1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Uingereza yatishia hatua kali dhidi ya Urusi

Isaac Gamba
14 Machi 2018

Saa 24 zilizotolewa na Uingereza kuitaka Urusi kutoa maelezo kuhusiana na kuhusishwa kwake na shambulizi la sumu dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi umemalizika pasipo Urusi kueleza chochote.

https://p.dw.com/p/2uHzH
England Theresa May
Picha: picture-alliance/dpa/Pa/PA Wire

Uhusiano kati ya Uingereza na Urusi umezorota kwa haraka katika kipindi cha siku kumi tangu jasusi wazamani  Sergei Skripal na binti yake Yulia  waliposhambuliwa kwa sumu mjini Salisbury kaskazini magharibi mwa Uingereza.

Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May alisema hapo jana kuna uwezekano mkubwa  kuwa Urusi inahusika kwa njia moja au nyingine na shambulizi hilo kwa sababu imeshindwa kudhibiti sumu hiyo na kutaka  Urusi itoe majibu  katika kipindi cha saa 24 ambazo zimemalizika usiku wakuamkia leo.

Msemaji wa ubalozi wa Urusi mjini London amesema  Urusi haitatekeleza wito huo hadi pale itakapo pokea sampuli ya kemikali hiyo huku  pia  Urusi ikitoa mwito  kufanyika uchunguzi wa pamoja kuhusiana na  tukio hilo.

Msemaji wa ubalozi huo wa Urusi mjini London  ameongeza kuwa  Urusi haikuhusika na shambulizi hilo na kuongeza kuwa nchi yake itajibu hatua yoyote itakayochukuliwa kama adhabu dhidi yake kuhusiana na tuhuma hizo.  

   Bi Theresa May  amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya Urusi iwapo itashindwa  kutoa maelezo ya kina kuhusiana na tuhuma hizo kufikia usiku wa kuamkia leo Jumatano.

Hatua zinazofikiriwa ni pamoja na kuzuia mali za viongozi wa Urusi pamoja na maafisa wengine wa nchi hiyo , kuzuia Urusi kuwekeza katika masoko ya kifedha ya Uingereza pamoja na kuwafukuza wanadiplomasia wa nchi hiyo.

Waziri Mkuu Theresa May  anatarajia kuainisha hatua hizo katika bunge leo Jumatano  baada ya mkutano wa baraza la usalama la taifa.

        Uingereza yaomba ushirikiano kwa washirika 

Russland Präsident Wladimir Putin
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: Reuters/Kremlin/A. Nikolskyi

Uingereza pia inaripotiwa kutoa mwito kwa washirika wake wa nchi za magharibi kwa ajili ya ushirikiano wa pamoja juu ya sakata hilo.

Hayo yanajiri huku Umoja wa Ulaya ukiahidi kuipa ushirikiano Uingereza katika mzozo huo na Urusi.

  Ahadi hiyo iliyotolewa na makamu wa rais wa halmashauri ya Ulaya Valdis Dombrovskis ina kuja mnamo wakati kukiwa na wasiwasi  nchini Uingereza kuhusu ushirikiano wa kiusalama  baada ya nchi hiyo kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya mwishoni mwa Machi 2019. 

Naye msemaji wa mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Federeca Moghereni amelieleza shirika la habari la Reuters kuwa matumizi ya silaha za sumu katika jaribio la kuwaua raia nchini Uingereza  ni suala linalostua   hivyo  Umoja wa Ulaya unaungana na Uingereza  katika kuhakikisha haki inapatikana  na kuahidi kutoa ushirikiano itakapolazimu. 

Rais wa Marekani Donald Trump amemueleza waziri mkuu Theresa May kwa njia ya simu kuwa Urusi  inapaswa kutoa majibu  yasiyo kuwa na utata kuhusiana na jinsi gani  silaha hii ya sumu iliyotengenezwa  Urusi ilivyotumika  nchini Uingereza hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa ikulu ya White House.

 Akizungumza na waandishi wa habari Trump ameongeza kuwa pindi watakapo pata ukweli juu ya tuhuma hizo basi wataishutumu Urusi au yeyote anayehusika. 

Kwa upande mwingine waziri wa mambo ya nje wa Uingereza Boris  Johnson alizungumza na mawaziri wenzake wa Ufaransa na Ujerumani  pamoja na Katibu Mkuu wa NATO-  Jens Stoltenberg na kusema iwapo itathibiitishwa Urusi kuhusika na tuhuma hizo basi huu utakuwa ni uzembe unaotishia Jumuiya ya kimataifa.

Mwandishi : Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri       : Daniel Gakuba