Urusi yakataa madai ya kuwafadhili waasi mwaka 2014
8 Juni 2023Balozi Shulgin ametoa matamshi hayo mbele ya mahakama ya kimataifa ya haki iliyoko mjini The Hague akiyataja madai hayo kuwa ni "propaganda na uzushi" akitaka kesi hiyo kutupiliwa mbali kwani Urusi inakana madai yote na kwamba Ukraine haijatoa ushahidi wowote kuthibitisha shutuma hizo.
Soma pia: MH17: Hitimisho lenye utata kwa ajali ya ndege
Suala hilo linahusiana na kesi iliyofunguliwa na Ukraine mwaka 2017 katika mahakama ya Umoja wa Mataifa hata kabla ya uvamizi wa Urusi mnamo mwaka jana. Katika kesi hiyo Ukraine inaishutumu Urusi kwa kuwapatia silaha na fedha waasi wanaoiunga mkono Moscow katika eneo la Mashariki mwa Ukraine tangu mwaka 2014. Kwa kufanya hivyo Urusi ilikikuka mkataba wa kimataifa unaozuia ufadhili wa ugaidi, kulingana na madai ya Kyiv.
Moscow pia inashutumiwa na Ukraine kwa kudungua ndege ya abiria ya MH17 mwaka 2014 iliyowaua watu 298. Kwa mujibu wa madai ya Ukraine, ni kwamba Urusi iliwapatia waasi kombora la kuzuia ndege la Buk lililoidungua ndege hiyo aina ya Boeing, madai ambayo mawakili wa Urusi wameyakataa. Wakili wa Uingereza Michael Swainston anayeiwakilisha Urusi amesema kwamba "hapakuwa na kombora la Urusi la Buk" na kwamba ushahidi huo ni "upuuzi wa kidijitali usio na misngi".
Tukielekea Ukraine kwenyewe, mamlaka nchini humo zimesema raia mmoja ameuawa katika mashambulizi ya Urusi mjini Kherson wakati mkoa huo ukikabiliana na mafuriko makubwa yaliyotokana na kuharibiwa kwa bwawa kubwa la kuzalisha umeme kwenye eneo linalodhibitiwa na Urusi. Ofisi ya mwendesha mashitaka wa Kherson imenukuliwa ikisema kuwa mashambulizi hayo yametokea wakati wa kuwahamisha raia na raia wanne wamejeruhiwa katika kijiji jirani. Ukraine ilichukua tena mji mkuu wa mkoa wa Kherson mnamo mwezi Novemba lakini mji huo bado kwa kiasi unashambuliwa na Moscow.
Mapema leo Rais Volodymyr Zelenskiy ametembelea majimbo ya kusini yaliyoathirika na mafuriko ya Kherson na Mykolaiv kujadili juu ya opereisheni za dharura. Mkaazi mmoja wa Mykolaiv amesimulia masaibu wanayopitia.
"Nina wasiwasi na watu ambao wameketi kwenye nyufa za nyumba zao, walioachwa huko ambao hawawezi kuokolewa kwasababu wapo eneo linalodhibitiwa, watu hao wamejikalia tu wanasubiri kujifia. Hicho ndio kinaumiza zaidi. Tuna hofu kwasababu tumepitia mengi! mengi mno hata kiasi tunahisi hofu yetu kama imepungua."
Urusi kwa upande wake nayo inaishutumu Ukraine kwa kuwaua watu wawili wakati wa zoezi la kuwahamisha raia katika sehemu ya mji huo wanayoidhibiti. Nchi zote mbili zinatupiana lawama kwa uharibifu wa bwawa la kuzalisha umeme la Kakhovka siku ya jumanne na kusababisha mafuriko kutoka mto Dnipro.