Uturuki, Ufaransa, zatupiana lawama kuhusu Libya | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.06.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Uturuki, Ufaransa, zatupiana lawama kuhusu Libya

Uturuki imepuuzilia mbali "madai yasiyo na msingi" ya Ufaransa kuwa meli za kivita za Uturuki zimeonyesha uchokozi uliopitiliza dhidi ya manowari ya Ufaransa inayoshiriki katika operesheni ya NATO Bahari ya Mediterrania

Ufaransa imesema wanamaji wake walikuwa wanajaribu kuikagua meli ya mizigo walioishuku kupeleka silaha nchini Libya -- jambo lililopigwa marufuku chini ya vikwazo vya Umoja wa Mataifa. Afisa wa wizara ya ulinzi ya Ufaransa amesema meli za Uturuki zililenga rada mara tatu, hali iliyoashiria kwamba shambulizi la kombora lilikuwa linakaribia. Lakini afisa wa jeshi la Uturuki amesema meli ya Ufaransa ilifanya hila za kasi kubwa na hatari, ambazo zilikuwa zinakiuka sheria za usalama baharini na utaratibu wa NATO.

Mahusiano kati ya Ufaransa na Uturuki yameharibika katika miezi ya karibuni kuhusiana na hatua ya Uturuki kuiunga mkono serikali inayotambulika na Umoja wa Mataifa ya Umoja wa Kitaifa yenye makao yake mjini Tripoli. Hapo jana maafisa wa ngazi ya juu wa Uturuki walikuwa Libya na kukutana na serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya Uturuki kuisaidia kuzuia mashambulizi ya vikosi vya serikali ya upande wa mashariki. Mevlut Cavusoglu ni waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki

Der türkische Aussenminister Mevlut Cavusoglu

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Uturuki Mevlut Cavusoglu

Ufaransa inaituhumu Uturuki kwa kukiuka mara kwa mara marufuku ya Umoja wa Mataifa ya biashara ya silaha Libya ikisema kuwa Uturuki ndio kikwazo cha kupatikana mpango wa kusitishwa vita nchini humo.

Umoja wa Ulaya una operesheni ya majini katika Bahari ya Mediterania inayolenga kusaidia kutekeleza marufuku ya biashara ya silaha, lakini Uturuki, mwanachama wa NATO ambaye juhudi zake za kujiunga na Umoja wa Ulaya zimekwama, inashukuku kuwa inaegemea zaidi upande mmoja, kwa kuungazia utawala wa Libya unaotambulika kimataifa mjini Tripoli, ambao Uturuki inaunga mkono. 

Serikali ya Tripoli ikiongozwa na Fayez Sarraj inaungwa mkono na sio tu Uturuki, ambayo iliwapeleka wanajeshi na mamluki Januari kuulinda mji mkuu, lakini pia Italia na Qatar. Wanajeshi pinzani chini ya kamanda Khalifa Haftar, walioanzisha operesheni ya kuikamata Tripoli mwaka jana, wanaungwa mkono na Ufaransa, Urusi, Jordan, Umoja wa Falme za Kiarabu na nchi nyingine muhimu za Kiarabu.

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Josep Borell anajaribu kupata uungwaji mkono wa NATO kwa operesheni ya wanamaji ya umoja huo, lakini wanadiplomasia na maafisa wanasema Uturuki huenda ikapinga hatua ya aina hiyo. Borrell, ambaye atashiriki katika mkutano wa video wa mawaziri wa ulinzi wa NATO leo, amesema anatumai makubaliano ya ushirikiano wa Umoja wa Ulaya na NATO yanaweza kufikiwa haraka, kwa sababu kusaidia kuitekeleza marufuku ya silaha ni suala la maslahi ya usalama ambalo linaungwa mkono na jumuiya zote.