1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ushindi kwa Chama cha AKP cha waziri mkuu Erdogan katika uchaguzi wa bunge nchini Uturuki

24 Julai 2007

+Washindi wa uchaguzi huu wa bunge ni wananchi, mustakbali wetu na pia utulivu wa nchi yetu. Ushindi huu hautatufanya tuwe na vichwa vikubwa. Kinyume na hivyo. Ushindi huu unatufanya tuwe na dhamana zaidi. Hatutatetereka na kuachana hata nchi moja na misingi ya jamhuri yetu. Tutafanya kazi zaidi ili Uturuki iwe mwanachama kamili wa Umoja wa Ulaya na kuendeleza marekebisho yetu ya kidimokrasia.+

https://p.dw.com/p/CHAZ
Waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan(kushoto), na waziri wake wa mambo ya kigeni, Abdullah Gül.
Waziri mkuu wa Uturuki, Tayyip Erdogan(kushoto), na waziri wake wa mambo ya kigeni, Abdullah Gül.Picha: AP

Hayo ni maneno ya waziri mkuu wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, aliyoyatoa dakika chache baada ya kuwa wazi kwamba chama chake cha Haki na Maendeleo, AKP, kushinda katika uchaguzi wa bunge uliofanywa jumapili iliopita. Baada ya kuhesabiwa kura zote, amtokeo yanaonesha chama cha AKP kimejipatia asilimia 46.5 ya kura, hiyo ni asilimia 12 zaidi ya kura ilizopata katika uchaguzi wa mwaka 2002, hivyo sasa kuwa na viti 340 katika bunge la wajumbe 550. Chama cha Umma, CHP, kinachoongozwa na kiongozi wa upinzani, Deniz Baykal, na ambacho kimejengeka katika fikra za kijamhuri kimejipatia asilimia 21; kile cha kizalendo cha MHP ambacho kilikuwa hakiwakilishwi katika bunge liliopita kimeweza kuvuka kiunzi cha asilimia kumi ya kura kinachohitajiwa huko Uturuki ili chama kiweze kuingia bungeni. Mara hii kiempata asilimia 14.

Uchaguzi huu ulikuwa lazima uitishwe kwa vile waziri mkuu Tayyip Erdogan alishindwa kumfanya waziri wake wa mambo ya kigeni, Abdullah Gül, kuwa rais wa nchi hiyo kutokana na upinzani kususia kikao cha bunge cha kumchagua rais. Pia jeshi lilikuwa upande wa upinzani likihoji kwamba kuchaguliwa kwa Abdullah Gül, mtu anayejiambatanisha na imani za Kiislamu na mkewe ni mwenye kuvaa ushungi, kungehatarisha msingi wa katiba ya Uturuki yenye kutenganisha kabisa dini na serekali. Jeshi katika dola ya kisasa ya Uturuki, tangu ilipoanzishwa na muasisi wake, Kamel Ataturk, limejiona kwamba ndio mlezi na mlinzi wa katiba ya nchi hiyo. Katika miezi iliopita ya April an Mei, mamia kwa maelfu ya watu walikwenda mabarabarani kuiopinga serekali ya chama cha AKP. Hivyo uchaguzi wa mwisho wa wiki ulikuwa utanzuwe yale mabishano makali kama nchi hiyo iwe yenye sura ya kidini au isioambatana kabisa na dini. Matokeo ya uchaguzi yamempa haki Tayyip Erdogan na kudhihirisha kwamba wapigaji kura hawajashawishiwa na mabishano hayo, lakini zaidi na mambo muhimu zaidi, kama anavosema mbunge Lale Akgün wa Chama cha SPD hapa Ujerumani , ambaye ni wa asili ya Kituruki:

+Sivyo. Baada ya hapa kuweza kuiangalia vizuri kampeni ya uchaguzi na pia kuziangalia tena kwa undani programu za vyama, mimi siamini kwamba Chama cha AKP kitafuata siasa ya kuifanya Uturuki kuwa nchi ya Kiislamu, hisia hiyo haionekani miongoni mwa wananchi. Chama cha CHP pia kimeiona hali hiyo na kiliwachana na kampeni ya kuwatia wananchi hofu, kwa vile kiligundua kwamba kampeni kama hiyo haiwavutii watu. Watu walikuwa wana hamu ya kujibiwa masuali kama vile watakuwa na vipato gani, vipi ukosefu wa nafasi za kazi utakavokabiliwa, na vipi juu ya hali ya huduma za afya. Nafikiri mnamo miaka minne iliopita Chama cha AKP kilitoa majibu mazuri kwa masuali hayo.+

