Dreyer, waziri mkuu wa jimbo jirani la Rhineland-Palatinate, amesema maafa hayo yanaonyesha haja ya kuongeza juhudi za kukabiliana na ongezeko la joto duniani.

Jeshi la Ujerumani limetuma wanajeshi wapatao 900 kusaidia katika juhudi za uokozi kwenye maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko hayo.

Mafuriko hayo pia yameathiri maeneo ya Luxemburg, Uholanzi na Uswisi.

Vyanzo: (ap, dpa,)