Bila ya shaka ushindi wa Tayyip Erdogan unatokana na sababu mbili: Uturuki hivi sasa inajionea uchumi wake ukin’gara sana, ukipanda kwa asilimia sita hadi tisa katika miaka ya karibuni, hali ambayo haijaonekana katika miaka kabla ya utawala wa Chama cha AKP.Pili: wananchi wamekasirishwa na jeshi la nchi hiyo hasa pale lilipotishia kwamba litafanya mapinduzi pindi mtu aliyetakiwa na waziri mkuu Erdogan kuwa rais wa nchi atachaguliwa. Mtu huyo, Abdullah Gül, hivi sasa amechomoza kuwa ni mtu anayependwa sana nchini humo. Pale Tayyip Erdogan alipkuwa akiwahutubuia wananchi katika siku hiyo ya ushindi mbele ya makao makuu ya chama chake, alipokelewa na miito ya wananchi waliokuwa wanapiga kelele kutkak Abdullah Gül awe rais wa nchi. Kama anavosema Hassan Cemal wa gazeti la kiliberali la MILLIYET:

+Hili ni jibu la wananchi dhidi ya jibu walilolitoa wanajeshi. Lakini hii haina maana kwamba serekali ivimbe kichwa.+

Lakini wachunguzi hawana hakika kama Tayyip Erdogan atapendekeza tena Abdullh Gül awe rais; huenda atajaribu kuepusha kutokea mikwaruzano mingine baina yake na wale wanashikilia dola na dini zitengane kabisa. Kazi ya kwanza ya bunge hapo wiki ijayo itakuwa kumchagua rais kuchukuwa nafasi ya sasa ya Rais Ahmet Nacdet Sezer, mtu aliyekibisha sana chama cha AKP. Akitambua mgawanyiko wa kisiasa ulioko Uturuki, Erdogan amewahikishia wale wanaomshuku kwamba anafanya njama ya kuibadilisha dola hiyo isioelemea katika dini. Alisema atatawala kwa niaba ya Waturuki wote, huku akimnukuu Mustafa Kemal Ataturk, muasisi anayeheshimiwa wa nchi hiyo. Nikimnukuu , alisema: kwa hisani yenu kuweni na hakika, bila ya kujali nani mnampigia kura, kura zenu zina maana kwetu pia. Tunaheshimu uchaguzi wenu…tuna dhamani na malengo ya pamoja yanayotuunganisha sote.

Alikula kiapo kwamba atasonga mbele na marekebisho ya kiuchumi na kisiasa yanayotakiwa na Umoja wa Ulaya ili nchi hiyo iweze kujiunga nao umoja huo. Lakini chama chake hakina wingi wa thuluthi mbili bungeni kwueza kuibadilisha katiba ya nchi, kwa hivyo itambidi ashirikiane na vyama vya upinzani katika masuala mengi.

Vyama vingine visivoelemea katika dini vimewea kuingia bungeni. Kiole cha CHP kikiw ana viti 112 na kile chenye siasa za kizalendo cha MHP kikiwa na viti 71. Wakurd ambao ni kabila la wachache katika Uturuki, karibu ya robo ya wakaazi milioni 70 wa Uturuki, wameweza kuikwepa ile sheria inayotaka chama iwe na asilimia kumi ya kura kuweza kuingia bungeni. Badala yake Wakurd, wanaoishi kwa wingi katika eneo la kusini mashariki ya nchi hiyo , wameweza kupata wabunge 27 wanaojitegemea. Bila ya shaka chama cha kizalendo kitapinga kutolewa haki zaidi kwa Wakurd na watu wa dini za wachache pamoja na kufanywa marekebisho mengine yanayotakaiwa na Umoja wa Ulaya, na kitamshikilia Erdogan atume majeshi hadi kaskazini mwa Iraq kuwaandamana na kuwaangamiza waasi wa Kikurd wa chama cha PKK ambao wana maficho yao huko.

Majeshi ya Uturuki yamekuwa yakipambana na waasi wa Chama cha PKK tangu mwaka 1984 katika mzozo uliochukuwa hadi roho za zaidi ya watu 30,000. Michafuko imezidi mnamo mwaka uliopita.

Kama wabunge wepya wa Kikurd watasababisha kuweko sura nyingine katika siasa za Uturuki na madai yao kuwa katika ajenda ya serekali mpya, Mehboob Khan anayeishi Istanbul aliniambia hivi:

Tayyip Erdogan anaweza akajihisi kama yuko fungate hivi sasa, lakini uwazi ni kwamba ana kazi kubw ambele yake, na sio kwamba wingi wa kura alizopata maana yake anaweza kufanya analotaka.